Thursday, July 3, 2014

my article for newspaper: kutandika kitanda

Jinsi ya kutandika kitanda ili kionekane nadhifu na maridadi

Linaweza kuonekana ni jambo rahisi ila kufahamu mbinu za kutandika kitanda kionekane nadhifu na maridadi ni faida ya kila mmoja iwe ni mtu wa umri mdogo au wa makamo na awe ni mwanaume au mwanamke. Kuwa na kitanda kilichotandikwa vyema sio tu kinaonekana nadhifu, bali pia unajisikia vizuri wakati ukifunua shuka kwa ajili ya kulala usiku. Kitanda nadhifu kinaleta burudiko la moyo vilevile, kwa ajili kinaleta hisia ya utulivu na muonekano wa kuwa na mapangilio chumbani. Kitanda kilichotandikwa nadhifu pia, ni nadra kuanza kuhangaika kupanga shuka wakati wa kulala na hii inamaanisha amani zaidi na muda mchache wa kupambana na shuka na blanketi.

Awali ya yote ondoa malazi yote ( shuka na blanketi au komfota) pamoja na mito kitandani. Chukua shuka safi ambazo zinafiti ukubwa wa kitanda chako. Kama shuka zako ni zile za seti ya shuka moja ya kufitisha (hii ni ile yenye mipira kwenye kona zake) na ya pili ni flati (haina mipira), basi chukua hii ya mipira na ifitishe kwenye kona nne za godoro. Shuka hizi za kufitisha zinarahisisha sana utandikaji wa kitanda hasa kama saizi ya shuka na godoro ni sawasawa. Huna haja ya kunyoosha kusawazisha mikunjo kwani huwa inajisawazisha yenyewe ukishavalisha kwenye kona za godoro. Kama ni saizi sawa na godoro itafiti vizuri kabisa.

Baada ya hapo juu ya shuka ya kwanza tandaza ya pili ambayo ni ile flati kwa jinsi ambayo upande wenye pindo kubwa unakuwa kichwani na ule wa pindo dogo unakua miguuni. Hakikisha shuka hii inaning’inia ukubwa sawa kwenye pande zote za kitanda ikifuatiwa na kuichomekea kwenye godoro sehemu za miguuni wakati maeneo la kichawani na pembeni yakiachwa bila kuchomekewa.

Tandaza blanketi juu ya shuka ya flati ukilinyoosha vizuri kwa kadri unavyosogea. Ruhusu urefu kiasi wa blanketi kwa ajili ya kuchomekea miguuni. Kunja blanketi eneo la kichwani ukiwa umelishikisha pamoja na lile shuka la flati urefu wa saizi ya upana wa mto mkubwa wa kitandani. Baada ya kukunja chomekea kwa pamoja blanketi na shuka kwenye pande mbili ndefu za kitanda.Kama kitanda kinatumika kila siku utandikaji huu ni njia rahisi kwa mlalaji kufunua upande anaopandia kitandani, shuka ya juu iliyokunjiwa na blanketi na kuingia kitandani kulala. Ila kama kitanda husika hakitumiki mara kwa mara, kwa mfano kama ni kitanda cha chumba cha mgeni unaweza kufunika  kwa kuchomekea kote kote na juu yake kuweka kava la kuzuia vumbi hadi mgeni atakapotembelea.

Sasa basi endapo kitanda tunachotandika ni kwa ajili ya matumizi ya kila siku njia ya kukunja shuka na blanketi ni utandikaji utakaofaa zaidi. Eneo la kichwani mahali ambapo pamekunjiwa blanketi, lile shuka la kufitisha litakuwa linaonekana kwa hivyo chukua mito na weka juu yake.  Huenda unahitaji mito miwili tu kwa ajili ya kulalia, ila unaweza kuongeza mito kadhaa midogo midogo kama mapambo kukipa kitanda mvuto.Unaweza kuweka mito mitano hadi sita kuendana na ukubwa wa kitanda chako. Kanuni ya kuweka mito kitandani ni kuwa lile eneo la kichwani lisibaki na uwazi wa ukubwa wa mto. Kwa maana ya kwamba kama kuna uwazi wa kutosha mto uliobakia basi ongeza mto. Kwa mmoja namna hii ya utandikaji inaweza kuwa mwisho na akajiridhisha kitanda kimekamilika na kina mvuto, ila kwa mwingine anaweza kupenda kuongezea komfota.

Kwa hivyo kama wewe ni mmoja wa wanaopenda kutandika komfota kitandani basi litandaze juu ya blanketi huku ukilinyoosha vizuri kuondoa mikunjo yote inayoweza kutokeza. Huna haja ya kuchomekea komfota na huwa lenyewe ni njia mojawapo ya kupamba kitanda – liache tu likining’inia urefu unaolingana kwenye pande zote za kitanda na hapo kitanda kinakuwa kimemalizika kutandikwa.

Kuna baadhi yetu ambao hatuoni umuhimu wa shuka ya pili. Uzoefu wa kutumia shuka moja (ikiwa ni ile ya kufitisha ni bora zaidi) na komfota pekee inafanya utandikaji wa kila siku wa kitanda uwe rahisi, ila kiukweli ni kuwa hii shuka ya pili inaulinda mwili wa mlalaji usikwaruzwe na ugumu wa blanketi au komfota na pia husaidia kuweka blanketi au komfota safi na bila kusahau kuongezea mwili joto. Ni rahisi zaidi kufua shuka mara kwa mara kuliko blanketi au komfota, na pia makava haya ya kitanda yanadumu zaidi yakifuliwa mara chache.

Kutumia shuka ya flati ambayo ina ukubwa wa kutosha inafanya kitanda kiwe rahisi kulalia na kutandika tena asubuhi ya pili. Tumia shuka na blanketi zenye ukubwa wa kutosha kiasi kwamba havitachomoka chomoka ukiwa umelala. Kama una blanketi dogo ni bora kulikunja na kuliweka chini ya mito na ukawa unalikunjua na kujifunika wakati wa kulala tu kwa maana ya kwamba wakati wa kutandika unalikunja kwani ukiamua kuchomekea blanketi dogo litakusumbua kwa kuchomoka kila mara.

Zaidi ya kutandika safisha chumba chako cha kulala ili kuonyesha zile juhudi zako za kutandika. Kitanda pekee kikiwa maridadi ilhali sehemu ya chumba iliyobaki ni mrundikano unadhifu hauwezi kuonekana. Kutandika kitanda kunakuwezesha kuanza siku yako vizuri na kunakufanya ujiikie kuwa na mpandilio zaidi mapema mwa siku yako.


Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi na pia ni mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com

No comments:

Post a Comment