MGANGA mmoja wa kienyeji amekamatwa akifanya ushirikina
katika Mahakama ya wilaya ya Bunda mkoani Mara kwa kutumia tunguli ili
kuwezesha kushinda kesi.
Mganga huyo ni moja kati ya waganga sita, ambao
walikamatwa
kwa kosa la kupiga ramli chonganishi na kufunguliwa kesi katika
mahakama hiyo ya wilaya.
Mtuhumiwa huyo pamoja na wenzake hao, walikamatwa Machi
11 mwaka huu saa 6:00 mchana katika kijiji cha Kabasa wilayani hapa, wakipiga
ramli chonganishi ya kuchonganisha wananchi kinyume cha sheria.
Mtuhumiwa huyo aliyeshikwa juzi akifanya ushirikina huo
katika mahakama hiyo ni Riku Wasaga Yahaya (50), mkazi wa kijiji cha Kabasa
wilayani hapa.
Mtuhumiwa huyo pamoja na wenzake hao, walipokamatwa
wakipiga ramli chonganishi, walifunguliwa kesi namba 86 ya mwaka huu katika
mahakama hiyo.
Mwendesha mashitaka wa Polisi, Athumani Salum, alidai
kuwa juzi wakati watuhumiwa hao wakiwa mahakamani hapo, wakisubiri kesi yao
kutajwa, mbele ya hakimu wa mahakama hiyo, Said Hamad Kasonso, mtuhumiwa Yahaya
alionekana akifanya ushirikina kwa kutumia tunguli.
Ilidaiwa baada ya mtuhumiwa huyo kupekuliwa na polisi,
walimkuta akiwa na vibuyu viwili vya tunguli na dawa ya ungaunga na mchanga
mfukoni mwake, alivyokuwa anavitumia kufanyia ushirikina katika mahakama hiyo.
Hakimu Kasonso alisema mtuhumiwa huyo na wenzake watano,
walikamatwa wakijaribu kufanya ushirikina wa kuroga mahakama hiyo, jambo ambalo
ni la ajabu mno, kwani Mahakama ni chombo ambacho kazi yake ni kutoa haki na
kutafsiri sheria kikamilifu na kwa kina zaidi ili haki iweze kutendeka.
Hakimu Kasonso alisema kuwa kitendo hicho cha ushirikina
ndani ya chombo cha haki, kamwe hakiwezi kuvumiliwa na hivyo mahakama hiyo
inawapeleka mahabusu watuhumiwa wote sita kwa muda wa siku 14 hadi Mei 22,
mwaka huu, kesi yao itakapotajwa tena mahakamani hapo.
"Mahakama ni chombo cha kisheria ambacho kinatoa
haki baada ya kuitafsiri sheria kwa kina zaidi na kisha kutoa maamuzi, sasa
kitendo cha kuja kufanya ushirikina katika chombo ambacho kazi yake ni kutenda
na kutoa haki, kamwe hakiwezi kuvumiliwa, hivyo watuhumiwa wote waende mahabusu
siku 14," alisema.
Mwendesha mashitaka wa mahakama hiyo, Athuman Salum,
aliwataja watuhumiwa wengine katika ile kesi yao ya awali ya kupiga ramli
chonganishi kuwa ni Komoga Wasaga Msiba, Thomas Nyakojaribu, Oro Odewa
Kalidoshi, Mariamu Thomas na Daud Thomas, wote ni wakazi wa kijiji cha Kabasa
wilayani Bunda.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment