Wengi tutakubaliana kuwa zulia la
ukuta kwa ukuta sio sahihi kuwekwa jikoni, ila kizulia cha kutupia kina faida
kadha wa kadha jikoni. Kizulia hiki kinasaidia kuepusha miguu na sakafu ya
baridi na kinaongeza rangi, hata kiwe kidogo namna gani. Yote kwa yote sababu
kuu yaweza kuwa ni kwa ajili ya burudani ya miguu na kuiepusha na baridi. Kama
unaweza kusikia baridi ya kukera kwenye nyumba yako mwenyewe basi ni ukakasi. Kuweka
kizulia jikoni kunakamilisha sakafu na mvuto wa jiko. Vinginevyo uwe unapenda
sana rangi kiasi kwamba umepaka kabati zako za jikoni rangi ya kung’aa kama
vile pinki, kijani ama nyekundu.
Kizulia cha kutupia kinaweza kuleta
rangi bila kukufanya utumie hela nyingi, kama hii ndio sababu ya kuamua kuweka
kizulia jikoni hapa basi ni dondoo chache za kukusaidia kupata kilicho sahihi.
Kuchagua kizulia sahihi kwa ajili ya
jiko, ni vyema kufahamu nia yako kuu ya kuamua kukinunua. Inaweza kuwa ni kwa
ajili ya kuepusha miguu na ubaridi wa sakafu au kuongeza staili, rangi na mvuto
kwenye sakafu ya jiko. Pia fikiria ukubwa na umbo la kizulia ambacho kitafaa
zaidi kwa nafasi iliyopo. Usisahau kuzingatia vifaa vilivyotumika kutengenezea kizulia
utakacho na kufahamu ni utunzaji kiasi gani utakaohitajika. Chagua kizulia
ambacho hakitelezi (hakikimbii sakafu) kwa ajili ya sababu za kiusalama.
Hasa kama sakafu ya jiko lako ni
laini, yakung’aa na inayoteleza, ni muhimu sana kuchagua kizulia chenye mnato/mpira
kwa chini kinaposhikana na sakafu. Mpira huo utasaidia kizulia kikae mahali
pamoja kisihame hame kinapokanyagwa, ambapo kinaweza kusababisha mtu kuanguka.
Chagua
mahali sahihi pa kuweka kizulia chako cha jikoni. Ni wapi unapotumia muda
mwingi unapokuwa jikoni? Pengine ni
mbele ya sinki, kwa hiyo ni kuwa utachagua kuweka kizulia eneo hili. Au labda
una eneo kubwa la kutembea kwenye sakafu ya jikoni. Basi angalia mahali hapo
kati unapoweza kutupia kizulia chako ili kilete burudani ya miguu maeneo
kadhaa. Vile vizulia vyembamba virefu vinafaa zaidi wa jiko lenye sakafu ndogo.
Kama lengo lako kuu la kuhitaji
kizulia jikoni ni kuondoa ubaridi na kuleta nesa nesa ya miguu, basi unene wa
kizulia unahusu. Utahitaji mbonyeo kati ya sakafu ngumu na miguu yako kwa
burudani. Ulaini wa kizulia pia unaepusha miguu yako na baridi la sakafu ya
marumaru au mbao au hata saruji. Hakuna anayetaka kuwa kwenye maumivu wakati
akiosha vyombo!
Chagua
manyonya sahihi, iwe ni sufi au pamba. Kizulia ambacho kinasafishika kirahisi
kwa sabuni na maji. Urahisi wa kusafisha ni lazima ukumbukwe kwenye kuchagua
kizulia cha jikoni, hasa kwa vile vinavyowekwa chini ya sinki au mbele ya stovu
au jokofu. Vizulia vya sufi vinaweza kuwa
chaguo sahihi kimuonekano ila kwa kawaida vinashika madoa kirahisi na vinahitaji
usafishaji wa kitaalam kwahivyo ni vyema kuweka vizulia vya aina hii kwenye
vyumba vingine nyumbani ila sio jikoni au chumba cha kulia chakula, anasema
muuzaji Aisha Mbegu. Vizulia vya kufumwa kwa mimea ya asili kama vile katani au
majani ya baharini vinaweza kuwa chaguo sahihi kwa ajili ya kuweka chini ya
meza ya kulia chakula, kwa ajili kwa kawaida ni rahsisi kuvifuta na kusafisha
hata kwa kufagia.
Haijalishi utaamua kuchagua kizulia
cha jkoni kilichotengenezwa kwa vifaa vya aina gani, kuchukua kipimo cha eneo
unalotaka kuweka kizulia ndani ya jiko lako itakusaidia kupata kilicho sahihi. Wakati
wa kuamua aina za vizulia, jitahidi kutafakari rangi, na ni kwa namna gani
ukubwa na muundo utakavyogusa muonekano
mzima wa jiko lako.
Wacha kizulia chako kitengeneze
stori. Chagua ambacho kitaongeza uzuri kwenye jiko lako. Sakafu za jiko huwa
zinapooza, kizulia kinaweza kuongeza uchangamfu na ladha binafsi kwa kuunganisha
rangi za jiko pamoja. Kama nilivyosema kabla, chagua kizulia kitakachoongeza
rangi, ambapo ni rahisi kubadilisha kizulia ili kuondoa muonekano wa jiko utakapochoka
zile rangi zake za kudumu ulizozizoea.
Hongera kwa kufanya eneo kla sakafu
ya jiko lako kuwa na mvuto, nesanesa na budurani! Utakapoweka kizulia cha
jikoni hutatamani kukiacha.
Makala hii
imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa
makazi na pia ni mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au
maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com
No comments:
Post a Comment