Thursday, August 27, 2015

Unapoenda dukani kununua mapambo ya kiutamaduni fahamu dondoo hizi

Mandhari nzuri ya mapambo ndani ya nyumba ni ile ambayo inahakikisha umezungukwa na vitu na rangi ambazo unazipenda. Uwezo wa kuweka pamoja vitu hivi, kwa jinsi ambayo vileta muonekano wa kuvutia sio lazima iwe ni kitu cha kuzaliwa nacho.

Huenda unatafuta vesi za maua za asili ya kichina zenye michoro na rangi nzuri au mapambo ya ukutani ya wanyama wa asili ya mbuga za Kitanzania, ndoto yako ya kupamba nyumba yako kwa namna hii inaweza isiwe rahisi kutimiza.

Hata hivyo chukua tahadhari; nimeongea na Asna Mshana ambaye anauza mapambo ya asili kwenye duka la kitalii Arusha kwa zaidi ya miaka 20 na hapa anatuelezea dondoo za kuzingatia unapoenda kununua mapambo ya aina hii ili uweze kuwa na matokeo unayoyataka:

Unaponunua mapambo yenye asili ya kiutamaduni iwe ni makubwa au madogo hakikisha unanunua yale yenye ubora.

Nunua pambo ulilolipenda bila kuzingatia fasheni na fahamu ni wapi unaenda kuliweka ndani ya nyumba yako kabla hujalinunua, kupamba kwa vitu vya kiutamaduni kunahitaji umakini.

Kuwa makini unapogusa vitu, kuna mapambo ambayo ni rahisi kuvunjika au kunyofoka kwahivyo unaweza kuharibu na ukatakiwa ulipe.

Kuwa na muda wa kutosha kwani baadhi ya maduka yanayouza vitu vya kitamaduni hayajaweka vitu hivi kwenye mpangilio kwahivyo unahitaji muda wa kuchagua. Kama kuna kitu unahitaji na hukioni, muulize muuzaji kama wanacho. Anaweza kukuelekeza vizuri.

Kuna baadhi ya vitu mwanga wa dukani unaweza kukupoteza, kama ni hivyo basi omba kukitoa  nje ili uweze kuona rangi yake halisi.

Labda unanunua kichwa cha mnyama chenye manyoya, uliza jinsi ya utunzaji na usafishaji wake.

Zaidi ya yote huhitaji kununua mapambo ya kiutamaduni kwa mkupuo. Kumbuka kuwa kupamba kwa vitu hivi kunaweza kukufanya teja kwa maana ya kwamba kununua tena na tena, kwahivyo usiwe na haraka ya kununua vingi kwa wakati mmoja. Ni juu yako kuamua ni nini unataka kwa wakati husika na ni kwa namna gani utakihusisha na nyumba yako


Makala hii imeandaliwa na Vivi, kwa maoni au maswali tuma kwenye barua pepe viviobed@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment