Thursday, September 5, 2013

My article for newspaper: mlango wa mbele



Jinsi ya kupata mlango sahihi wa mbele wa nyumba yako

Mlango wa mbele wa nyumba ni sehemu muhimu ya ni jinsi gani watu wanakuchukulia na kutegemea ni nini watakachoona watakapoingia nyumbani kwako. Mlango maridadi unapeleka ujumbe mkubwa na hisia ya kujisikia vizuri kwa yeyote anayekaribia makazi yako. Lakini zaidi ya umaridadi milango ya kuingilia lazima iwe imara sawa kuhimili upepo, mvua, jua, wavamizi, wakati huo huo ukiwa mariradi  vya kutosha kwa hisia nzuri za mwanzo. Kwa bahati mbaya kuweza kupata mlango wa kukidhi viwango vyote hivi si kazi ndogo. Mlango wa mbele wa nyumba unachukua sehemu kubwa ya muonekano wa nyumba kwa hivyo ni muhimu kuweka mlango sahihi wa kuendana na hadhi yako. Mlango ukidhi viwango vya ulinzi na uweze kufunga na kufunguka bila kikwazo.
Kwenye makala hii utapata dondoo za jinsi ya kuchagua mlango sahihi wa mbele kwa ajili ya nyumba yako ambapo sikuzote ukiuangalia utabaki unajiamini kwa uamuzi wako huo.

Amua kama unataka mlango wa mbele wa mbao, kioo, chuma au vyote kwa pamoja. Ingawa kuwa na mlango wa mbele wa kioo itaruhusu mwanga mwingi wa jua na pia unaweza kuwa maridadi zaidi, unamshawishi zaidi mwizi kuvunja na kuingia kuliko ule wa mbao au chuma. Kama utaamua bado kuweka mlango wa kioo wa mbele wa nyumbani basi weka vioo vya kiboksi kidogodogo badala ya kioo kimoja kikubwa cha moja kwa moja na pia kioo kisiwe karibia na kitasa ili kuepuka kuvunjika au kmrahisishia mwizi kuvunja na kufungua loki.

Unatakiwa kuwa na uhakika kuwa staili ya mlango uliyochagua itaendana na muonekano uliobaki wa nyumba yako. Unaweza ukapiga picha ya nyumba na kuipeleka kwa wauzaji au watengenezaji wa milango ya mbele ya nyumba ili waweze kukushauri ni mlango gani utakaokufaa. Pia kwa kupata mawazo juu ya staili mbalimbali za milango ya mbele ya nyumba zilizopo unaweza kutembelea kwenye mitandao na majarida ya ubunifu wa nyumbani.

Oanisha rangi za mlango wa mbele na ya ukuta wa nyumba au dirisha. Kumbuka kuwa unataka mlango wako wa mbele uonekane zaidi ya vingine. Mlango wa chuma ni imara zaidi na bei nafuu ukilinganisha na wa mbao ngumu ila unaweza kubonyea na kupata mikwaruzo zaidi ya wa mbao.  Ukishafanya utafiti na kupima faida na hasara za kila aina ya milango ambayo ipo sokoni utakuja na uamuzi ambao utakuwa sahihi kwa muonekano na hisia juu ya mlango wa wa mbele wa nyumba yako.

Mlango wa mbele wa mbao ngumu ni chaguo la watu wengi na na ndio maarufu zaidi kwenye nyumba nyingi.  Kama utaamua kuchagua mlango wa mbele wa nyumba wa mbao basi ongeza urembo kama vijinafasi kwa vioo iwe ni vya kuficha ama vya wazi ambavyo vinapatikana kwa ukubwa wowote utakaotaka. Na kama hofu ni mwizi kuvunja basi unaweza kuweka chuma kwa ndani lakini epuka kuweka vioo hivyo karibia na kitasa kwani utamrahisishia mwizi kazi yake! Zaidi ya umaridadi pia hivi vipande vya kioo utakavyoweka vitasaidia kuongeza mwanga wa jua ndani ya nyumba.
Milango ya mbele ya nyumba inapatikana kila mahali iwe ni ile iliyotengenezwa tayari au hata kama ni ya kutoa oda utengenezewe. Watengenezaji watakufanyia staili yoyote unayotaka kwa hivyo unaweza kubuni mlango wako mwenyewe. Kwa vile umeweka oda ya kutengenezewa basi inaweza kufikia hadi wiki mbili kabla ya kuweza kuupata mlango wako.

Uamuzi muhimu zaidi ni swali kwamba mlango wako umetengenezwa kwa mbao gani? Mlango wa mbele unafaa uwe umetengenezwa kwa mbao ngumu kama mkongo au mninga. Mkongo ni mzuri zadi kwani mninga una madoa doa mengi ambayo yanaweza kuwa kero. Uzuri wa mbao ni kuwa unaweza kuweka urembo wowote na mtindo wowote unaotaka. Ule muonekano wake wa asili hata kabla ya kupaka rangi tayari ni maridadi. Uwe na kati ya shilingi laki saba hadi  milioni moja kwa mlango wa mbele uliokamilika kwa maana ya mlango wenye fremu na bawaba kabla ya kitasa.

Mlango wa mbele uendane na ukubwa wa nyumba. Dondoo hii ya muhimu huwa inasahaulika na huenda ulishaona nyumba kubwa pengine hata ni ya ghorofa moja lakini ina kimlango cha mbele kidogodogo ambacho kingekuwa sahihi kwa nyumba ndogo. Mlango wa mbele ufunguke vizuri bila kikwazo, rangi maridadi na kitasa imara. Usisahau kuloki mlango wako wa mbele. Hata email zina loki ambayo ni neno la siri sembuse loki imara ya mlango wa mbele wa nyumba yako!

Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi anajishughulisha na usafi wa mazulia na nguo; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023

No comments:

Post a Comment