Makosa makubwa ya kuepuka wakati wa kununua sofa
Moja ya umuhimu wa makala kama hii ni kusaidia wadau kuchagua kilicho chema kwa ajili ya nyumba zao. Sofa ni fenicha ambayo muda mwingi wa maisha ya nyumbani unakuwa pale hivyo inatakiwa ikidhi viwango vya nyumba na maisha unayoishi. Kuhakikisha unapata sofa sahihi, epuka makosa haya makubwa unayoweza kufanya wakati wa kuinunua. Habari njema ni kuwa makosa haya yanaweza kuepukwa kama kutafanyika maandalizi kabla ya manunuzi. Makosa haya makubwa basi, ni yapi ambayo mara kwa mara wanunuzi wanayarudia?
Kusahau kupima ukubwa wa sebule yako
Unatakiwa
kujua ukubwa wa chumba kabla ya kukua sofa ili kuwa na uhakika kuwa fenicha
hiyo mpya itafiti. Usikimbilie kununua fenicha kabla ya kuwa na uhakika wa
ukubwa wa chumba, zingatia itakavyokaa kwa kujali milango na madirisha.
Kama
eneo husika kuna mwanga mwingi unaoingia zingatia rangi ya kitambaa kwani vipo
vinavyopaushwa na jua. Sofa inatakiwa iendane na ukubwa wa chumba, isiwe kubwa
sana wala kiduchu. Usitegemee kumbukumbu wakati ukiwa kwenye chumba cha
maonyesho ya sofa, huwa inadanganya kuona kuwa sofa ni ndogo kwenye chumba hicho
kwani eneo ni kubwa, pia sofa iwe na uwiano na fenicha nyingine sebuleni.
Kutokuwa makini
na rangi
Je
unafahamu kuwa rangi ya sofa inayoonekana kutokuwa na nguvu kwenye chumba cha
maonyesho inaweza kuwa kinyume kwenye sebule yako? Nenda na mto wa sofa
unaoupenda na kuutupia kwenye sofa unayotaka kununua ili kuona itakuwaje ndani
mwako.
Mvinyo mwekundu unaenda kumwagika kwenye sofa zako, kama una wanyama wa ndani kama paka nao wanaenda kufanya mambo kwenye sofa yako, mwenza na watoto wanaenda kula bisi kwenye sofa zako; hata uwakataze mara ngapi. Kwa kuwa maisha halisi yanaendelea kila siku, unahitaji sofa ya kuweza kubeba madhila yote haya.
Kuchagua aina mbaya ya kitambaa cha sofa ni kosa la gharama. Chagua rangi na aina ya kitambaa kutokana na jinsi sofa inavyoenda kutumika. Kama sebule inatumika sana na ukanunua sofa ya kitambaa laini au rangi za mwanga, inaenda kuharibiwa hata kabla hujaifurahia. Rangi ya sofa iendane na fenicha, samani, rangi ya ukuta na taa.
Rangi nyeupe, maziwa au nyingine ya mwanga isiwe chaguao lako kama kwenye makazi yako kuna uwezekano wa tope na mikono michafu kufikia sofa. Siku zote chagua rangi ambayo unaipenda na unaweza kuishi nayo, usichague kwa kuangalia mitindo ya nyakati. Utaishi na hiyo rangi uliyochagua kwa miaka.
“Siwezi kukuambia ni mara ngapi nimefanya kazi na wateja ambao wanataka kubadili kitambaa cha sofa zao ambacho bado kiko vizuri bali ni kwa sababu tu wameichoka rangi yake”, anasema mtengeneza sofa Hamis Rajabu. Bahati mabaya ni kuwa haichukui muda kuchoka vitambaa vya maua maua, vyenye mistari mikali na vile vya rangi za giza, anasema Hamis. Ushauri wangu ni kuwa, chagua rangi ya kitambaa ambayo itashirikiana na rangi nyingi. Kama unapenda rangi nilizosema zinachosha mapema basi weka japo kwenye kiti kimoja cha pembeni lakini siyo kwa sofa nzima, anashauri Hamis
Kutokuomba ushauri
kwa wauzaji
Ongea
na watu wanaouza watakupa mawazo ambayo yatakupelekea kufanya maamuzi ya busara.
Hata hivyo unamuizi wa mwisho ni wako ila unapenda kuwauliza wataalam usikie
wanasemaje.
Kutofikiria sofa
ina burudiko kiasi gani
Utakubaliana
na mimi kuwa mara nyingi unaweza kushindwa kupata usingizi kitandani, ila ukija
kwenye sofa ukaegesha aidha ukiangalia muvi au kusoma kitabu haraka sana
unapata usingizi. Ni muhimu kuwa sofa unayotaka kununua ikawa ya matumizi na
burudani.
Kununua sofa
kabla ya kuijaribu
Kama
ambavyo sofa haitakiwi kuwa ndogo sana au kubwa sana kwenye chumba, vilevile
isiwe ndogo sana au kubwa sana kwako. Kama ni mrefu, hakikisha ukikaa miguu
yako itakaa vizuri. Kamwe usinunue sofa kabla ya kuijaribu, ikalie, ilalie,
ijaribu kwa kila namna ambayo utaitumia nyumbani. Kama unapenda kupata usingizi
wa mchana kwenye sofa hakikisha mikono yako iko vizuri kwenye sofa unayotaka
kununua.
Haya ni makosa makubwa ya kuepukwa wakati wa kunua sofa. Endapo utafanya makosa haya utaishia kutoridhika na sofa uliyonunua.
Tukutane wiki ijayo!
Makala hii
imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa
makazi na pia ni mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au
maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com
No comments:
Post a Comment