Friday, January 23, 2015

MAHUSIANO: Majivu kwa ajili ya kuzuia mimba?! Wanayalamba??


Baadhi ya wanawake wanaamini kwamba wakitumia njia za kisasa wanaweza kuharibu maumbile yao ya mwili ya asilia pamoja na kupata ulemavu.
Wapo wanaoamini kuwa uzazi wa mpango upo kwa ajili ya kupunguza idadi ya watu kwa kuua mayai ya uzazi pindi watakapotumia dawa za kisasa kama kuchomwa sindano, kumeza vidonge, vipandikizi na kuwekewa kitanzi.
Kutokana na kuamini njia za kisasa zina athari kwa afya zao, baadhi ya wanawake hususan waishio vijijini wanatumia majivu kama njia ya kuzuia kupata mimba.
Hali hiyo imekuwa ikichochewa na waume zao kutowaruhusu kutumia njia za kisasa za uzazi wa mpango. Wapo wengine wanakoroga bluu na kunywa pindi wanapohisi wamepata mimba ikiwa ni imani ya kwamba mimba itaharibika.
Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga ina hospitali moja iliyopo Mwadui  maeneo ya mgodini. Wilaya hii pia ina vituo vya afya  vinne, zahanati 45 za Serikali na  nne za  watu binafsi.
 Wanawake katika vijiji vya Ilebelebe, Ikoma na Itilima wanaeleza kuhusiana na mikanganyiko hii ya njia za uzazi wa mpango.
Wanawake wanasema nini?
Mkazi  wa Kijiji cha Ilebelebe, Suzana Mhoja (37) mwenye watoto sita anasema baadhi ya wanaume  wamekuwa chanzo cha wanawake kushindwa  kutumia  uzazi wa  mpango kwa kuhofia kuvunja ndoa zao  kutokana na kutoruhusiwa kwa imani kuwa wataua mayai  ya  uzazi.
Anasema yeye ni miongoni mwa wanawake waliowahi kutumia majivu kama njia ya kuzuia kupata mimba baada ya kupata taarifa kutoka kwa wanawake wenzake.
Anasema licha ya kutumia majivu, alibeba ujauzito kabla ya muda wa miaka miwili aliokuwa amepanga uwe na wa kupumzika ili kutoa nafasi ya kulea aliyetangulia.
“Sitamani tena kuendelea kuzaa lakini wanaume hawataki kabisa kusikia suala hilo la njia za mpango wa kisasa. Ningeweza kutumia kwa siri lakini nahofu ya kuvunja ndoa yangu,” anasema.
Wakazi wa Kijiji cha Ikoma, Sophia Maige (29) na Salume Mshamindi (33) wanabainisha kuwa kama huduma za afya zingekuwa katika kila kijiji, uzazi wa mpango ungefanikiwa vizuri kwani elimu ya uzazi wa mpango ingewafikia wanaume kwa urahisi tofauti na ilivyo sasa.
Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment