Wakati
wa sikukuu ni wa kula na kunywa; weka chumba cha chakula tayari.
Chumba cha kulia chakula ni mahali ambapo familia
hukutana na kula chakula huku wakishirikishana kila mmoja juu ya mwenendo wa
siku yake ulivyokuwa. Sikukuu kadhaa zikiwa njiani zaja wengi wetu tunajua kuwa
ni wakati wa kufurahi na jamaa zetu kwa kula na kunywa.
Kimsingi, wakati wa sikukuu unapaswa kuwa ni wa
kusheherekea na kujumuika kwa wakati maalum na wapendwa wetu. Lakini kutokana
na orodha ndefu ya mambo ya kufanya, zawadi za kununua, wageni wa kukarimiwa, mipango
ya safari, wakati wa sikukuu kweli unaweza kuzalisha msongo wa mawazo. Kwa hiyo
iwe unaalika familia kadhaa pamoja au
unapamba chumba chako cha kulia chakula kwa ajili ya watu wawili, makala hii
itakupa dondoo chache za jinsi ya kufanya sikukuu yako iwe njema.
Kwanza panga mapema, usisubiri hadi dakika ya
mwisho. Lakini ni nani asiyekaa hadi dakika ya mwisho na kuanza kuweka mipango
siku hizi? Hata hivyo ni wazo zuri kuanza kuangalia kwenye stoo yako ni nini
unacho na ni nini bado kinafanya kazi toka mwaka jana. Halafu tayarisha orodha
ya nini unahitaji ili utakapoenda madukani kununua unajua moja kwa moja
mahitaji yako.
Tafuta nafasi kwenye chumba chako cha kulia chakula
kwa ajili ya mapambo. Kwa mfano ongeza ladha ya sikukuu kwa kufunga utepe wa
rangi za sikukuu nyuma ya viti vya meza ya chakula. Usijaze mapambo ya sikukuu kwenye
kila kitu kilicho chumba cha kulia chakula, na wala usitoe vifaa vyako vingine
unavyotumia kila siku kwa ajili ya mapambo ya sikukuu. Ila badilisha muonekano
wa kila siku kwenda kwenye wa kisikukuu sikukuu kwa mfano ondoa picha za kila
siku na badala yake pamba kwa picha za msimu wa sikukuu. Kumbuka kutengeneza
sehemu ya kati ya mapambo yako. Usisambaze mapambo kila eneo la chumba.
Sehemu ya kati ya mapambo ni ile inayoonekana zaidi
kwa mfano kwenye chumba cha chakula sehemu hiyo itakuwa ni meza ya chakula. Meza
ya chakula ndio fenicha kuu kwenye chumba cha kulia chakula. Inachukua nafasi
kubwa zaidi na ndio inayotoa picha kamili ya muonekano wa chumba chote. Pamba
meza hii wakati wa mlo wa sikukuu kwa vitu vya msingi kama kitambaa cha meza,
napkini na bakuli la matunda. Tupia
kitambaa cha kupitia eneo la kati tu kisichofunika meza yote ili kuweza kuacha
uzuri wa meza uonekane. Meza iliyopambwa vizuri ni msingi wa mlo wenye
kumbukumbu.
Kosa moja kubwa ambalo watu wengi wanafanya ni
kuremba mno pambo la kati la kwenye meza. Pambo hili kwa makosa linafanywa kuwa
kubwa sana kiasi kuwa wageni wa upande mmoja wa meza hawaonani na wale wa
upande wa pili hivyo linawagawa pande mbili na hivyo kupelekea kugawa
mazungumzo ya wageni wako. Weka pambo la kati lililo dogo. Kitambaa cha meza
kisaidie kuelekeza macho kwenye pambo la kati na sio kishindane na pambo hilo kwa hivyo weka kitambaa kisicho na
mbwembwe nyingi. Angalia usipoteze nguvu
nyingi kwenye kupamba na ukashindwa kufurahia sikukuu.
Meza za chakula kwa matumizi ya nyumbani ziko kwa
ukubwa na maumbo tofauti tofauti kuendana na idadi ya watu kwa mfano zipo za
watu wanne na hadi hata watu kumi na mbili. Meza hizi hasa zile za mbao ngumu
zinauzwa gharama kubwa kwa hivyo kabla hujanya manunuzi hakikisha unanunua
itakayokidhi mahitaji yako.
Kwa ujumla chumba cha kula chakula kilichokamilika
kwa uchache kinatakiwa kiwe na fenicha ambazo ni meza, viti na kabati la
pembeni. Kuendana na ukubwa wa chumba fenicha hizi zinaweza kuzidi lakini zisipungue.
Kazi ya kabati la pembeni ni kuhifadhia vyombo vya ziada, vitambaa vya meza na
pia juu yake panatumika kama sehemu ya kuwekea mabakuli ya vyakula na/au kuwekea mapambo na mishumaa. Kioo cha ukutani juu ya
kabati hili kitasaidia kuakisi mwanga na kuonyesha kama eneo ni kubwa kuliko
kiukweli lilivyo.
Taa maalumu ya kuning’inia juu ya meza ya chakula ni
lazima. Taa hii iwe na ukubwa sahihi kuendana na ukubwa wa chumba na pia muonekano
wake uoane na mapambo mengine yaliyopo eneo hilo.
Wakati wengi wetu tukifikiria chumba cha kulia
chakula tunafikiria meza, viti, kabati na taa kuna kitu ambacho kina umuhimu
sawa na hivi nacho ni pazia. Zaidi ya fenicha zote ngumu zinazojaza chumba hiki
ni muhimu kuwa na vitambaa ambavyo vinaleta hali ya ulaini. Kwa hiyo kama huna
utamaduni wa kuweka pazia kwenye chumba chako cha kulia chakula, inalipa kuanza
kufikiria kufanya hivyo.
Ni rahisi kuchoshwa na hekaheka na shamrashamra za
sikukuu, lakini usisahau sehemu muhimu sana ya sikukuu ni kuona wapendwa wako,
kuwa na wakati mzuri pamoja na kuhesabu baraka zenu !!
Makala
hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Kwa maoni niandikie barua pepe viviobed@yahoo.co.uk au kwa simu 0755 2000 23