Wakati ukiwa unasafisha makazi yako
mwishoni mwa wiki hii, kumbuka kufanya usafi wa uhakika. Mara nyingi huwa
tunasafisha maeneo na vitu vinavyoonekana. Makala hii itakujuza baadhi ya
sehemu na vitu ambavyo kwa wengi ni rahisi kusahaulika kusafishwa na mwishoni
utasema, ee kweli hapa huwa sisafishi.
Tunakumbuka kusafisha ndani ya
jokofu, lakini je juu na chini yake? Ndani ni kwasababu huenda kila
tunapofungua mlango wa jokofu harufu mbaya na macho yanatuashiria kuwa sasa ni
wakati wa kusafisha. Juu ya jokofu kunabeba vumbi ambalo sio rahisi kuliona
vinginevyo uwe ni mrefu sana. Nyuma na chini ya jokofu vile vile kunaweza kuwa
kumebeba vumbi sawa na lile la juu. Na chini sio vumbi tu hata mabaki ya vyakula
vinavyodondoka kwenye sakafu ya jikoni. Kinachotakiwa ni kusimama juu ya kiti
na kusafisha juu wakati kwa chini
unachotakiwa ni kuomba mtu wa kukusaidia kulisogeza ili usiharibu sakafu yako
kwa kuburuza. Jokofu likishakuwa limesogezwa, ni kiasi cha kufagia na kudeki. Baada ya hapo lirudishe mahali pake.
Tunategemea
feni majumbani mwetu kwa ajili ya kuleta mpepea wa ubaridi. Kwa kadri feni
inavyotumika, ndivyo inavyojaa vumbi. Feni hasa za darini ni maarufu kwa kujaza
tabaka la vumbi. Njia rahisi ya kuzisafisha ni kufuta kwa kutumia ufagio uwe wa
kawaida au wa buibui uliofungiwa kitaulo kilicholoa kwenye brashi zake.
Kulingana na majira na matumizi, feni zisafishwe walau mara moja hadi mbili kwa
mwezi .
Ni
kichekesho cha muda mrefu kuwa ndani ya nyumba sofa ndio eneo linalomeza vitu
vidogodogo. Kwa sababu hii mito ya sofa (ile ya kukalia na kuegemea) inapaswa kuondolewa
na ndani ya sofa kusafishwe. Japo kwa nyumba nyingi ndani ya sofa ni rahisi
kusahaulika kusafishwa hadi pale vitu kama hereni, kalamu ama opener inapopotea
ndio eneo hili linakumbukwa kua huenda mtoto kaficha humo. Kulingana na aina na
ukubwa wa familia yako pengine huhitajiki kusafisha ndani ya sofa mara kwa
mara. Usafi huu ujumuishe na kufua foronya za mito, ni kazi rahisi japo huwa inasahaulika.
Ndoo
za taka za ndani ya nyumba zinaashiria kuwa zinahitajika kusafishwa ila pipa la
nje linakosa kiashiria hiki kutokana na eneo lililopo. Ukiona jirani anaanza
kuguna kila unapofungua pipa lako la nje la taka basi ni wakati wa kufikiria
kulisafisha kiaina. Kwa kawaida mapipa ya taka ya nje yanahitaji kutupiwa jicho
la usafi zaidi wakati wa kiangazi kuliko wa masika.
Kama una taa za vivuli ndani ya nyumba yako, kumbuka kusafisha kile kifaa kinachosababisha kivuli. Kuendana na jinsi kilivyotengenezwa iwe ni kwa kitambaa, kioo au plastiki zinaweza kusahaulika kufunguliwa na kusafishwa.
Majani ya mimea iliyooteshwa ndani ya nyumba husahaulika kufutwa vumbi. Haishangazi kukuta mmea wa ndani iwe ni nyumbani au mgahawani ukiwa na majani yaliyojaa vumbi.
Vipasha vyakula (microwave) vinachafuka sana ndani kwa kuwa wengi wanapasha vyakula ambavuo havijafunikwa. Uchafu huu wa matone ya michuzi unaorukia kwenye kuta za microwave hubaki na kukaukiana na ajili unapata moto kila vyakula vingine vinapopashwa. Haishangazi kukuta microwave ambayo kwa jinsi ilivyo ndani unapata ukakasi kupashia chakula.
Ingawa wengi hawana taabu ya kukumbuka kusafisha vioo iwe ni vya madirisha au vya kujitazama, kioo cha luninga ni eneo ambalo kwa wengi linasahaulika kusafishwa. Endapo luning hii inatumiwa na watoto wadogo ni rahisi kuona alama za vidole kwenye kioo pale inapokuwa imezimwa. Chukua muda kufuta vumbi luninga yako weekend hii ili kufanya kioo king’ae tena.
Vumbi linajikita kwenye vitabu. Chukua dasta kufuta vumbi vitabu vyako.
Ingawa tunaweza tusione uchafu na utando ulio kwenye vitasa vya milango ya nyumba zetu lakini upo. Na tunapovisafisha tunaweza tusihisi tofauti, lakini unajisikia vizuri kushika kitasa kisafi. Na zaidi ya yote kukinga nyumba yako na vijidudu vinavyotoka kwenye mikono michafu inayofungua milango kwa kushika vitasa hivi.
Ni nini na wapi unapofikiri watu wengi wanasahau kusafisha? Je kuna popote nimesahau?
Makala hii
imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa
makazi na pia ni mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au
maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com
No comments:
Post a Comment