Thursday, July 31, 2014

my article for newspaper: kusafisha bafuni


Hakuna anayetaka kusafisha bafuni, lakini ukisafisha kila unapotumia, kazi inakuwa na maumivu kidogo kuliko kuacha hadi wakati wa usafi mkubwa. Makala hii itakujuza ni jinsi ya kuweka kuta, bafu, sinki, bomba, eneo la kuogea na bakuli la choo nadhifu kila wakati.
Unapoanza kusafisha bafuni, kwanza ondoa vitu vyote vya kuhamishika kama vile vizulia, tenga la nguo chafu, kimeza au kikabati na kindoo cha taka.
Hakikisha kuwa dirisha liko wazi ili hewa ipite kuondoa hewa nzito.

Baada ya hapo ondoa buibui kwenye kona za dari ikifuatiwa na kufuta vumbi mlango kwa nje na ndani. Kwa ujumla wakati wa kusafisha chumba anzia juu kushuka chini. Ruhusu taka za vumbi na buibui zimwagike sakafuni kwa ajili utasafisha mwishoni. Kitambaa cha kufutia kinafaa sana kwa kazi hii japo pia waweza kutumia fagio.

Mimina blichi ama sabuni za kusafishia kwenye bakuli la choo na iache iondoe uchafu taratibu.

Weka dawa ya unga wa kusafishia zile sehemu ambazo zina uchafu. Kama kuna uchafu umejijenga kwenye lile eneo la kuogea, sinki ama pembeni na bomba weka unga wa kusafishia halafu sugua taratibu kwa brashi. Ukiacha unga huu ukae kati ya dakika 10 hadi 15 wakati ukifanya jambo jingine itaruhusu kulainisha uchafu. Hakikisha unasoma maelezo ya dawa ya kusafishia ili kuwa na uhakika unatumia kiasi sahihi ambacho hakitaharibu maeneo yako. Pia ni vyema kujaribu dawa eneo dogo kabla ya kusafishia eneo kubwa.

Paka sabuni au dawa nyingine za kusafishia kwenye kuta za bafu kama ni za marumaru. Kwa kutumia sponji ama brashi sugua sehemu uliyoweka sabuni. Isuuze vizuri kuondoa michirizi yoyote michafu na kama ukuta ni wa karibia na sinki ama bakuli la choo ukaushe kwa taulo. Ukuta wa sehemu ya kuogea unaweza kuuacha bila kuukausha. Ni vyema kuvaa glovu wakati wa kusugua kwani baadhi ya madawa na sabuni zinaweza kuchubua ngozi.

Safisha bomba la kuogea ambalo sio siri kuwa wasafishajiwengi huwa hawakumbuki kusafisha. Bomba inatumika tu kusafishia kwingine ila yenyewe inasahaulika kusafishwa. Ni kama msemo wa mshumaa kujiunguza kumulikia wengine! Kwa sababu hiyo utakuta kwenye bomba na vichwa vyake kunakuwa na uchafu wa sabuni zilizogandian. Hali huu huweza ikasababisha makazi ya vijidudu.

Pazia la bafuni huwa linaandamwa na ukungu eneo linalogusana na sakafu. Ni vizuri zaidi ukalifungua na kulifua kwenye maji ya moto kwa kiasi kidogo cha sabuni na blichi. Kumbuka adui nambari moja wa ukungu ni blichi. Kiasi kidogo kitaondoa uchafu bila hata kusugua.

Angalia eneo la sinki na sugua mabaki ya sabuni na dawa za mswaki kwa sabuni kidogo pamoja na sponji au brashi. Mswaki wa zamani unaweza kutumika kuondoa uchafu kutoka eneo la kati  ya bomba na mishikio yake. Kuwa makini kuwa brashi la kusugulia bakuli la choo lisitumike kusugulia  sinki. Hii inaweza kusambaza maradhi kwa kuruhusu vijidudu vya kwenye choo kuingia kwenye sinki la mswaki. Kuzuia hali hii isitokee, brashi la bakuli la choo liwe la peke yake. Ni muhimu kutumia blichi kusafishia bafuni ili kusaidia kuua vijidudu.

Safisha kioo kwa kutumia ama maji na taulo au dawa ya kusafishia vioo na taulo.

Safisha nje ya choo ukianza na ile sehemu ya juu ya kuvuta maji, taratibu endelea kusafisha eneo lote la nje ya choo ambalo ni pamoja na mfuniko na eneo la chini ya pale pa kukalia na futa kwa taulo. Kumbuka kitaulo hiki kimetengwa kwa kusafishia choo pekee.
Sugua ndani ya bakuli la choo kwa brashi yake halafu vuta maji. Huna haja ya kusugua kwa nguvu nyingi. Acha sabuni na dawa ya kusafishia ikufanyia kazi hiyo.

Sasa ni wakati wa kusafisha sakafu ukinanzia na zile sehemu zilizojifisha hadi zile za wazi. Safisha mavumbi yote na uchafu wote ulio chini na pale eneo la choo lilipounganika na sakafu. Eneo hili kwa kawaida huwa ni chafu sana na lile bomba la nyuma linajaa mavumbi. Malizia kwa kusuuza kwa maji masafi kuondoa sabuni itakayoweza kubaki na kusababisha utelezi.

Subiri kidogo sakafu ikauke ndipo urudishe vile vitu ulivyoondoa awali.
Ili kuweka bafu lako katika hali ya usafi na kupunguza kutumia nguvu kubwa ya kusafisha unatakiwa uwe unasafisha maeneo mbalimbali ya bafu mara baada ya kuyatumia. Kwa mfano safisha bakuli la choo kila baada ya kulitumia, vile vile eneo la kuogea pamoja na sinki. Hata kama sehemu hizi hazionekani kuchafuka safisha tu kwani madini yaliyoko kwenye maji nayo yaweza kufanya alama. Kama utafanya hivi, usafi mkubwa utakuwa na maumivu kidogo kwani uchafu hautakuwa umejijenga.


Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi na pia ni mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com

2 comments:

  1. Dawa gani nzuri ya kung'arisha choo?

    ReplyDelete
    Replies
    1. huwa natumia harpic na sijawahi kujutia hela yangu. inafanya vizuri kwa kweli

      Delete