Tuesday, March 29, 2016

Kanuni 10 za mpangilio wa sebule

Iwe ni chumba kitupu yaani sebule mpya au ni ya zamani lakini unataka muonekano mwingine, kupanga fenicha sebuleni inaweza kuwa ni changamoto. Unachotakiwa kufanya ni kufuata hatua hizi zenye kanuni za mantiki na ndipo utagundua kwamba kumbe mpangilio huo ni jambo rahisi tu.

Chagua eneo la kivutio cha chumba
Kamwe usidharau nguvu ya eneo macho yanapoelekea mara wewe au mgeni wako aingiapo sebuleni. Kuna wakati eneo hili linajitengeneza lenyewe kwa mfano eneo lenye dirisha kubwa au usanifu mwingine wowote uliofanyika wakati wa ujenzi. Vinginevyo unaweza kulitengeneza kwa mfano eneo ambalo luninga na miziki itakaa. Popote pale penye eneo hili la kivutio ndipo unatakiwa upange fenicha kupazunguka.


Usigusishe fenicha na ukuta
Ukubwa wa chumba ndio unaamua ni eneo kiasi gani libaki ukutani bila kugusana na fenicha, ingawa hata kwenye sebule ndogo kabisa unapaswa kuacha
inchi kadhaa kati ya migongo ya fenicha na ukuta. Lakini kama una chumba kikubwa, panga fenicha katikati huku ukiacha hatua kadhaa kati ya fenicha na ukuta.

Tengeneza eneo la mazungumzo
Watu waliokaa sebuleni wanatakiwa waweze kuongea kawaida kwa uhuru bila kupayuka ama kuumiza shingo kumtazama anayeongea naye. Panga sofa na viti kwa mpangilio ambao zitatazama japo si kazima ziwe kwenye mstari ulionyooka bali ziwe karibukaribu. Kama sebule ni kubwa sana ni afadhali kuweka maeneo mawili. Wapo watu wenye sebule za hivi ambapo wana kawaida ya eneo moja kukaa wageni na la pili hukaa wenyeji.

Tafuta uwiano
Uwiano ni jambo muhimu sana kwenye kupanga fenicha sebuleni. Usipange kubwa tu peke yake na ndogo tu pele  yake. Hakikisha unachanganya ukubwa na maumbo tofauti pamoja.

Zingatia pa kupita
Watu wasiruke fenicha ili kupita. Kuwe na nafasi ya kutosha angalau hatua moja kati ya meza ya kahawa na sofa na pia viti.

Weka zulia lenye ukubwa sahihi
Zulia liwe na ukubwa wa kutosha kiasi kwamba miguu ya mbele ya fenicha iwe huu ya zulia. Hii ni ili kumwezesha aliyeketi hapo miguu yake kuwa juu ya zulia. Maeneo mengine ya nyuma na  kuzunguka fenicha ni sawa yakibaki bila zulia, hakuna umuhimu.

Weka meza ya kahawa kati
Weka meza kubwa ya kahawa katikati ya mzunguko wa fenicha zako. Meza hii ni kiunganishi cha fenicha za sebuleni na pia inatoa nafasi kwa watu kuweka vinywaji vyao na vilevile mwenye nyumba kuweka mapambo yake. Hakikisha unaacha nafasi ya kutosha kati ya meza na sofa au viti ili kumwezesha mtu kupita.

Weka meza za kando mkono unapozifikia
Kila sehemu ya kukaa iwe ni sofa au kiti inatakiwa iwe na ukaribu wa meza ya kando au ya kahawa. Watu hawatakiwi kusimama ili kwenda kuweka au kuchukua kinywaji mezani. Na kwa swala la urefu, meza za kando ziwe na urefu sawa na sehemu ya sofa ya kuwekea mikono ukiwa umekaa. Na kwa upande wa meza ya kahawa, urefu wake unatakiwa kuwa sawa na wa sofa au hata chini yake.

Ruhusu mwanga
Mwanga ni moja ya jambo muhimu pale unapopanga fenicha sebuleni. Kuwa makini usijeweka kabati refu dirishani likasababisha upungufu wa mwanga. Mara zote tumia mchanganyiko wa taa mbalimbali kama vile za darini, ukutani, za vivuli za kusimama toka sakafuni na za mezani ambazo unaweza kuziweka juu ya meza za kando, kwenye shelfu wakati zile za sakafuni unaweza kuzisimamisha pembeni au katikati ya sofa moja na nyingine. Taa zinapaswa kuwekwa katika ngazi mbalimbali ili kuleta uwiano sahihi.

Tumia picha na sanaa za ukubwa sahihi 
Vitu ambavyo umetundika ukutani, iwe ni sanaa, picha, vioo au vinyago vinapaswa kuwekwa kuhusiana na fenicha. Usitundike kipicha kidoogo nyuma ya sofa kubwa. Ukubwa wa sanaa uendana na ukubwa wa fenicha.


Vivi anakuwezesha kupendezesha nyumba yako. Simu 0755200023

No comments:

Post a Comment