Sio siri kuwa kununua sofa ni hela nyingi. Kama utaweza
kuchagua ya rangi sahihi ni kwamba hutajutia. Pamoja na changamoto unayoweza
kukutana nayo wakati wa kuchagua rangi ushauri wangu ni kwamba chagua ambayo
haitakubana katika kupendezesha sebule yako.
Sofa ya kati ya rangi hizi zifuatazo itakupa wigo mpana
wa kupendezesha ndani kwa
kukuwezesha kubadilisha yale mapamba madogomadogo
kila unapohitaji kufanya hivyo.
Nyeupe
Sofa nyeupe haina kikomo cha muda. Pia unaweza kuongezea
pambo la rangi yoyote unayotaka. Huu ni muonekano mmoja ambao kamwe hauchoshi.
Sasa unaweza ukawa unajiuliza je utaiweza kuitunza kwa hiyo rangi yake?
Malighafi ambazo sio moja kwa moja kitambaa ni rahisi kusafishika.
Nyeusi
Sofa nyeusi ni ongezeko muhimu kwenye sebule yoyote.
Inafiti kwenye rangi na mitindo mbalimbali ya upambaji na inafanya iwe rahisi
kuongeza mapambo sebuleni kwako kwasababu karibia kila kitu kinaendana na nyeusi.
Krimu
Krimu ni rangi nyingine pia inayokupa wigo mpana wa
kupamba. Ni rangi ya kiwango inayooana na nyeusi, bluu, nyekundu au kijivu.
Biskuti
Ndio, ni rangi kama ya biskuti hizi hizi tunazokula ila
sio zile nyeusi zenye chokoleti. Rangi ya biskuti iko kwenye kundi la rangi
zisizoegemea kwenye upande wowote na inaoana vyema na bluu, nyeusi na nyekundu.
Udongo
Wengi wenu bila shaka mna sofa za rangi ya udongo
kwasababu ndio imekuwa maarufu kwa miaka kadhaa ya nyuma. Changamoto ya rangi
hii ni kuwa unaweza kujikuta kila kitu ni rangi ya udongo kuanzia kabati, meza
na mapambo madogodogo kama vile mito, fremu za sanaa za picha pamoja na michoro
ya ukutani. Rangi hii kwa sofa ni poa kama utaiepuka kwenye hivi vitu vingine.
Pia kama una watoto ni rangi nzuri kwani inasaidia sana kuficha madoa.
Ila kwa siku za karibuni rangi ya udongo ni kama vile
imewekwa kando baada ya kijivu kuonekana kuja kwa kasi na kuwa maarufu zaidi.
Lakini bado sofa za rangi la udongo ni nzuri na mara zote zina muonekano wenye
kiwango cha juu.
Kijivu
Sofa za kijivu zinaendana vyema na rangi asili ya mbao,
pia nyeusi na nyeupe. Rangi ya kijivu kinashika kasi kubwa kwenye kupendezesha
nyumba kwa sasa.
Rangi za asili
Rangi za asili kama vile kijani na bluu ya maji nazo
zinatulia vizuri kwenye sofa. Kijani kinaendana vizuri na udongo, nyekundu,
chungwa, zambarau na bluu. Sofa ya kijani haikubani kupamba na rangi nyingine.
Ngozi
Rangi ambazo pengine usingezipata kwenye malighafi
nyingine za kutengenezezea sofa, unazipata kwenye ngozi.
Hakika rangi hizo hapo juu zinakuwezesha kupendezesha kwa
urahisi pale unapotaka kubadilisha mapambo mengine madogomadogo. Kwenye fenicha
kubwa kama sofa epuka rangi kali kama nyekundu na zambarau kwani zinaweza
kukupa shida ya kuoanisha na mapambo mengine. Rangi kali za kuwaka zitumie
kwenye vitupio kama mito, vitambaa, na sanaa za ukutani na za kwenye kabati la
mapambo.
No comments:
Post a Comment