JAJI Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Sumbawanga, Kasukulo Sambo juzi alinusurika katika mapambano yaliyoibuka eneo
la Soko Kuu mjini hapa mkoani kati ya askari polisi na madereva wa pikipiki za
magurudumu matatu maarufu kama Bajaj, baada ya madereva hao kugoma na kufunga
barabara kwa kulala kifudifudi.
Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) walifika eneo
hilo la tukio wakiwa na silaha nzito wakitumia usafiri wa gari lao lenye namba
PT 1854 tayari kukabiliana na mgomo huo .
Licha ya madereva hao kulala kifudifudi barabarani, pia
waliweka mbao zilizopigiliwa misumari kuzuia gari lolote lisipitie eneo hilo la
tukio na kuchoma matari ya magari.
Miongoni mwa watumiaji wa barabara waliokumbwa na adha
hiyo ni Jaji Sambo ambaye gari lake lilizuiwa na kunusurika kushambuliwa na
madereva hao waliokuwa wamejawa na ghadhabu.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Jaji Sambo
alithibitisha kutokewa na mkasa huo na kwamba maofisa askari wa usalama
barabarani waliingilia kati na hatimaye akaruhusiwa kupita eneo hilo na gari
lake .
“Nilipofika eneo hilo nilikuwa madereva wa bajaji wakiwa
wamegoma wakitaka kuonana na Mkuu wa Mkoa kwa kufunga barabara kuu
…..walinizuia nisipite hadi askari polisi wa usalama barabara alipoingilia kati
pia mlinzi wangu alilazimika kushuka gari akiwa tayari na bastola kwa
kujihami…. “Hatimaye niliweza kupita hapo salama saliminik lakini mkasa huo
umesababisha adha kubwa kwa watumiaji wengine wa barabara,“ alieleza Jaji
Sambo.
Shughuli za kawaida katika soko kuu la mjini Sumbawanga
zilisimama kwa muda wa saa moja baada ya jeshi la polisi mjini hapo kuvutana
juu ya mgomo wa ghafla ulioitishwa na madereva wa pikipiki za magurudumu matatu
maarufu kwa jina la bajaji.
Kaimu Kamanda Polisi mkoa wa Rukwa, Kamishina Msaidizi wa
Polisi, Leons Rwegasira amethibitisha kutokea kwa vurugu hizo na kueleza kuwa
bado jeshi hilo linatumia busara kulishughulikia tatizo hilo kabla ya kuanza
kamata kamata.
Aliongeza kuwa hakuna majeruhi aliyeripotiwa wala
uharibifu wowote uliotokana na vurugu hizo ambapo aliwasihi vijana kuacha
kujichulia sheria mkononi na kuanza kurusha mawe kwenye gari la polisi.
Vurugu hizo zilizodumu kwa zaidi ya saa moja zimetokea
leo saa sita mchana ambapo madereva hao wa bajaj wanaotoa huduma za usafiri katika
Manispaa ya Sumbawanga na vitongoji vyake vilisababisha taharuki kubwa kwa
wakazi wa mjini humo.
Mwenyekiti wa madereva hao, Fred Jackson alisema wameamua
kugoma kutokana na utaratibu wanaoutumia askari wa usalama barabarani mjini
Sumbawanga ambapo kila siku wamekuwa wakipanga kiwango cha makusanyo ya fedha
kutoka kwao na hivyo kulazimisha makosa yasiyokuwapo.
Alisema wameshajipanga kugoma mpaka uongozi wa serikali
utakapoyashughulikia malalamiko yao ikiwa ni pamoja na kuwabaini askari wa
usalama barabarani wanaofanya ukamataji kwa lengo la kujipatia kipato na siyo
kusimamia sheria.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment