Majira haya ya kipupwe upepo ni mwingi na kazi ya usafi inaongezeka kwa ajili takataka nyingi kwa mfano majani makavu na vumbi zinapeperuswa kila mahali na wengi wanaofanya usafi hasa wa nje ya nyumba wanalalamika kuwa mazingira yanachafuka muda mchache tu baada ya kusafisha. Wengi wetu wanaliona hili na huku jua likiwa kali. Haijalishi unajali mazingira kiasi gani bali kuwa eneo ambalo limesafishwa vizuri kunakupa hisia za ukaribisho na kuhuisha nafsi na ni muonekano chanya kwako. Kuwa mazingira safi kunaongeza nguvu chanya kwenye mwili na mazingira yako. Ukiweza kudumisha usafi kwa kipupwe hiki basi utakuwa umeweza kutengeneza nguvu hii.
Lengo ni kuishi burudani na mazingira yako, ili nguvu iliyopo kwenye mazingira hayo ifanye kazi upande wako kuliko kinyume chako. Kwa jinsi tunavyoguswa na mazingira yetu ndivyo pia tunavyoakisi maeneo haya.Wengi wetu tulishaingia ndani ya jengo au chumba na mara hiyohiyo tukajihisi kuchefukwa. Kinyume na hapo, vilevile wengi tulishaingia maeneo na kutufanya kujisikia burudiko na utulivu wa nafsi. Kuwa katika eneo safi na tulivu kunaleta uwiano na starehe ndani ya mazingira hayo.
Katika mazirngira kitu nambari moja kinachozuia utengenezwaji wa nguvu chanya ni mrundikano. Mrundikano unaweza kutufanya kujisikia kuelemewa, msongo, kuchanganyikiwa na kukwama. Mrundikano ni pamoja na kitu chochote ambacho hakipendwi tena au hakitumiki, hakiko kwenye mpangilio, vitu vingi mno kwenye eneo dogo, ujazo na ujazo, miradi ambayo haijakamilika, kila kitu kilichopo kwenye hali ya kuvugu na/au kila kitu kichafu.
Tembea kuzunguka nyumba yako – nje na ndani. Fungua milango ya makabati, angalia kila mahali. Je una mlima wa makorokoro nyuma ya nyumba yako? Kwa sababu tu huuoni mrundikano huu kila siku, haimaanishi hauko pale! Vitu vinavyokuzunguka vinakusemea ulivyo iwe vinaonekana au havionekani. Kuepuka kuelemewa wakati ukiwa unajaribu kuondoa mrundikano ni vyema kufanya zoezi hilo hatua kwa hatua. Hatua ya kwanza ni kuigawa kazi kwenye mafungu madogo dogo. Chagua kabati moja au shelfu kama hatua yako ya kuanzia. Jipongeze pale unapomaliza. Halafu nenda eneo linalofuata.Unaweza ukawa na muda maalum wa kushughulikia eneo moja kwa siku. Jambo la muhimu ni kuwa weka mikakati ya kazi ambayo itawezekana. Kama ukisubiri muda wa kutosha kufanya kazi yote pamoja, hautakaa upatikane – na hicho ni kisingizio cha kutokuanza kabisa.
Wakati ukianza kazi yoyote ya kuondoa mrundikano, panga kuchambua vitu hapo hapo ulipo. Kusanya (au weka kwenye maboksi) vitu vya kundi moja; kwa mfano, vitu vya kutupa, vitu vya kupeleka stoo, vitu vya kugawa, vitu vya kuuza, vya kuweka masijala na kadhalika. Ukishakuwa umechambua, sasa ni wakati wa kupeleka kila kimoja kunakohusika (vya kuuza unaweza kuhifadhi stoo kwa muda!). Sasa tafuta makao ya vile unavyohitaji. Huenda ni wakati wa kununua mifuko au vikontena kwa ajili ya vitu hivyo. Ndiyo njia pekee kwamba ni vyema kununua vikontena baada ya kujua ni nini unataka kuweka ndani. Baadhi ya watu wanafanya makosa kwa kununua kontena kabla ya kuchambua vitu na hii inafanya visiwe na ukubwa sahihi au pia navyo kuwa mrundikano vilevile.
Je, unakuwa na wakati mgumu wa kuachilia vitu? Unahifadhi vitu kwa labda “lolote litatokea”? Je, unahifadhi zawadi ambazo hujawahi kutumia kwa sababu hutaki kuwavunja moyo waliokupa? Je, unajisikia vibaya usipozungukwa na vitu vingi? Je, unahifadhi nguo ambazo hazikutoshi kwa miaka 10 kwa wazo kwamba utazivaa tena baada ya kupungua kilo 7? Je, umehifadhi vitabu vya hadithi ambazo huzikusisimui tena? Utakapojibu maswali haya kwa uaminifu utaanza kufahamu ni wapi mrundikano ndani ya makazi yako unapotokea.
Kuachilia vitu ambavyo hatuvitumii tena, hatuvihitaji wala hatuvipendi ni hatua muhimu ya kuondoa mrundikano na kuanza kusafisha. Inaweza kuwa ngumu sana kwa baadhi. Kama unahitaji msaada kwenye huo mchakato, shika kifaa ambacho kwa namna yoyote ile hakikusaidii tena, kiambie asante kwa namna ambayo wakati fulani kilikusaidia kwenye maisha yako, na baada ya hapo kiachilie. Kumbuka kua kuachilia vya zamani kunaleta nafasi ya vipya. Inaonyesha imani ya yatarajiwayo.
Kuna wengi wanaoweza kufaidika na usivyohitaji. Je ni vyema kushikilia kitu ambacho hutakaa ukitumie lakini unakiweka kwa kuwa nyanya yako alikupa miaka 15 iliyopita ,au ni busara kumpa mtu ambaye atakitumia na kukithamini? Kwa kuachilia vitu kwenda kunakohitajika, unaondoa mrundikano na unajisikia vizuri kwenye jambo hilo.
Kipupwe ni msimu mzuri wa kuondoa mrundikano. Kwa jinsi unavyyoondoa mrundikano kwenye mazingira yako ndivyo unavyotengeneza nguvu chanya kukuzunguka. Badilisha maisha yako kwa kuondoa mrundikano!
Makala hii
imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa
makazi na pia ni mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au
maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com
No comments:
Post a Comment