Thursday, July 17, 2014

my article for newspaper: kung'arisha nguo nyeupe

Jinsi ya kung’arisha nguo nyeupe

Sababu kadhaa zinaweza kufanya nguo nyeupe zipoteze weupe wake. Huenda utafuata kanuni za utunzaji wa nguo nyeupe, lakini bado zinaweza kubadilika na kuwa na rangi ya njano baada ya muda. Unjano mara nyingi unatokea kwenye nguo ambazo hazijahifadhiwa vizuri kwa kugusana na mbao au bodi za kabati.

Haiepukiki kuwa baada ya muda nguo hupata udongo na kuanza kuonyesha uchakavu. Nguo nyeupe ni chambo cha madoa, na madoa hayo huonekana zaidi ya nguo yenyewe. Habari njema ni kuwa nguo nyeupe hata iwe imendamwa na madoa kwa kiasi gani, bado inaweza kuokolewa.

Soma makala ifuatayo ambapo Aisha Idd ambaye ni mtaalam wa kufua anatujuza namna tunavyoweza kurudisha tena uhai wa nguo nyeupe. Anasema kuna njia kadhaa za kuweza kuzing’arisha tena. Baadhi ya njia zinaweza kuharibu vitambaa laini kwa hivyo kuwa makini.

Unatakiwa kufua nguo nyeupe mara kwa mara. Madoa yanavyokaa kipindi kifupi, ndivyo ilivyo rahisi kuyaondoa. Hii hasa inahusu kwa njano ya kikwapa itokanayo na kutokwa jasho na deodoranti. Weka dawa ya kuondoa madoa kwenye maeneo haya na mengine yenye madoa kabla ya kufua nguo nzima.

Njia ya kwanza na iliyozoeleka na wengi ya kung’arisha nguo nyeupe ni kuweka blichi wakati wa kufua. Blichi ya klorini inashauriwa kutumika zaidi kwa kipimo kilichoelekezwa kwenye chupa na kwenye nguo za pamba. Itumie tu kwa nguo nyeupe na ambazo zinaruhusu blichi. “Hakikisha unasoma lebo ya nguo kabla ya kuamua kutumia njia fulani ya kuing’arisha,” anasema Aisha. Kuna nguo hata kama ni nyeupe ila lebo yake inasema usitumie blichi.
Pia blichi ikizidi inaweza kuharibu nguo na wakati mwingine kuleta mistari ya njano kwenye nguo nyeupe kwa hiyo kuwa makini na kiasi cha blichi kinachotakiwa kuchanganywa na maji. Wakati mwingine yapasa kuloweka nguo zako kwenye maji yenye blichi kwa usiku mzima.

Unaweza kuweka rangi ya bluu kwenye maji ya kusuuzia ili kufanya nguo zako nyeupe zing’ae.  Unachotakiwa ni kufuata maelekezo kwenye chupa ya bluu. Bluu inaongeza ubluu kwenye nguo ambao unaifanya ionekane nyeupe zaidi na ing’ae. Bluu inatakiwa kuwekwa na maji ya baridi.

Kuanika nguo nyeupe zikauke juani ni njia mojawapo pia ya kuzingarisha. Kwenye jua kuna mionzi ya UV ambayo inafanya nguo nyeupe izidi kuwa nyeupe, anasema Bi Aisha. Bila shaka! Mwanga wa jua ni zana mojawapo kuu ya asili tuliyonayo ya kufanya nguo nyeupe zizidi kuwa nyeupe bila kutumia kemikali.

Vinega; ndio vinega hii hii unayoifahamu pamoja na sabuni yako ya kufulia vitang’arisha nguo zako nyeupe. Vinega ni kilainishi na marashi ya nguo, hii inawekwa kwenye maji wakati wa kusuuza. Usijali harufu kwani nguo zako hazitanukia kama vinegar bali harufu itapotea juani wakati wa kukaushwa.Vinega hii nyeupe pia inasaidia kuondoa mabaki ya sabuni kwenye nguo. Onyo: Kamwe usichanganye vinega na blichi kwani inafanya kemikali hatari kwa nguo zako, anasema Aisha.

Juisi ya ndimu ni njia nyingine ya asili ya kung’arisha nguo nyeupe. Weka nusu kikombe cha chai na sabuni kwenye maji ya kufulia (hata kama unafua kwa mashine) na endelea kufua nguo nyeupe kama kawaida. Itumie tu kwenye nguo nyeupe kwani inaweza kuharibu nguo za rangi.

Magadi soda (Baking Soda) nayo inaleta matokeo ya ajabu kwenye kung’arisha nguo nyeupe bila kutumia blichi. Hii pia weka nusu kikombe cha chai pamoja na sabuni yako ya kufulia. Nguo zitatoka nyeupe na zitang’aa kuliko.  Usishange hii ni moja ya viambato kwenye dawa za meno, ni kwa ajili ya kuongeza weupe.

Hizo hapo juu ni njia mbalimbali za kufanya nguo nyeupe ziwe nyeupe zaidi. Zingatia kuchagua sabuni za kufulia ambazo zimetengenezwa kwa ajili ya kung’arisha na zitumie mara kwa mara kwa matokeo mazuri. Fua nguo nyeupe kwa maji ya baridi ili kufanya madoa na unjano usizame na kung’angania zaidi kwenye nyuzi za nguo. Usichanganye njia moja na nyingine pamoja kwani unaweza kutengeneza kemikali itakayoharibu nguo zako.

Kwa hivyo kwa matokeo mazuri, fua nguo zako nyeupe kwa sabuni za kawaida za kufulia ukiongeza moja ya njia za kung’arisha hapo juu tulizojuzwa na Bi Aisha. Halafu tundika nguo zikauke juani. Utashangazwa ni kwa namna gani zimeng’aa. Bottom of Form


Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi na pia ni mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com

No comments:

Post a Comment