Tuesday, November 15, 2016

Namna ya kuchagua marumaru za sebuleni

Naomba ingia instagram @mtotomagazine u like picha hii. Asante sana 

Wakati tunapokuwa tunaendelea kufikiri muonekano wa nyumba zetu iwe ni mpya inayoendelea kujengwa au ni ya zamani unayofanyia marekebisho, chumba ambacho tunazingatia sana ni sebule. Kwanini? Bila shaka ni kwasababu ni chumba ambacho yoyote awe mgeni au mwenyeji ana uhuru wa kukaa anapokuwa ameingia ndani. Kwahivyo, ni
hakika kuwa tunapaswa kuipamba na kuiweka katika muonekano wa kuvutia kwa namna yoyote ile. Wengi wetu wakiwa wanapendezesha sebule tokea hatua ya mwanzo wanazingatia zaidi rangi ya ukuta na upangaji wa fenicha kwa mfano upande utakaowekwa luninga na kadhalika. Lakini je ni vipi kuhusu sakafu? Haudhani kuwa ina umuhimu sawa na kwingine? Hata kama una sebule iliyopendezeshwa vizuri ila ubora hafifu wa marumaru utaangusha muonekano mzima. Kwahivyo, ni muhimu kuchagua marumaru sahihi kwa ajili ya sakafu ya sebuleni, ambapo mbali  na kuvutia, ni kwamba itadumu na kuwa na urahisi wa utunzaji ikiwa ni pamoja na kusafisha.

Inakupasa utazame vitu vingi kama vile bajeti, ubora, ukubwa na rangi, inakubidi ujue dondoo kadhaa kichwani wakati unapochagua marumaru za sebuleni.

Wakati unapoenda dukani au labda mshauri kakuletea picha na sampo au katalogi, kuna uwezekano mkubwa kuwa utapenda mojawapo ya atakazokuonyesha, kama uko kwenye hatua ya kuchagua marumaru za sebuleni basi makala hii ni kwa ajili yako. Twende pamoja.

Kama itakupasa kuongeza hela kidogo kwa ajili ya marumaru ambazo ni bora zaidi, basi fanya hivyo kwasababu ni uwekezaji wa mara moja. Hauendi kubadilisha marumaru za sakafu kila mwaka, sio? Kwahivyo baada ya kutafiti aina mbalimbali na bei zake tumia hela kidogo ya ziada ili kununua zile bora zaidi kwa kuzingatia kwamba ni kitu cha kudumu.

Kununua tu marumaru za gharama na bora haitoshi, inakupasa kuzitunza vilevile. Kama hutafanya hivyo na kuzisafisha mara kwa mara inawezekana vipi ziendelee kuvutia na kuwa imara? Marumaru za poselini ni rahisi kusafisha kuliko za seramiki, inaweza kukupasa kuchagua za poselini.

Kabla hujaamua kununua marumaru za sakafu ya sebuleni inakupasa kuwa na uhakika kuwa zitaendana na mtindo mzima wa chumba hicho. Sakafu inagusa muonekano mzima wa sebule, kwahivyo kabla ya kununua marumaru za sebuleni fikiria rangi ya kuta, fenicha na samani zitakazokuwa hapo.

Kama zilivyo kuta, sakafu pia ina uwezo wa kuifanya sebule ionekane kuwa na mwanga au giza. Kama hautakuwa makini na rangi ya sakafu na ushirikiano na maeneo mengine itaifanya sebule ielezewe kwa jina moja tu, mbaya.
Mara zote jitahidi kupishanisha rangi ya kuta na ya sakafu, kwa mfano kama kuta zina rangi ya mwanga basi sakafu iwe na rangi ya giza na kinyume chake ni sahihi pia. Ila kama kuta na sakafu zote zinatakuwa na rangi za giza, zitakifanya chumba kionekane kidogo na kisicho na uhai. Hata kama utaweka taa nyingi kiasi gani, haitasaidia.
Epuka marumaru za kuteleza kwani zinaweza kusababisha mwanafamilia kuanguka na kuvunja mfupa hasa kitu kikiwa kimemwagika au wakati wa usafi.

Nimeongelea mambo kadhaa ya kuzingatia wakati wa kuchagua marumaru za sebuleni, ila ni vyema ifahamike kwamba mbali na rangi, unatakiwa uchague zilizo sahihi kwa nyumba yako, kwa mfano nyumba kubwa inapendeza ikiwa ma marumaru zenye maumbo makubwa.


Ni nini tena tunatakiwa kuzingatia kwa marumaru za sebuleni ambacho nimesahau? Nijulishe tuelimishane.


No comments:

Post a Comment