Zile nyakati ambazo luninga ya kichogo kuwekwa juu ya meza au kabati la sebuleni zinaelekea ukingoni. Teknolojia imefanya luninga za kisasa zisikalishwe juu ya fenicha ili kupata muonekano angavu kutoka kila pembe. Luninga za kileo zina kipengele cha kuifunga ukutani kusaidia kuhifadhi eneo, kuboresha mambo na kuwezesha watu kuona vizuri kioo cha luninga yao.
Tunapozungumzia luninga za kufunga ukutani ni aina ya plasma na LCD. Kwa siku za karibuni luninga hizi zimekuwa ni chaguo maarufu zaidi kwa wenye nyumba wengi kutokana na kuwa na muonekano angavu, pembe pana za kutazama na wigo mpana wa rangi.
Moja kati ya jambo kubwa kabisa kuhusu kufunga luninga ukutani ni sio tu nafasi unayohifadhi ukilinganisha na kama ungeweka juu ya meza au kabati au shelfu bali pia ni muonekano nadhifu kwa mapambo yako ya ndani ya nyumba. Kwa mfano kama ulikuwa unaogopa kuwa luninga yako mpya itachukua eneo kubwa na hata nafasi ya kukaa kuongea na wageni wako kwenye mazungumzo yasiyohitaji kutizama luninga, unaweza kuweka kiti kimoja au viwili vya ziada chini ya ukuta ambao luninga imefungwa. Wewe na wageni wako mnaweza kukaa na kufurahia ushirika wa kila mmoja, lakini kama fenicha zako za sebuleni ziko kwenye mpanglio wa macho kuelekea kwenye luninga mpya yenye mvuto basi mazungumzo yenu yanaweza kukosa kitu fulani kwa akili kuzingatia zaidi muonekano wa luninga kuliko mazungumzo. Hata hivyo bado utakuwa na sofa au fenicha zilizopangwa kuelekeza macho kwenye luninga wakati utakapotaka kuongea huku ukitazama luninga.
Kwa maneno mengine, pia unaweza kuweka baadhi ya shelfu za vitabu au meza ya kahawa na kuacha nafasi ya kati wazi kwa kuweka kila fenicha yako ya kukalia karibia na ukuta ilikofungwa luninga, kama unataka chumba kiwe na muonekano wa thieta ya nyumbani.
Unaweza ukafikiri ni kupoteza hela lakini luninga hizi za kufunga ukutani za plasma na LCD zina faida kwenye nyumba yako kwa hivyo usidharau. Teknolojia hii mpya sio tu kwa ajili ya muonekano angavu na mfumo bora wa sauti, ni kuwa hizi luninga za kioo kilicho flati na za kufunga ukutani zinawasaidia wenye nyumba wengi kutimaza upya nafasi ya sakafu iliyokuwa ikipotea, kwenye sebule, kwenye vyumba vya familia na hata kwenye vyumba vya kulala. Kufunga luninga ukutani ambayo inakufanya kuondokana na hilo kabati, meza ama shelfu la sebuleni inaweza ikaboresha sana nyumba yako kuliko hata hiyo luninga yenyewe.
Kuweza kufunga luninga ukutani unatakiwa kuwa na fundi anayejua jinsi ya “kucheza” na ukuta kwa maana ya kuutoboa au mseremala kuongeza mbao na fundi umeme wa kuunganisha waya za umeme na luninga na jinsi ya kuficha mrundikano wa waya na kebo. Kuna mambo muhimu ya kuzingatia kabla hujaamua kufunga luninga yako ukutani ambayo ni pamoja na kuamua ni ukuta upi unataka kufunga, waya zitakaa kaaje, muonekano, ukubwa na uzito wa luninga. Nyingi ya luninga hizi za plasma na LCD ambazo zinapendeza zaidi zikifungwa ukutani zina vifaa maalum vya kufungia ambavyo unatakiwa kununua kulingana na ukubwa na uzito wa luninga yako.
Katika kuamua ni wapi pa kufunga, fikiria ni wapi unapojisikia burudani zaidi wakati unapotazama luninga, unapendelea iwe juu ya usawa wa jicho ukiwa umekaa au iwe levo sawa na macho? Je unataka sauti kila mahali au ni eneo fulani tu la chumba. Kikawaida inatakiwa jicho lako liende katikati ya kioo cha luninga ukiwa umekaa. Unatakiwa kukaa raha mustarehe wakati ukitazama luninga. Pia, kuna uwezekano wa kuona picha vizuri zaidi kichwa kikiwa wima kuliko kikiwa kwenye pembe. Kama unapendelea kuifunga luninga juu basi iweke kwa pembe ambayo itainama kuelekea chini.
Kaa kwenye hilo eneo unalopendelea kukaa kutizama luninga na angalia ukutani pale ambapo una mpango wa kufunga luninga yako. Je kuna mwanga unapiga kinyume na eneo hilo? Kama ndio je unaweza kurekebishika tuseme kwa kufunga pazia labda au kwa kusogeza taa ya kuhamishika. Mwanga kinyume na luninga unaweza kusumbua na hata kuharibu muonekano wa picha, kwa hiyo kabla ya kufunga luninga yako kuwa makini na vyanzo vya mwanga vya eneo unalotaka kufunga.
Fahamu kwa kina mahitaji yako ya burudani. Vyumba vya thieta za nyumbani kwa mfano, vinahitaji spika sahihi kwa sauti sahihi. Mahali pa kuweka spika napo panahusika kwa spika mbili au nne kuhitajika kuwekwa mbele ya luninga. Na nyingine mbili kwenye kona nyingine za maeneo ya kukaa.
Baadhi ya luninga ni nzito sana kufunga ukutani kwa hivyo kama nyumba yako ni ya zamani sana au haina kuta imara, utatakiwa kuiseti juu ya fenicha. Ukubwa pia unahusika kwenye kufunga luninga ukutani kwa ajili nati maalum vya kufungia vinaweza kufanya kazi kwa luninga zenye uzito na ukubwa fulani. Haijalishi aina ya ukuta ilipofungwa, luninga inatakiwa iwe imefungwa imara kiasi cha kuzuia isianguke, na pia isicheze cheze hata kama iko karibia na mlango uliofunguliwa kwa nguvu. Kama huna uhakika na uimara wa kuta zako ni vyema kupata ushauri wa mtaalam.
Waya zinakaaje? Baadhi ya watu wanatoboa ukuta na kudumbukiza waya upande mwingine wa chumba ili kufanya chumba cha luninga kisiwe na mrundikano wa waya. Hata hivyo wengi wanapendeleaa kuwa na kila kitu yani luninga na waya kwenye chumba kimoja na kwa maana hiyo kuna jinsi ambayo fundi anaficha waya nyuma ya luninga iliyofungwa. Kuficha hizi waya inaweza kuwa ngumu au rahisi kutegemea na kiwango cha fundi cha utaalam na uvumilivu kwenye kufanya kazi yake. Ni vyema kufikiria jinsi ya kuficha/hifadhi waya zako kabla ya kuamua mahali pa kufunga luninga ukutani kwa kuwa kwa njia utakayochagua, eneo fulani la ukuta linaweza kufanikisha zaidi kuliko lingine.
“Luninga nyingi za flati hazina yale matundu ya kufungia ukutani
yakiwa wazi— yanakuwa yamezibwa na vifuniko vya plastiki, unachotakiwa ni kuchukua
bisibisi na kuyafungua”, anasema muuzaji Minja.
Walio wengi wanaweka
luninga zao za plasma au LCD juu ya stendi au meza au fenicha nyingine. Lakini
ni burudani gani iliyoko hapo? Moja ya jambo poa kuhusu kuwa na kuninga
isiyokuwa ya kichogo ni uwezo wa kuifunga moja kwa moja ukutani! Luninga ya
flati iliyofungwa ukutani ni mvuto wa mtazamaji. Pamoja na picha maridadi na
sauti ya kiwango, luninga ya plasma au LCD inaleta mvuto na unadhifu wa
muonekano wa chumba, hata hivyo nyaya na kebo za umeme zinazozagaa zinaweza
kuharibu picha ya unadhifu ambao luninga za flati zilizofungwa ukutani
zinasababisha.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi ni mjasiriamali upande wa usafi wa mazulia, nguo na magari; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment