Hatua ya kwanza ya kuandaa kuta zako kabla ya kupaka rangi ni kuondoa fenicha zote ambazo zinahamishika kirahisi kutoka kwenye chumba. Funika kwa vitambaa zile kubwa ambazo huwezi kuondoa au kusogeza. Ondoa kila kinachowezekana kwenye ukuta kwa maana ya labda umetundika mapambo ya picha na fremu pamoja na taa na vishikizo vyake. Ili upunguze maeneo ya kuweka tepe kama itawezekana pia ondoa swichi za taa na vitasa vya milango ambayo hutaipaka rangi. Hii itafanya upakaji rangi uwe rahisi na kupunguza kazi ya kufunika vifaa hivi. Kumbuka kuzima umeme wakati ukiondoa swichi na taa. Tunza vimisumari na sukuruu vizuri kwenye mfuko mdogo na hata ikiwezekana ziweke alama. Rangi zinadondoka kwenda chini kwahivyo hakikisha kila kilichopo chini ya eneo unalopaka rangi kimeondolewa au kimefunikwa. Pia matone mengine ya rangi yanaweza kwenda upande upande kutegemea na jinsi mpakaji anavyochakarika na kazi yake hivyo hakikisha walau eneo la mita mbili linalopakwa rangi vitu vyote vimefunikwa au vimeondolewa.
Ukishakuwa sasa umeondoa vitu utaziona kuta vizuri kwa uwazi kwa hivyo hatua inayofuata ni kuziba nyufa, matundu na kukwaruza maeneo rangi ya zamani ilikovimba au inakobanduka. Kufanya marakebisho haya ni muhimu sana kabla ya hatua ya kupaka rangi. Utatakiwa kutandaza makaratasi ya plastiki chini kabla hujaanza marekebisho haya ili kuzuia vumbi na uchafu wa mchanga usichafue hasa kama sakafu ni ya zulia la ukuta kwa ukuta. Kazi hii ya marekebisho sio ya kupuuza inabidi kuwa na fundi anayeelewa kazi yake kwani inatofautiana sana kitaalam kwenye kurekebisha tuseme nyufa, matundu na kona zilizovunjika.
Baada ya hapo hatua inayofuata
ni kuhakikisha sehemu zilizofanyiwa marekebisho zimekauka na fundi atumie
kitambaa kufuta vumbi kwenye yale maeneo yote aliyorekebisha. Hii ni muhimu
kwani rangi haishiki eneo lenye vumbi. Kama kuna eneo limeota ukungu, lisafishwe kwa
maji na hakikisha ukuta unaachwa ukauke ili kuzuia ukungu kujitokeza tena hapo
baadaye. Kuna dawa za utangulizi (Primers) ambazo zinasaidia kuzuia ukungu na
fangasi.
Hatua inayofuata ni kujiridhisha kuwa kuta ni safi hazina chembe ya vumbi wala utando wa
buibui na ni kavu. Unatakiwa uwe unaweza kufuta ukuta na sponji bila chochote
kudondoka toka ukutani. Kama kuna rangi ya
zamani ambayo inatoka itatakiwa kukwaruzw tenaa ili itoke, laa sivyo rangi mpya
utakayopaka juu yake nayo itaanza kubanduka mapema.
Sasa kuta zako ni safi,
kinachofuata ni kufunika kwa kuweka utepe maeneo yote ambayo hutaki yashike
rangi. Kama umeondoa zile swichi za taa kama nilivyoelekeza mwanzoni basi
utakuwa na sehemu chache sana
za kufunika. Hata hivyo bado itakubidi kufunika fremu za madirisha na pembeni
mwa vitu vya mbao ambavyo hutaki vishike rangi ya kuta. Tepe za mpaka rangi
zimetengenezwa maalum kwa kazi hiyo na gundi yake haifanyi uharibifu wakati wa
kuondoa.
Hatu inayofuata ni
kupaka dawa ya utangulizi kwenye yale maeneo ambayo yamefanyiwa marekebisho.
Kumbuka hapa tunaangali kuta ambazo tayari zilishapakwa rangi zamani na sio
kuta mpya. Kama zingekuwa kuta mpya basi hii
dawa ya utangulizi ingepakwa kuta zote kabla ya kupaka rangi. Hi inasaidia
kuleta matokeo mazuri kwani dawa ya utangulizi inasaidia kuweka mshikamano na
rangi kwa hivyo pia kusaidia kupunguza gharama kwani inahitajika mizunguko michache
ya rangi kukiwa na dawa ya utangulizi.
Mara unapomaliza hatua hizi chache
muhimu za utangulizi, sasa uko tayari kupaka rangi! Ingawa kazi ya maandalizi
ya kuta kabla ya kupaka rangi inaweza kuonekana kubwa, matokeo ya mwisho ni
mazuri na nguvu iliyotumika inalipa!
Paka rangi! Weka mizunguko mingi iwezekanavyo
hadi ukuta uonekane maridadi na kuwe na ulinganifu wa eneo lote kwa maana ya
kwamba kusiwe na mawimbi mawimbi. Kwa rangi ya ubora wa juu unapaka mizunguko
michache (miwili au mitatu tu) na kupata matokeo mazuri.
Umeshamaliza kupaka kuta zako rangi na
zimeshakauka, sasa ondoa zile tepe. Kama kuna
rangi kidogo imevujia chini ya hizi tepe chukua kibrashi kidogo na uguse maeneo
hayo kwa uangalifu usije ukachafua kwingine.
Baada
ya mzunguko wa mwisho wa rangi kukauka kabisa, anza kurudishia vile vitu vya
ukutani kama swichi na sanaa zako za fremu
ulizokuwa umeondoa ikifuatiwa na kurejesha fenicha na kila kitu mahali pake. Sasa
umemaliza kupamba kwa kupaka rangi, kilichobaki ni kusherehekea!
Kuamua
kuwa unataka kupaka upya rangi makazi yako inatakiwa uwe na muda wa kutosha.
Fikiria kama una watoto wadogo na wanyama wa ndani kama
vile paka watakuwa wapi kipindi cha maandalizi na kupaka rangi. Kumbuka utakuwa
unaangalia kuta hizi kwa muda mrefu na hakikisha utafurahia mradi huu
uliosimamia.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi ni mjasiriamali upande wa usafi wa mazulia, nguo na magari; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment