Huenda pengine ndio unaanza maisha ya kujitegemea au ya
ndoa, unahitaji kuwa na vifaa vya msingi jikoni vya kuanzia kwa miezi michache
ya mwanzo—hata miaka michache. Au labda ni mzazi unayetaka kumsaidia
huyo kijana wako, binti au rafiki namna ya kuanza maisha. Pia kama ni bibi
harusi mtarajiwa makala hii inakuhusu. Nimefanya kazi kubwa ya kutafiti katika
maduka ya vifaa vya jikoni na kukuandalia orodha ya vifaa vya msingi kabisa vinavyotakiwa
kuwepo jikoni kwa ajili ya kukuwezesha kuandaa chakula katika maisha yako hayo
mapya.
Nia hapa ni kuonyesha orodha ya vifaa vya kawaida kabisa
vya msingi vya jiko dogo la kisasa.
Ni rahisi kuangukia kwenye ushawishi wa
muonekano lakini kitu kimoja cha kujua kwa kweli ni kuwa hauna haja ya kuvunja
benki ili kuwa na vifaa vya jikoni vya kiwango. Orodha hii ya vifaa vya msingi jikoni inaweza
kubadilika kutokana na hitaji la mhusika. Pia vyombo vya mezani kama vile
sahani vijiko na glasi vinategemea zaidi ladha ya mtu binafsi na kwa sababu
hiyo sijaviorodhesha hapa. Kwa hivyo vifaa vya
msingi vya jiko dogo la kisasa ni kama vifuatavyo:
Visu
Kisu kikali cha mpishi ni moja kati ya
vifaa muhimu zaidi jikoni, na kama utanunua kilicho sahihi kitatumika kwa miaka
mingi. Nunua visu vya jikoni ambavyo havishiki kutu.
Ubao wa kukatia
Ubao sahihi wa kukatia utafanya visu vyako
vidumu, na rahisi kusafishika. Kuna aina nyingi za mbao hizi kama vile plastiki,
miti na hata glasi.
Kifungulia chupa na makopo
(opener)
Nunua ambayo unaweza kufungulia chupa na
makopo ya aina tofauti tofauti. Nzuri ni ile iliyo rahisi kwa matumizi.
Kisaga vyakula (Blender)
Kama kawaida nunua ambayo ni rahisi
kutumia na yenye kazi nyingi tofauti ambapo utaweza kusaga vyakula vyako na
kutengeneza juisi.
Vikaangio na masufuria
Iwe uko singo au ni wanandoa wapya kwa
kuanzia unahitaji vikaangio japo viwili na sufuria nne hadi sita. Sokoni vikaangio
na sufuria zipo zilizotengenezwa kwa material
nyingi mno. Nunua ambazo hazing’ang’aniani na chakula (nonstick).
Stovu
Watengenezaji
wengi wameunganisha stovu na tanuri ukinunua mbayo unaweza kutumia nishati
zaidi ya moja itakuwa ni busara zaidi.
Jokofu
Kwa
maeneo mengi ya nchi yetu walau inahitajika kuwa na jokofu kwa ajili ya
kuhifadhia chakula kisiharibike. Kwa kuanzia si mbaya ukawa nalo dogo kwenye
jiko lako hili la kuanzia maisha.
Kipasha chakula
(Microwave)
Hiki
kinafanya kazi kubwa ya kupashia na hata kupikia baadhi vya vyakula. Habari
njema ni kuwa zipo za bei rahisi kabisa. Ni rahisi kutumia na wengi wanapendelea
kuziweka juu ya kaunta ya jiko. Huna haja tena ya kupashia chakula kwenye
sufuria.
Kikausha mikate (Toaster)
Hiki nacho kwa wengi wanaopendelea kula
mikate iliyokaushwa huwa wanakiweka juu ya kauta.
Mabakuli/Vikontena
Wanasema
mapishi ni sanaa, sio? Kuwa na mabakuli na vikontena ndani ya jiko lako la
kuanzia maisha vitakusaidia katika maandalizi ya mapishi na hata vikontena
vitakusaidia kupashia na pia kuhifadhia vyakula kwenye jokofu.
Kindoo cha
uchafu
Unapoandaa
chakula na kuosha vyombo lazima utahitaji hiki kindoo kwa ajili ya kuwekea
uchafu. Ni muhimu kiwe kile cha mfuniko wa kujifunga chenyewe.
Jiko
lenye vifaa vya msingi vinavyopaswa kuwepo jikoni ni rafiki kwa mpishi.
Unapokuwa na vifaa sahihi na unajua jinsi ya kuvitumia, unaweza kuelekeza akili
yako kwenye chakula unachoandaa. Kama nilivyosema awali vifaa hivi vinaweza
kuongezeka kutegemea na mhusika na mazingira unaweza kuwa na vifaa hivi vya
msingi jikoni kwa kuanzia na baadaye ukaongeza kidogo kidogo kwa kadri ya
mahitaji yako. Mpishi mzuri anatumia vifaa tofauti tofauti na mwishoni
anapata vile hasa anavyohitaji.
Makala hii
imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa
makazi na pia ni mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au
maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com
No comments:
Post a Comment