Friday, November 30, 2012

shape ya hizi nail polish mmmmhh!

kweli biashara yahitaji mbinu nyingi. najiuliza hizi nail polish zinahusiana vip na makalio..

Tuesday, November 27, 2012

My article for newspaper: Mlango wa mbele

Mlango wa mbele ni kivutio cha nyumba

Mlango wa mbele wa nyumba yako ni kielelezo chako. Mlango huu zaidi ya kuleta mvuto wa nyumba pia unakuhuisha mara uingiapo nyumbani.

Mlango wa mbele ni moja ya vitu vya mwanzo watu wanavyoona kuhusu nyumba. Rangi, staili na hali yake ni sehemu kubwa ya jinsi nyumba inavyoonekana kwa nje. Mlango huu una kazi ngumu ya kufanya nje kuwe nje na ndani kuwe ndani. Unapata adha ya unyevu, jua, upepo na hata vumbi na kama umetengenezwa kwa mbao kuna uwezekano wa kusinyaa na kuvimba kuendana na hali ya hewa ya majira ya mwaka. Hali hii inafanya mlango kuwa mgumu kufunguka nyakati nyingine au kupiga kelele. Njia nzuri ya kuzuia ni kuhakikisha mlango umepakwa dawa sahihi za kuzuia hali hii kabla ya kuujengea kwenye nyumba.

Mlango wa mbele wa nyumba unaweza kuwa wa mbao, chuma ama glasi. Vyovyote uwavyo uangalizi wa mara kwa mara unahitajika ili kuufanya uonekane maridadi kila wakati. Kama mlango unapigwa na jua la moja kwa moja hakikisha unaupaka  rangi au finishi inayonyonya miale ya jua ili kufanya rangi yake idumu muda mrefu.

Kaya nyingi zimefanya mlango wa mbele kuwa rasmi kwa maana ya kwamba unatumika zaidi na wageni. Kutokana na kuwa hautumiwi mara kwa mara ni muhimu kuhakikisha kuwa unafanya kazi jinsi inavyotakiwa. Swali ni kuwa ni kwanini watu wengi hawatumii mlango wa mbele mara kwa mara? Ni kama vile mlango huu umewekwa kwa ajili ya wengine na wanafamilia hawastahili kuutumia wao wenyewe ambapo wengine hao huja na kuutumia mara chache kwa mwaka. Wakati mwingine hata marafiki na majirani wakija nyumbani, wanatumia mlango wa nyuma au wa pembeni ila sio wa mbele. Matokeo yake mlango wa mbele unakaa tu bila kutumika.

Watu wengi wanaingia ndani mwao kwa kupitia mlango wa nyuma ambao labda umeunganika na varanda iliyojazwa vitu vingi ama hata pengine umeunganika na gereji. Ule usemi wa unachokiona mwanzo kinadumu zaidi ni muhimu sana hapa. Kama unaingia ndani ya nyumba kupitia mlango wa nyuma uliojaa makorokoro na vifaa vya miradi ambayo haijakamilika au hata vifaa vya bustani moja kwa moja utajisikia kuchoka hata kabla hujafika ndani. Nyumbani kwako panatakiwa kuwa himaya yako. Jipe raha kwa kupitia mlango wa mbele, hata kama inamaanisha kuegesha gari yako kwanza halafu unazunguka mbele. Utashangaa ni vip utakavyohuisha nafsi yako!

Mlango wa mbele unasema mengi kuhusu watu wanaoishi kwenye nyumba husika. Kuna watu eneo la ndani la mlango huu linatumika kama stoo. Mlango wa mbele uliozibwa kwa ndani ni alama kuwa wenye nyumba hawataki mtu apitie mlango huo.
Kwa kawaida kitu kinachokuvutia kinakuhamasisha na hivyo kukuongezea nguvu mwilini. Kama mlango wa mbele unakuhamasisha ina maana nguvu inazalishwa. Kama huo mlango huupitii hata mara moja kwa mwezi basi hamna nguvu.

Mazingira ya mlango wa mbele kwa nje ni muhimu sana. Je ni rahisi kuuona mlango uko wapi na kuna njia nyepesi ya kuufikia? Je maua na mimea ya eneo lile imepunguzwa kuufanya mlango uonekane? Jicho linavutwa kuutazama na ni nini hasa kinachokuvutia ukitazama maeneo ya nje ya mlango wa mbele wa nyumba yako? Mlango wako huo unavutia vile ambavyo unasema unapenda katika maisha? Njia ya kueleweka kupitia mlango wa mbele, rangi za kuvutia au mapambo, ni hatua za kwanza kukuwezesha kutumia mlango huo na hivyo kujiongezea nguvu ya kusonga mbele na maisha. Weka eneo la mlango safi na huru, kwa ndani pasiwe stoo na mwisho utumie mlango huu. Kama bado unashawishika kuwa ni usumbufu kutumia mlango wa mbele kwa kila siku basi amua kuutumia japo mara moja kwa wiki. Ukiwa unajua kuwa unajiongezea nguvu kwa kutumia mlango huo.

Kwavile  imeonekana kuwa kaya nyingi hazitumii mlango wa mbele kila siku, basi ni vyema kuhakikisha na kucheki mara kwa mara kuwa mlango unafanya kazi vyema na hata eneo lake ni safi kwa ajili ya ukaribisho rasmi wa wageni. Usianze kuondoa buibui, vumbi na mavi ya mijusi kwenye mlango wako huo mbele ya mgeni wakati wa kumfungulia. Fanya hatua ya mwanzo ya mgeni anayekutembelea kuwa ya kumbukumbu. Pia hakikisha kuwa kile kizulia cha mlangoni ni kisafi.

Macho yanafurahia kuona vitu vizuri, mlango wako wa mbele ni moja ya pambo la kwanza kabisa wageni wanaloona wanapofika nyumbani. Mlango wako uvutie na uoane na mapambo yako mengine ya nje ya nyumba. Mlango huu pia unakulinda unapokuwa ndani, kwa hiyo unatakiwa kuwa imara.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Kwa maoni niandikie barua pepe viviobed@yahoo.co.uk au kwa simu 0755 200023

Wednesday, November 21, 2012

What I do best..



My client Monica wearing dress designed by Vivi. We can work together to get the outfit you need..Karibuuu

My article for newspaper: Master bedroom



Chumba cha kulala cha wakuu wa familia ni kama mahali patakatifu

Chumba hiki ni kile cha  baba na mama wa familia – ni koloni lao hapo nyumbani kama wengine wanavyoweza kusema. Wazazi mkiwa ndio nguzo ya familia basi mnahitaji chumba cha kipekee. Mnaokaa kwenye chumba hiki ndio mnaolipa bili na kufanya kazi kwa bidii ili mfanikiwe kwenye hilo. Kwa nini chumba chenu kisiwe maalumu? Wakuu wa familia mnastahili chumba hiki!

Je wewe mkuu wa familia unakipenda chumba chako cha kulala? Chumba hiki kiwe kama mahali patakatifu kwa wanandoa au yeyote anayelala mle. Ni nini cha kwanza unachokiona mara baada ya kufungua mlango wa chumba hiki, na ni nini unachokiona cha kwanza mara baada ya kufungua macho asubuhi. Chumba hiki kiwe ni sehemu huru pasipo na usumbufu kama wa kufua, kompyuta au midoli ya watoto. Midoli imekuwa ni tatizo kwenye chumba cha kulala hasa kwa wazazi wanaokimbia mchakamchaka wa maisha ya kila siku. Midoli inaishia chumba cha wazazi na hata kitandani.  Kuwa wazi  na kuweka mipaka juu ya chumba hiki na hata midoli ya watoto isijazane chumbani kwako na kitandani. Kwa ujumla watoto wawe na sehemu ya kucheza na kuweka midoli yao. Chumba cha kulala cha wakuu wa familia ni cha watu wazima ndani ya familia.

Fenicha kuu kwenye chumba hiki ni kitanda. Kimsingi, kitanda kina lengo moja kuu: ni kufagilia usingizi wenye afya. Chumba cha kulala cha wakuu wa familia kinahitaji kitanda chenye kukidhi vigezo vya usingizi bora. Kama matangazo tuseme ya magodoro yanavyoonyesha ni kuwa tunatumia theluthi moja ya maisha yetu kulala. Sasa kwa nini godoro, malazi na fremu ya kitanda visiwe maalumu. Kuna njia nyingi ya kupata kitanda bora kwa bajeti yeyote. Kitanda chenye fremu ya chuma tuu kilichosogezwa karibia na ukuta hakikidhi vigezo. Kila kitanda kinahitaji bodi la kichwani (makala zijazo tutaongelea umuhimu wa bodi hili) ambayo yanapatikana kwa saizi na mitindo mbalimbali.

Kwakuwa msisitizo wa chumba hiki ni kwa wanandoa kama kuna sehemu kubwa weka sofa au viti viwili vya kukalia badala ya kimoja. Mara zote fikiria vitu kwenye seti. Kama wewe ni mwanaume au mwanamke uliye singo lakini ndio mkuu wa familia weka picha ya peke yako kusisitiza utambulisho wako kuwa huna mtu. Kama mnaolala humo mko kwenye mahusiano basi mambo ni kwa seti kama vile taa za vivuli mbili, vimeza vya kando viwili na hata kama mishumaa basi miwili.  Kumbuka unatengeneza mandhari ya kupumzika na kuondoa msongo wa mawazo wa siku nzima. 

Chagua sanaa inayoelezea uhusiano wenu iwe ni picha ya ngalawa, ndege au hata maneno ya kimahaba. Sio sawa kuweka picha za marafiki, mababu na hata wanafamilia wengine kwenye chumba hiki. Tatizo ni kuwa chumba kinaanza kuonekana kinguvu kimezidiwa na vitu. Watu wote hawa wana haja gani chumbani kwako. Pambeni chumba cha kulala kwa picha zenu nyie wanandoa mnaolala humo.

Epuka rangi za kukolea sana kwa mfano kama ukiweka pazia za damu ya mzee au bluu ya weusi inaweza kuwa tabu kuamka asubuhi kuwahi kutafuta rizki. Kanuni inasema kuwa mlango usiwe mstari mmoja na kitanda, kwa maana ya kuwa ukiwa umelala kitandani uuone mkango lakini ukifungua mlango macho yasione kitanda moja kwa moja. Mlango ukiwa namna hii unawapa walalaji kujiamini zaidi kuwa wanamiliki chumba na usingizi unakuwa mwororo.

Vifaa vya umeme leo hii ni changamoto kwenye chumba cha kulala. Kompyuta, luninga na vifaa vingine vya umeme vinatuzunguka na kutunyonya nguvu kwa  kuleta nguvu ya uvutano mithili ya sumaku ambayo baadaye inaleta msongo wa mawazo. Ili kupumzisha mwili na kuuweka katika afya njema basi ni vyema kuwa mbali na vifaa vya umeme chumba cha kulala. Kama hamna jinsi kuwa ni lazima vifaa hivi viwepo chumbani basi sio tu vizime na kuacha vijitaa vinawaka bali chomoa kabisa kwenye umeme wakati wa kulala.

Kumbuka kuwa kila kitu kwenye nyumba tunazoishi kinatupa ujumbe. Chumba chako cha kulala wewe mkuu wa familia kinakupa ujumbe gani? Je kinakukumbusha majukumu yote unayohitajika kukamilisha au kinakupa hisia za utulivu na kukukaribisha kupumzika? Je kinakushawishi kuwasha luninga au kinakuleta kwenye faragha? Je kinaongeza msongo wa mawazo kwenye maisha yako? Au kinakupa pumziko la nafsi hata kama uko singo? Kama ndio basi umetengeneza chumba cha kulala ambacho ni kama mahali patakatifu.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Kwa maoni tuwasiliane kwa barua pepe viviobed@yahoo.co.uk au kwa simu 0755 2000 23

Wednesday, November 14, 2012

My article for newspaper: Mapambo ya msimu wa sikukuu




Njia chapchap za kupamba ndani na nje ya nyumba yako msimu huu wa sikukuu

Chochea furaha na msisimko wa kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka kwa kupamba ndani na nje ya nyumba yako. Vitu rahisi hata  kama ni vijipambo vya meza tu huleta tofauti kubwa ya muonekano wa mazingira ya nyumbani.

Baadhi ya njia tofauti unazoweza kuhuisha muonekano wa kizamani wa nyumba yako ni kama ifuatavyo:
Ongeza picha: Kuongeza picha nyumbani kwako kunaongeza muonekano mpya mara moja kutoka ule wa zamani. Ni njia rahisi kabisa kuhuisha sebule yako. Au unaweza kuongeza picha za familia yako ama nunua picha za fremu kuleta muonekano wa kipekee.
Mimea na maua: Pamba mazingira ya ndani na nje ya nyumba kwa maua na mimea. Vesi ya maua au mmea uliooteshwa kwenye chungu kwenye kona ya mahali ndani mwako vinaleta mvuto.
Badili pazia: Hizo pazia za kila siku zinafanya nyumba isionekane tofauti au na mvuto kwa ajili ndio hizo hizo kila siku. Hakuna kitu kinacholeta tofauti kubwa kwenye muonekano wa nyumba kama pazia. Weka mapazia ya aina, mitindo na vitambaa na mishono mbalimbali.
Rangi:  Kupaka rangi ni njia iliyozoeleka zaidi wakati wa kusheherekea. Zimua kuta za mazingira ya nyumbani kwako japo kwa kuongeza koti moja tu ya rangi. Kama labda kupaka rangi chumba kizima ni gharama na kazi kubwa basi paka hata mlango tu.
Weka mito mipya: Badilisha mito ya sebuleni kwako na uweke ya rangi mbalimbali. Mito yenye rangi kali zilizokolea kwenye sofa zako au hata ile mikubwa ya kukalia sakafuni inabadilisha muonekano wa ndani ya nyumba bila ya kutumia gharama au kazi kubwa.
Panga vitu upya: Sio cha zaidi bali tu ni kuhamisha tuseme fenicha moja toka eneo moja hadi lingine. Kufanya hivyo utashangaa jinsi itakavyohuisha muonekano wa mahali.
Pamba eneo la lango kuu:  Kinachoonekana kwanza kinamkaa mtu moyoni daima kwa hiyo unaweza ukahuisha muonekano wa kuingialia nyumbani kwa kupamba eneo la kuingilia. Kwa mfano vyungu vya maua vya chini au vya kuning’inia lango kuu vitaleta mvuto wa kipekee.
Boresha fenicha: Paka rangi fenicha ya zamani au hata ibadili kuongeza matumizi yake. Hii haitaleta tu muonekano mpya bali pia itaongeza thamani na matumizi ya fenicha hiyo.
Weka virembo vidogodogo:  Katika nyumba nyingi utakuta kuna sehemu ambazo unaweza kuweka virembo vidogodogo kama vile juu ya kabati au shelfu na kadhalika. Kutumia nafasi hizi kuweka marembo kutaleta mvuto ndani ya nyumba na kuongeza uzuri wa kutazama na kushangaa.
Mapambo ya msimu:  Vitu vya wakati husika vyenye mvuto vinaweza kuwekwa kama mapambo nyumbani bila hata kutoa jasho. Kwa mfano unaweza weka matunda au maua ya msimu kwenye bakuli la kuvutia, au vesi na kuweka mezani na ikavutia sana.                                                                                      
Pia unaweza kuzungushia taa zisizo na gharama za msimu wa sikukuu kwenye miti ya bustanini au eneo la lango kuu au hata eneo la ngazi wakati wa sikukuu na kuleta muonekano wa maajabu.
Kama tujuavyo sikukuu za mwisho wa mwaka zinazokuja ni krismasi na mwaka mpya hivyo usisahau kupamba kwa mti wa krismasi! Mti huu umekuwa ni pambo la kipekee kwenye nyumba nyingi duniani na hata maeneo ya jumuiya na ofisi nyingi kila mwaka kwenye sikukuu ya krismasi.

Kama unataka kuongeza viungo vya mapambo kwenye nyumba yako yenye muonekano wa siku zote wala huhitaji kutumia gharama kubwa. Mabadiliko kidogo lakini yeye mashiko yatafanya nyumba yako kuonekana upya. Kutembea kwenye nyumba inayoonekana tofauti wakati wa sikukuu kiukweli kutahuisha na kuongeza msisimko wa sikukuu. Hutakiwi kuwa mtaalamu wa mapambo ya nyumbani ili kuleta mabadiliko haya. Kinachotakiwa tu ni kuwa mbunifu wa kufikiri. Jinsi ya kushehereke sikukuu ni kupamba nje na ndani ya nyumba kwa vitupio murua. Kutegemeana na ladha yako unaweza kupamba kwa rangi zilizozoeleka kwa sikukuu za mwisho wa mwaka ambazo ni Top of ForBnyekundu, nyeupe na kijani. Mawazo ya upambaji ni lukuki, kutegemea na bajeti, ladha binafsi na mazingira ya makazi yako.
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Kwa maoni tuwasiliane viviobed@yahoo.co.uk au simu 0755 2000 23.

Tuesday, November 13, 2012

Fashion designing is my passion!

Top
  
Gauni nililombunia mteja wangu Monica. Nashona nguo kwa kuwa ni kitu nakipenda na nachukua muda mwingi kuhakikisha nguo inatoka bomba.

Tuesday, November 6, 2012

My article for newspaper: Mapambo ya bafuni



Mapambo ya Bafuni
Ongeza mvuto bafuni kwako kwa gharama kidogo tu. Kuanza kujenda bafu tokea mwanzo ni gharama ila kuongeza mvuto kwenye lililoko tayari sio kazi kubwa. Kwa baadhi ya watu bafuni ni sehemu ambayo inaachwa kando (au ya mwisho kabisa kufikiriwa)kwenye maswala haya ya mapambo ya ndani. Fahamu kuwa bafuni panaweza kubeba ujumbe mzito hasa kwa wageni wanaokutembelea nyumbani.

Unapopanga kupamba bafu lako (au chumba kingine chochote) pa kuanzia ni kwenye ukuta. Ukuta unachukua sehemu kubwa ya chumba kwa hivyo fikiria ungetaka ukuta wa bafu lako uweje. Je unapenda kuweka taili ukuta wote hadi juu au nusu tu halafu umalizie na rangi. Taili hadi juu ni gharama ila inasaidia kunyonya mvuke hasa kama bafu linatumika na maji yote ya moto na baridi. Pia kama huwezi kuweka taili kuta zote unaweza kuweka hadi juu kwenye kuta za eneo la kuogea na kuta zingine ukaweka nusu ili kujipambia kwa kupiga rangi mbalimbali kwenye kuta zilizobaki bila taili. Taili za kufika hadi mwisho wa ukuta zimeonekana kuleta muonekano wa usafi zaidi na hata kama kuna mapambo au vitundikio vingine unapenda kuweka ukutani basi kuna mashine za kutoboa ukuta wenye taili na hivyo kuweza kutundika mapambo yako kirahisi.

Eneo la kuogea
Taulo na vizulia vidogo vyenye plastiki kwa chini za kuzuia maji ni vitupio muhimu bafuni; utakapoweka vya rangi mbalimbali na kuvibadili mara kwa mara basi vitabadili muonekano wa bafu zima. Weka pazia la eneo la kuogea lenye mvuto linalooana na rangi za taili.
                                                                                                                                                    Eneo Eneo la sinki
Kwa kuboresha muonekano wa eneo hili njia kuu ni kubadili staili ya bomba la sinki. Mabomba ya sinki yanakuja na mitindo mipya kila leo kwa hivyo kwa kuweka bomba jipya itabadili muonekano mzima wa eneo hili. Kama kioo juu ya sinki ni kidogo badili uweke kikubwa ambacho pia kitasaidia kuongeza mwanga bafuni. Badilisha taa ya juu ya kioo iendane na rangi nyingine za hapo bafuni kama vile rangi za mataulo au hata za pazia la eneo la kuogea.

Labda hili ni bafu lako la kuanza maisha baada ya kuachana na wazazi iwe ni kwa kuanza maisha ya ndoa au maisha ya peke yako ya kujitegemea basi kuna vitu kadhaa ambavyo ni muhimu kuwa navyo bafuni. Nimeorodhesha vitu ambavyo nadhani ni muhimu kuwapo bafuni kwako nyumbani, na kwa kweli nimechagua vile ambavyo vinavutia! Unaweza kuishi bila baadhi ya hivi vitu lakini kwa nini ufanye hivyo?
Kumbuka unastahili sehemu nzuri ya kujiandaa kabla ya kwenda kuchakarika siku nzima. Kwa nini usiwe na kila unachohitaji mahali hapo?

Bafuni pawe na mwanga wa kutosha. Linapokuja swala la taa za ndani, bafuni mara nyingi hapapewi kipaumbele na ni pa mwisho kufikiriwa kati ya vyumba vingine vyote. Wenye nyumba wengi wanaweka zaidi hela yao kwenye taa za sebuleni na jikoni. Bafuni kunahitajika taa hasa eneo la kioo, wengi wanaweka ile taa moja tu ya juu ya kichwa. Bafuni ni sehemu ya kuhuisha mwili kwa kuumwagia maji na ni sehemu ya kuanzia na kumalizia siku yako hivyo tusipasahau wakati wa kuamua swala la mwanga wa nyumba.
Bafuni kuwe na vioo vya kukidhi hitaji lako. Weka kioo popote bafuni unapodhani ya kuwa unahitaji kuweka kioo. Usinganganie tu utamaduni wa kioo cha bafuni kinakuwa juu ya sinki. Pia kuwe na seti ya mataulo yale hasaa ya kukausha maji na sio hayo ya barabarani yenye nailoni yasiyokausha vizuri.                                                                                                      
 

Vizulia, pazia la eneo la kuogea na kindoo cha uchafu maalum kwa mazingira ya bafuni ni muhimu viwepo bafuni.                                        
Bafuni kuwe na vifaa sahihi vya usafi na eneo la kuhifadhia . Pia mlango na kioo cha dirisha viwe vimetengenezwa kwa jinsi ya kuwepo faragha.

Kiwekeo cha miswaki ni kitu kidogo na  hutakiona cha maana kuwepo bafuni hadi pale mswaki wako utakapoanguka chini au chooni. Usisahau kuweka sabuni na taulo la mikono kwa ajili ya wageni.
 
Je kuna chochote hapa ambacho kimesahaulika kuwepo bafuni? Kuna katika orodha hii ambacho unadhani hukihitaji bafuni kwako? Kwa maoni niandikie viviobed@yahoo.co.k au simu namba 0755 200023