WAZIRI WA NISHATI NA MADINI, GEORGE SIMBACHAWENE |
Serikali imefuta mkataba wake na kampuni ya Selcom
iliyokuwa inauza umeme wa Luku kwa kile kilichodaiwa kuwa ni ubabaishaji katika
kutoa huduma hiyo.
Pia kampuni hiyo, ambayo imekuwa ikinunua umeme wa jumla
kutoka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) imesitishiwa mkataba huo kutokana na
kukiuka sheria na taratibu za ulipaji wa kodi.
Hata hivyo, mkurugenzi mtendaji wa Selcom, Sameer Hirji
hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo.
“Siwezi kuzungumzia chochote kuhusu hilo (mkataba).
Tutakuwa na mkutano na waandishi wa habari kesho (leo),” alisema.
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene aliitaka
Tanesco kufuata uamuzi wa Serikali kwa kuwa Selcom imekuwa ikilalamikiwa na
wateja kuwa na matatizo ya kiufundi kila wanaponunua umeme, hasa ifikikapo
mwisho wa mwezi.
“Hatuwezi kuendelea kuvumilia hali hii kwa sababu hafai.
Hiyo nafasi tumeiondoa, tunawapa wengine. Utendaji wao mbovu na umekuwa
ukisababisha wananchi kukosa umeme.
“Mteja anafika kwa wakala kununua umeme, anaambiwa
hakuna, tunarekebisha mitambo yetu,” alisema.
Selcom na Maxcom ndiyo kampuni pekee zilizoshinda zabuni
za kuuza nishati hiyo na kuingia mkataba na Tanesco wa kununua umeme wa jumla
na kuuza kwa rejareja. Hata hivyo imeelezwa kuwa Maxcom imekuwa ikifanya vizuri
kuliko Selcom.
Simbachawene, ambaye amechukua nafasi iliyoachwa na
Profesa Sospeter Muhongo, alisema pia wameichukulia hatua za kisheria kampuni
hiyo kutokana na kukuika taratibu za kulipa kodi.
“Kwa mujibu wa sheria za kodi hawawezi kuendelea kutoa
huduma na hili wala halina athari zozote kwa sababu wao ndiyo wamevunja
sheria... naomba wananchi wanunue umeme katika vituo vya Maxcom hadi pale
tutakapopata muuzaji mwingine,” alisema
Mkurugenzi wa Tanesco, Felchesmi Mramba alisema kabla ya
kuchukua uamuzi huo walipokea barua kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
wakiwataka wasitishe mkataba wao na Selcom.
“Ukiachilia mbali malalamiko yaliyokuwa yanatolewa na
wananchi. TRA walituambia tusifanye kazi na hao jamaa huku wakiwatuhumu kwa
kugushi nyaraka na kukiuka taratibu za kulipa kodi.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment