Thursday, November 14, 2013

My article for newspaper: Jinsi ya kuchagua rangi za dari



Inawezekana umekuwa na fikra ya kuwa dari sahihi ni dari nyeupe. Miaka mingi iliyopita dari halikuwa linahusika kwenye muonekano maridadi wa chumba. Ilikuwa tu kwamba ni dari. Ipo ipo tu huko juu, ikijisikia wivu kila wakati kuta nyingine zinavyopakwa rangi na yenyewe kuachwa kama ilivyo.

Katika kuchagua rangi za kupaka dari ya chumba, msanifu wa majengo bwana Haji anasema kanuni za msingi ni hizi: Dari ambazo zina rangi za mwanga kuliko za kuta zina hisia za kuwa juu wakati zile za giza zina hisia za kuwa chini. Kabla ya kuamua rangi unayotaka kupaka dari, fikiria vyanzo na kiasi cha mwanga chumba hicho kinachopokea wakati ule unaokitumia zaidi. Kwa mfano, mwanga wa jua unaogonga kwenye dari ya rangi ya pinki au bluu ya anga inaleta burudiko la nafsi. “Mwanga wa taa unaogonga kwenye dari ya rangi nyekundu ya nyanya inazaa mng’ao mkali,” anasema Haji.

Funguka na usidharau  uwezo ambao dari inaweza kuwa nao katika muonekano wa chumba. Kuna rangi ambazo zinaweza kukifanya chumba kiwe kikubwa, kidogo, rasmi au cha kawaida. Dari mara nyingi inasahaulika kuwa ni kama ukuta wa tano wa chumba. Wakati wa kubuni nyumba wenye nyumba wengi wanaweza wasifikirie kuwa muonekano na mtindo wa dari unahusu. Ukichagua rangi za mwanga zitafanya chumba kionekane kikubwa na ukichagua rangi za giza zitakifanya ionekane kidogo. Na mchanganyiko wa rangi uwe ni za mwanga au za giza una matokeo fulani juu ya hisia za ukubwa na udogo wa chumba.

Chumba cha sebule kikubwa chenye dari ndefu kinaweza kuleta hisia za kutokuwa na uwiano kwa kuwa sakafu na fenicha zinachukua chini ya nusu ya eneo, ikiacha eneo lilolobaki bila kitu. Rangi iliyopakwa kwenye dari ya aina hii inaweza kusaidia kuleta hisia za dari kuwa chini, inapumbaza jicho kuwa chumba ni kidogo na cha faragha zaidi. Kwenye chumba chenye fenciha chache za kutawanyika, dari zilizopakwa rangi zilizokolea inakuwa kitovu cha jicho, kuhamisha jicho kutoka kule kusikokuwa na vitupio.

Vyumba vidogo au vile vyenye dari fupi, vinaweza kuonekana na msongamano. Rangi za mwanga kwenye dari zinafanya vyumba hivi vionekane vikubwa. Kigezo kikuu cha kufanya nyumba ndogo ionekane kubwa ni kwa rangi za dari na kuta kutotofautiana sana. Kwa mfano, ukuta wa bluu iliyokolea na dari nyeupe haziwezi kufanikisha kuleta hisia za kukuza chumba. Lakini rangi kama njano isiyokolea ya ukuta na dari ya rangi ya maziwa zitawezesha chumba kionekane kuwa kikubwa, kuwa na mwanga na hewa.

Nyeupe mara nyingi inatumika kama rangi ya dari kwa kuwa inakubaliana na walau kila rangi kwenye gurudumu la rangi. Nyeupe juu ya kichwa ina tabia ya kupotea machoni kwa hivyo macho yanavutwa zaidi kwenye kuta na fenicha kuliko dari na kuwezesha sanaa zako za ukutani zionekane zaidi, na kama kuta hizo zina rangi za mwanga dari inaonekana iko juu, na pia kama kuta zina rangi isiyokolea zinaleta hisia ya chumba kuwa kikubwa.

Kwenye vyumba vinavyopokea mwanga wa jua kidogo, dari nyeupe inasaidia  kudaka huo mwanga kidogo na kuusambaza chumba kizima. Kama ilivyo kawaida ya rangi yoyote, rangi nyeupe inahitaji ushirikiano na rangi nyingine zilizoko hapo chumbani iwe ni ukuta, zulia, malazi, mbao ama pazia ili isijejisikia kama haipo mahali pake.

Kampuni zinazotengeneza rangi zina rangi nyeupe za aina tofauti tofauti, kuna ambazo ni za kupoa na kuna ambazo ni za kuwaka. Kwa hiyo chagua ambayo ungependa kuleta kwenye dari yako.
Vile vile kuna baadhi ya rangi  mbali na nyeupe ambazo kwa kuzitumia kwenye dari zinaweka kukufanya mara moja kubadili fikra zako kuhusu muonekano wa chumba. Baadhi yake ni bluu ya anga, njano ya siagi na pinki ya kitoto.

Vyumba vinavyokuwa na rangi sawa na ya kuta na dari vinasaidia dari kuchanganyika vema na eneo la chumba lililobaki. Kutegemea na rangi ulizochagua, hii inaweza kusaidia kufanya eneo liwe dogo au kubwa. Kwenye hivi vyumba vya kufanana kuta na dari unaweza ongeza utepe wa rangi ya mwanga na pia gusa yale maeneo ya kiusanifu, hii italeta mvuto kwenye chumba. Ni wapi unapoanzia na kumalizia kupaka rangi? Je mikanda ya dari unaipaka rangi sawa na dari lenyewe?

Kubadilisha rangi pale ukuta unapokutana na dari kutaelekeza jicho kwenye chumba badala ya darini. Pia muonekano wa rangi hauji tu toka kwenye rangi, unaweza kufikiri pia kuweka paa la vipande vya mbao.

Rangi unayochagua kupaka dari ya chumba inaweza kubadili kabisa hisia zako, lakini kuwa makini isizidi: kwa maeneo yale ya msingi ndani ya nyumba, ambayo watu wanakua mara nyingi, weka rangi ya dari isiyo kali ili usiwe unaichoka.
 
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi ni mjasiriamali upande wa usafi wa mazulia, nguo na magari; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment