Thursday, September 19, 2013

my article for newspaper: makosa yanayokufanya uonekane wa umri mkubwa



Baadhi ya makosa ya mitindo na urembo ambayo yanakufanya uonekane wa umri mkubwa zaidi ya ulio nao

Wanasema uzuri uko machoni mwa mwonaji. Ingawa hiyo yaweza kuwa kweli,  kuna dhana za ujumla za urembo ambazo walimwengu wamekubaliana nazo. Kwenye tamaduni nyingi watu wanapendelea kuwa na umri mdogo kwa kipindi kirefu kwa sababu wanaamini kuonekana mdogo kiumri kunapasisha kuonekana mrembo.

Kwa hivyo kwanini ufanye chochote ambacho kitakufanya uonekane mzee? Wakati pekee ambao mtu anatamani kuenekana mkubwa ni wakati anapokuwa mdogo. Ndio, wote tunajua kejeli hii.

Wanawake wanatumia muda, nguvu na hela nyingi kuonekana warembo. Na zaidi ya hayo, wengi wanajaribu kwa nguvu kula na kuishi vizuri ili wanaokane na ngozi changa. Ila kwa bahati mbaya, kuna makosa machache ambayo mwanamke anaweza kuwa anafanya ambayo kusema kweli yana mfanya aonekane mkubwa zaidi ya umri wake.

Labda ni wanawake wachache sana au hata pengine hamna ambao kwa makusudi watavaa kitu cha kuwafanya waonekane wanene. Lakini utashangaa ni wanawake wangapi wanavaa mitindo ambayo inawafanya waonekane wa umri mkubwa. “Sio tu mashauzi ambayo yananifanya nitake kuonekana wa umri mdogo, ni kwa ukweli kuwa sijisikii kuzeeka ndani, sasa ni kwanini  niwe na muonekano wa uzee kwa nje?”anauliza Bi Eunie ambaye anamiliki duka la kuuza nguo za wanawake.

Ni kweli huenda unahitaji miwani ya kusomea, lakini kama ukiivaa ikalalia ncha ya pua yako itakufanya uonekane umri umesogea. Hakuna mwanamke atakayeonekana wa umri mdogo akiwa na hiyo miwani midogo ya kusomea ambayo inaning’inia kwenye pua. Na hiyo kamba iliyounganishwa nayo pia ipo? Nayo inakufanya uonekane mzee pia. Kama ni lazima uvae miwani ya kusomea hakikisha ni maridadi hasa rangi ya fremu zake.

Baadhi ya wanawake wanapenda kuweka nywele zao rangi, na hapa naenda kupata upinzani mkubwa toka kwa wanawake wote wanaochagua kuwa na nywele za rangi tofauli na ile ya asili, lakini ukweli ni kwamba rangi ya kwenye nywele inakufanya uonekane wa umri mkubwa tofauti na ulio nao. Na hiki ndio kitu  wanawake wengi hawakitaki. Labda utakapokuwa mtu wa makamo itakuwa poa kuwa na nywele za kijivu lakini kwenye umri wa kati (ambapo vitabu vya dini vinasema umri wa kuishi ni miaka 70 na ukiwa na nguvu 80) unataka uwe kijana iwezekanavyo. Sio kwamba nywele za rangi hazikufanyi mrembo (kuna wanawake wengi wanaonekana warembo na nywele hizi) ni kuwa hazitakufanya uonekane kijana. Chaguo nzuri la rangi za nywele kwa umri wa kati ni zile zitakazoendana na uchanga wa ngozi yako.

Unapoweka nywele zako rangi na madawa mengine ya kuzindoa toka asili yake unaziharibu polepole. Hii ni ukweli hasa kama inafanyika kila wiki. Nywele zilizokaangwa na kukaangwa zinakupelekea kwenye muonekano wa mbali na ujana. Punguza kwenda saluni na kuweka nywele rangi mara kwa mara, utatunza nywele na hela! Pia staili ya nywele unayochagua inachochea muonekano wako. Kadri umri unavyosonga na wewe unataka uzidi kuonekana kijana nywele ndefu za kunyooka hazitakufaa kama ulivyokuwa wakati wa ujana wako. Nywele nyefu zilizonyooka za kulala zitachochoea muanguko wako na umri kuonekana umeenda bila kuonyesha ujana kwenye uso wako.

Kuvaa soksi na raba na nguo yoyote ambayo sio ya michezo au mazoezi itakufanya uonekane wa umri mkubwa kuliko ulionao. Unajua wabibi wanavyopenda kuvaa raba na soksi na nguo yoyote hasa mikoa ya baridi. Pia kuvaa zile soksi ndefu (stockings) na sandals au viatu vya wazi vinakutoa kwenye ujana. Badala ya kuvaa soksi hizi paka miguu yako mafuta mazito. Hii itafanya miguu yako inawiri na kuonekana na afya njema. Na kama ni kipindi cha baridi vaa stokings za kuangaza na viatu vya kufunika vidole.
Nyeusi inafanya maajabu kupunguza unene na inafaa kwa kila tukio, lakini kadri mwanamke umri wake unavyoenda rangi ya ngozi inafifia—na kuvaaa nyesi inaweza kuleta mpishano wa rangi na kusisitiza mikunjo ya ngozi na kuelekeza macho ya mwonaji kwenye mikunjo myeusi inayozunguka macho na chini ya mashavu. Ili uweze kuonekana kijana kwa rangi nyesi inabidi utupie mtandio wa rangi kali au mkufu—rangi yoyote kali itapunguza makali ya ile mipishano ya kufifia kwa ngozi na nguo nyeusi.

Kitambaa cha jeans kimekaa kiujana zaidi. Kuna zile suruali zilipendwa za jeans za kupanda juu hadi kufunga tumbo lote zikitaka kukaribia kifuani ambazo ni maarufu kama suruali za mama. Wamama na wasichana wengi walizipenda kwa ajili zilisaidia kubana matumbo yao. Kuzivaa hizi pamoja na mavazi mengine yoyote makubwa kuliko mwili wako yatakufanya uonekane umri umeenda.

“Kuvaa sidiria iliyolegea kutakufanya uonekane mfupi, mzee na mzito” anasema Bi Rehema Moshi ambaye ni mmiliki wa duka linalouza nguo za ndani za kina mama. Anasema ukitaka kununua sidiria mpya ili kujua kuwa ni ya ukubwa sahihi kwako basi hakikisha unaanza kuifungia kwenye zile hook za mwanzo. Kadri siku zinavyoenda itavutika kwa hivyo itabidi ufungie hook za karibu kwa ajili ya kuikaza. Pale itakapofika ukaivalia kwenye huku ya kukaza kuliko zote basi hapo utajua unahitaji sidiria mpya. Kwa kuwa ukubwa wa matiti unabadilika badilika kuendana na kuongezeka ama kupungua uzito pamoja na mabadiliko ya homoni, Moshi anashauri kununua sidiria mpya kila baada ya miezi sita. Kuvaa sidiria ambayo haikupi msaada wa kutosha kunyanyua matiti itakufanya kuwa na muonekano wa umri ulisogea.

Sasa nakugeuzia kibao msomaji wangu. Nataka kusikia toka kwako. Tafadhali niandikie kosa namba moja ambalo litamfanya mwanamka aonekane wa umri mkubwa kuliko alio nao.

Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi ni mjasiriamali upande wa usafi wa mazulia, nguo na magari; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment