KATIBU Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, amesema ripoti
za uchunguzi ya Operesheni Tokomeza na suala la Akaunti ya Tegeta Escrow
hazitatolewa hadharani.
“Hakuna mpango wa kuweka ripoti hadharani kwa sababu kuna
mambo ya
kesi zinazoendelea mahakamani, sasa ukianza kutoa hadharani unaharibu
hizo kesi mahakamani,” alisema Balozi Sefue.
Ametoa kauli hiyo siku chache baada ya kutolewa ripoti ya
uchunguzi dhidi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliachim Maswi
hahusiki katika kutolewa fedha za Escrow pamoja na ile ya Operesheni Tokomeza
iliyowasafisha waliokuwa mawaziri wanne wa serikali ya Rais Jakaya Kikwete.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Balozi Ombeni Sefue,
alisema mawaziri wanne waliopoteza nyadhifa zao kwa sababu ya Operesheni Tokomeza
hawakuwa na hatia ila walilazimika kujiuzulu ikiwa ni kuwajibika katika siasa.
Alipoulizwa kuhusu kitendo cha kusema viongozi
waliojiuzulu hawana makosa bila kutaja muhusika anayetakiwa kuwajibika kwa
yaliyotokea, Balozi Sefue alisema: “Kuwajibika kisiasa ni kwamba wewe ndiyo
kiongozi wa siasa kwenye wizara fulani, watu wa chini yako wakifanya kosa,
unawajibika kisiasa.
“Lakini haina maana kwamba wewe mwenyewe una kosa la
kuchukuliwa hatua nyingine ya nidhamu … kuondoka kwenye wadhifa wako ndiyo namna
pekee naweza kusema,” alisema.
Alipoulizwa hatua ya baadhi ya mawaziri waliojiuzulu
kutoa taarifa kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuhusu uhalifu uliokuwa ukitendeka
kwenye operesheni hiyo, Balozi Sefue alisema: “hilo mimi sijui na sijaliona
popote hata kwenye ripoti halipo”.
Wakati ripoti ya Operesheni Tokomeza iliposomwa bungeni,
baadhi ya wabunge akiwamo Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM) alitaka Waziri
Mkuu ajiuzulu kutokana na mateso waliyokuwa wakifanyiwa wananchi bila kuwa na
hatia.
“Wakati operesheni hii inafanyika, hata siku moja
hukuwahi kufika kwenye maeneo inapofanyika, ulikuwa wapi Waziri Mkuu wangu,
ulikuwa wapi? Watu wanabakwa, wanakufa, ulikuwa wapi Mheshimiwa Waziri Mkuu?
Kwa utaratibu wa nchi yetu tumekupa kila aina ya usafiri, kuanzia ndege,
helikopta, magari, ving’ora kila wakati vinalia, ulikuwa wapi Mheshimiwa Waziri
Mkuu wakati mambo haya yanatokea?” alisema Lugola.
Katika mapendekezo yake, pamoja na mambo mengine, Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, ilisema kuna baadhi
wanasiasa waliingilia mchakato wa Operesheni Tokomeza.
Mwenyekiti wake, James Lembeli, aliliambia Bunge kwamba
walibaini kuwa baadhi ya viongozi wa siasa na Serikali waliingilia utekelezaji
wa operesheni hiyo kwa manufaa yao binafsi.
“Kwa mfano, agizo la kuwataka wahusika wa Operesheni
Tokomeza kutowagusa viongozi wa siasa wa ngazi zote, kauli ambayo ilitafsiriwa
kuathiri utekelezaji wa Operesheni Tokomeza kwa kubagua Watanzania katika
makundi ya viongozi na wananchi wa kawaida.
“Hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Serikali ihakikishe
kuna uwajibikaji wa pamoja inapoamua kutekeleza jambo la kitaifa kama
Operesheni Tokomeza,” alisema.
Baada ya ripoti hiyo kusomwa bungeni, Serikali iliunda
tume ya chini ya Jaji mstaafu, Hamisi Msumi, ikiwa na hadidu za rejea sita.
Adidu ya rejea ya kwanza ilikuwa kuchunguza namna
Operesheni Tokomeza ilivyotekelezwa, kuchunguza iwapo maofisa waliotekeleza
Operesheni Tomokeza walizingatia sheria, kanuni, taratibu na hadidu za rejea
walizopewa.
Nyingine ilikuwa kuchunguza iwapo maofisa waliotekeleza
Operesheni Tokomeza walivunja sheria, kanuni, taratibu na hadidu rejea
walizopewa, kuchunguza iwapo kuna watu waliokiuka sheria yoyote wakati wa
utekelezaji wa Operesheni Tokomeza na iwapo hatua zilizochukuliwa na maofisa wa
Operesheni Tokomeza dhidi ya wakosaji hao na mali zao zilikuwa sahihi.
Tume hiyo pia ilitakiwa kupendekeza hatua zinazostahili
kuchukuliwa dhidi ya maofisa wa Operesheni Tokomeza waliokiuka sheria, kanuni,
taratibu na hadidu za rejea za Operesheni Tokomeza.
Ilikuwa pia na jukumu la kupendekeza mambo yanayopaswa
kuzingatiwa wakati wa kupanga na kutekeleza Operesheni nyingine kama hiyo
kuepuka malalamiko mengine yasitokee.
Akikabidhi ripoti yake ya Rais Kikwete, Jaji Msumi
alisema kuwa katika kutelekeza majukumu yake, tume ilitembelea mikoa 20 na
wilaya 38 na kupokea malalamiko mbalimbali kutoka kwa viongozi wa Serikali
ikiwa ni pamoja na mawaziri wanne waliojiuzulu kutokana na suala hilo.
No comments:
Post a Comment