Masika yanaanza, safisha mifereji kabla
haijasafisha mifuko yako
Kusafisha mifereji ya maji iliyojengewa kwenye nyumba (gutter) ni moja kati
ya kazi muhimu za kufanya kipindi hiki ambacho masika yanaanza. Japo mara nyingi huwa jambo hili inachukuliwa kijuu juu
tu, kwa bahati mbaya wengi wetu tunasubiri hadi madhara yatokee ndio
tunafikiria kusafisha mifereji ya nyumba zetu. Kuchelewa kuondoa majani ya miti
yanayodondoka na kuingia ndani ya mifereji ya nyumba pamoja na vumbi
kunasababisha matatizo makubwa mara mvua zinapoanza. Na hivyo kufanya kazi ya
kusafisha iwe ngumu na kubwa zaidi. Majani yaliyoozea ndani ya mifereji pamoja
na tope linalosababishwa na vumbi hukutana na maji ya mvua na kufanya tope
kubwa zaidi linaloziba mfumo mzima wa usafirishaji maji ndani ya makazi
yetu.
Kama utasafisha mifereji ya maji kwenye
makazi yako mara kadhaa kwa mwaka, hasa wakati wa miti kudondosha majani,
usafishaji utakuwa rahisi. Mara moja pekee au kuacha kabisa, inaweza kuja kuwa
kazi kubwa ambayo itakugharimu hela nyingi kwa shida zitakazotokana na
kutosafisha huko.
Tatizo la mifereji iliyoziba ni kuwa maji ambayo yanasimama yanaharibu ukuta
wa nyumba. Mifereji ya maji iliyojengewa kwenye nyumba yako imebuniwa kusukuma
maji yaende chini kutoka kwenye paa yaende mbali na nyumba na msingi wake kwa
ajili ya ukaukaji wa haraka wa maji maeneo yasiyohitajika kusimamisha maji au
kuwa chepechepe. Maji yanayobaki yamesimama kwenye mifereji iliyoziba
yanatafuta njia na kuweza kupenya kwa kupitia eneo lile ambalo ni dhaifu zaidi wakati
yakijitahidi kuondoka, na hii inamaanisha kuwa yanaweza kukimbilia moja kwa
moja kwenye ukuta na dari la nyumba yako.
Tatizo la kwanza kabisa la mifereji iliyoziba kwa majani na tope ni
kuongezeka uzito. Hayo majani yaliyooza yakiloa, yananyonya maji ya mvua kama sponji na yanakuwa mazito haswaa. Mzigo huu unaweka
msongo kwenye mifereji na vishikizo vyake na hii inaweza kuangusha mifereji
toka kwenye nyumba. Mifereji iliyoanguka ni gharama kuweza kuirudishia tena,
zaidi ya hayo taa au vioo vya dirisha vinavweza kuvunjika wakati mfereji
ukiporomoka chini.
Maji yanayofurika kwenye mifereji yanaharibu rangi ya nyumba na pia
michirizi ya maji inafanya alama kwenye kuta. Maeneo yenye mbao mirefeji
ilikopita nako kunaozeshwa na maji yaliyoziba na kuanza kuvuja.
Msingi wa nyumba na sakafu zenye nyufa ni dalili nyingine pia za mifereji
iliyoziba. Kama kwa kipindi kirefu maji
hayataondoka kwenye msingi wa nyumba kuelekea sehemu yalikoelekezwa yanaweka
kuangusha nyumba.
Sasa ni nini unachohitaji ili kufanya kazi hii ya kusafisha mifereji? Unahitaji
vitu vichache kuendana na njia utakayochagua. Ila dhana kuu ni rahisi, ni
kuchukua ngazi na kuvuta takataka toka kwenye mifereji. Unahitaji ngazi, ndoo
ya kuwekea uchafu, mpira wa bustani na kama
utapenda pia glavu.
Ondoa taka kutoka kwenye urefu wote wa mfereji na weka kwenye ndoo kwa ajili
ya kwenda kutupa na baada ya hapo fungulia maji kwa kutumia mpira wa bustani ili
kuondoa uchafu mdogo mdogo uliobaki. Hakikisha maji yanapita bila kikwazo na
huu pia ni wakati mzuri wa kuona kama mifereji
yako ina popote panapovuja kwenye kona au maungio. Kama
kuna mahali panapovuja unaweza ukanunua silikoni ya kuzibia na kwa urahisi tu
ukapaziba. Kumbuka kuwa maji yanatembea kufuata sehemu rahisi kupitia kwa hivyo
ukiwa na mfereji unaovuja ni sawa tu na kuwa na mfereji ulioziba.
Kama unapenda sana
unadhifu unaweza ukapaka nje ya mifereji yako rangi kufanya nyumba yako
ionekane mwaa.
Makala
hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi ni mjasiriamali upande wa usafi wa
mazulia, nguo na magari; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya
nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment