Siku moja baada ya Katibu Mkuu wa Chadema,
Dk Willibrod Slaa kuzungumza na mwananchi na kusema yupo salama, mke wake,
Josephine Mushumbusi amekanusha tuhuma zilizozagaa kuwa ndiye aliyemshauri
kiongozi huyo wa Chadema kujiuzulu na kumzuia kushiriki vikao muhimu vya chama.
Tetesi hizo zilivuma kwenye mitandao ya kijamii na vyombo
vya habari baada ya Dk Slaa kutoonekana katika vikao muhimu vya Chadema na
Ukawa, kuwa Mushumbusi hakupendezwa na kitendo cha Lowassa kupitishwa kuwania
urais chini ya mwavuli wa Ukawa na badala yake alitaka Dk Slaa ndiye awe
mpeperusha bendera.
Kwa mujibu wa taarifa hizo ambazo Mushumbusi
amezikanusha, aliamua alimfungia ndani Dk Slaa kama moja ya mbinu za kumzuia
asishiriki shughuli za kichama, tuhuma ambazo amezikanusha.
“Bosi wako akija kukuomba ushauri utamsaidia, lakini
akija akakuambia ameshafanya maamuzi unaweza kupingana naye?” alihoji
Mushumbusi akianza kutoa maelezo yake na kuendelea:
“Wakati wa vikao nilikuwa namwona (Dk Slaa) anachelewa
kurudi kila siku, siku moja akaja akaniambia uamuzi aliouchukua na mimi sikuwa
na la kusema, nikachukua shuka nikajifunika.”
Katika mahojiano yake ya kwanza na Mwananchi baada ya
kuzagaa kwa tetesi hizo, Mushumbusi pia alikana kumfungia Dk Slaa ndani ya
nyumba, akisema wakati maneno hayo yalipokuwa yanazagaa, alikuwa nje ya nchi na
wala hakujua kinachoendelea.
“Mwenyewe najiuliza nini kinaendelea, siwezi kufanya kitu
kama hicho. Nyumba yangu ina milango miwili, nawezaje kumfungia mtu, tena
mwanamume, hata watoto siwezi kuwafungia. Kuna mambo mengine mwanamke huwezi
kuyafanya kwa mwanamume. Mwanamume ni mwanamume tu,” alisema.
Alisema viongozi wa Chadema, ndugu, jamaa na marafiki
walikuwa wanafika nyumbani kwake na walikutana na Dk Slaa na kuzungumza naye...
“Kama ningekuwa nimemfungia wangezungumza naye vipi?”
Mushumbusi alisema mwanamke anaweza kufanya chochote
lakini kuna baadhi ya mambo ambayo mwanamume akiamua ni vigumu kumzuia.
Akifafanua tuhuma za kumshinikiza Dk Slaa kujiuzulu
Chadema, Mushumbusi alisema kiongozi huyo wa Chadema ana uamuzi wake na yeye ni
msaidizi tu ambaye hana uamuzi wa mwisho kwenye familia.
Hata hivyo, alisema endapo angeamua kumshawishi, uwezo wa
kufanya hivyo anao lakini yeye ni mwanamke mwadilifu anayependa mafanikio ya
mumewe.
“Kwani unanionaje? Mimi ni ‘strong’ (nina nguvu),
ningetaka ningefanya hivyo, nisingeshindwa,” alisema.
Pamoja na hayo, Mushumbusi alilalamika kuwa tuhuma hizo
dhidi yake zimesababisha asisikilizwe kama ilivyokuwa awali.
Bila kufafanua kwa undani, alisema kuna kundi linalounda
propaganda hizo ili abadili mtazamo kuhusu mumewe lakini jambo hilo haliwezi
kutokea.
“Nilisema nitampenda kama alivyo, sitajali chochote wala
akiwa katika hali gani au chama gani. Kazi yangu ni kumtia moyo ili kile
atakachofanya kifanikiwe,” alisema.
Anauza mkaa
Mbali na kukanusha vikali tuhuma hizo, Mushumbusi alisema
alikwishajitoa kwenye masuala ya siasa kwa miaka miwili sasa na badala yake
ameamua kufanya biashara ya kuuza mkaa.
“Nimenyamaza kimya, nimekaa kando ninaendelea na biashara
yangu ya kuuza mkaa, nipo mbali na siasa na sitaki kujua kinachoendelea, kwanza
hata mchakato wenyewe siujui,” alisema.
Aliwashauri wanawake kuacha kushabikia masuala
yanayotokea ndani ya ndoa yake na kuwataka wavae viatu anavyovivaa na wajue
kuwa anapitia wakati mgumu.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment