Friday, March 31, 2017

FAIDA YA SOFA ZA NGOZI


 Awali ya yote nitangulie kwa kusema kuwa endapo unahusika na bidhaa au huduma ihusianayo na nyumba na ungependa tufanye mahojiano tafadhali nijulishe kwa simu 0755 200023.

Ingawaje kuna wigo mpana wa malighafi za sofa kama vile vitambaa na jamii ya plastiki, ngozi imebaki kuwa ni chaguo la kifahari zaidi kwa ajili ya sofa. Hizi ni sababu tano za kwanini watu wanaopenda sofa nzuri na zenye ubora wa hali ya juu wanapendelea kuchagua za ngozi.

Ubora
Kama umesawahi kutembelea sebule au ofisi ambayo sofa zake ni za ngozi unajua hisia unayopata. Hakuna sofa zinazoonekana ni bora za kiwango na
kifahari kama za ngozi, anasema Festo William wa kampuni ya Furniture Center. Utengenezaji wa kisasa wa sofa za ngozi unazifanya zisiweze kuonyesha mipasuko, kusagika au kubanduka. Sofa inatulia na kuonekana imejaa vyema.

Burudiko
Kama vile ambavyo sofa na viti vya kitambaa vina tabia ya kupauka, vinapoteza umbo na ubora wake na kuonekana kuchoka na kuchakaa. Kwa upande wa sofa za ngozi kadri zinavyozidi kuzeeka, ndivyo ngozi yake inavyozidi kuwa laini na kukupa burudiko zaidi. Badala ya kuonekana kuchoka, ndiyo kwanza zinazidi kuvutia. Tofauti na vitambaa ni kwamba ngozi inapumua. Kwa maana ya kwamba inapokea joto na baridi kwa haraka sana kwa maana hiyo mara moja unajisikia burudani kuzikalia. Kutokana pia na kuwa na uwezo wa kunyonya na kuachilia hewa huwa sofa hizi hazishikamani na ngozi ya mkaaji hata pale ambapo ndani kuna joto kali kama ambavyo ingefanyika kwa malighafi zitokanazo na jamii ya plastiki kama vile sofa za PVC.

Uimara
Wataalam wanakadiria kuwa sofa za ngozi zinaweza kudumu mara nne zaidi ya zile za kitambaa. Ngozi ni ngumu lakini ni laini, ikimaanisha kwamba kiasili inakataa kuchanika.  Pia haizamishi uchafu mkavu au wa vimiminika. Mara nyingi sofa za ngozi zinasafishika kirahisi tu kwa kuzifuta na kitambaa kilicholoa maji.

Muonekano
Bwana Festo anasema kuwa sofa za ngozi zinakuja kwa rangi nyeupe, nyeusi na damu ya mzee. Rangi hizi hazichuji na pia kwa kuwa haziegemei upande wowote ni rahisi kuendana na rangi za vitu vingine vya ndani.

Gharama
Watu wengi wanaamini kuwa sofa za ngozi ni gharama kubwa mno. Ni kweli, lakini ni vyema kujua kuwa hii ni gharama ya mara moja ambayo ni vyema ukakumbuka kuwa zitakaa muda mrefu kuliko za aina hiyohiyo lakini za kitambaa. Mwisho wa siku sofa za ngozi ni kitu cha kudumu maishani.

Zaidi ya yote ni kwamba hazibebi vumbi na mizio kama vitambaa. Kwa mwenye nyumba ambaye anataka sofa zenye ubora na muonekano wa kifahari bila shaka sofa za ngozi ndio chaguo lake.

No comments:

Post a Comment