Thursday, October 30, 2014

My article for newspaper: Kupamba ndani nafuu na haraka

Njia za gharama nafuu na haraka za kubadilisha muonekano wa ndani ya nyumba yako.


Watu wengi wanafikiria kuwa kupamba ndani ya nyumba ni jambo kubwa na ambalo linahitaji hela nyingi. Lakini hii sio kweli, mtu anaweza kutafiti njia za kupamba nyumba kwenye mitandao au majarida ya mapambo ya nyumbani  na kuona ni njia zipi zinazoweza kumfaa kwa gharama aliyo nayo. Makala hii ni mojawapo ya vyanzo vitakavyokupa mawazo ya njia rahisi na za haraka zaidi za kupamba ndani ya nyumba yako kwa namna maridadi kabisa.

Kabati la mapambo ni njia mojawapo ya gharama nafuu na ya haraka ya kupamba ndani ya nyumba. Kabati hili unaweza kulitengenezersha kwa fundi kwa mtindo unaotaka wewe mwenyewe iwe ni kwa sehemu kubwa kuwa ni kioo kitupu au mchanganyiko wa mbao nusu na kioo nusu. Linaweza kuwekwa sehemu ya kona ya chumba.
Linapokuja swala la mapambo ya kabati la mapambo, eneo la ndani ndio la kujali zaidi. Pamoja na mtindo wa kabati husika vioo pamoja na taa ya ndani ya kabati vinamaliza kila kitu! Mapambo ya aina mbalimbali huwekwa ndani ya kabati hili na kuleta muonekano wa kuvutia. Na pia wengine hupendelea kuweka glass za kifahari za mvinyo za aina ya crystal na hii inalipendezesha mno kabati kwa kweli. Tunu sio kitu ambacho umenunua karibuni kwa hela nyingi. Ni kitu ambacho kina thamani kwako zaidi ya pesa inavyoweza kununua. Inaweza kuwa ni sanaa uliyopewa toka kwa bibi na imepitia vizazi kadha wa kadha hadi kukufikia wewe au inawezekana ni kitu kilichokuwa sehemu ya maisha yako ya utotoni au kitu maalum ulichopewa na mtu maalum. Ukizungusha macho yako kukitazama kinakupa burudiko la nafsi.

Ndani ya kabati la mapambo waweza weka pia mdoli wako ambao unadhani ni wa kipekee na unafaa kuwepo hapo. Pia waweza weka vitu mbalimbali kutoka sehemu tofauti za dunia. Zingatia kua huna haja ya kusongamani kila sanaa uliyonayo kwenye kabati lako la mapambo. Hakikisha unaacha nafasi kati ya kitu na kitu ili isilete muonekano wa mrundikano. Chochote ambacho unadhani kitafanya kabati lako lipendeze waweza weka humo.

Njia nyingine ya kupamba ndani kwa gharama nafuu na kwa haraka ni kwa kutumia maua ya kutenengeneza (maua mfu). Maua na mimea inafanya muonekano wa mahali uwe wa kuvutia. Mtu anaweza kuweka mimea na maua kadhaa ya kutengeneza katika sehemu tofauti tofauti za nyumba yake. Staili na rangi ya maua na mimea hii iendane na rangi ya chumba cha nyumba. Maua hayo yanaweza kuwekwa sakafuni au juu ya meza vilevile.

Mtu anaweza kutumia vibebeo vya mishumaa kupambia nyumba yake na ikaonekana maridadi. Unaweza kutafuta aina mbalimbali ya vibebeo hivi kwenye maduka ya mapambo ya ndani na unaweza kuchagua vya mbao au vya kioo.

Mito ni njia nyingine ya kupamba kwa gharama nafuu na kwa haraka. Unajisikia burudani ukiwa na mito ya staili na maumbo mbalimbali. Unaweza kutupia mito kadhaa ya  mapambo kwenye seti zako za sofa ambapo zitaleta matokeo makubwa na itakuwa vyema zaidi kama ukitumia mito ya rangi nyekundu na ya chungwa.

Badilisha muonekano wa madirisha kwa kubadilisha pazia na fimbo. Hii sio usumbufu kama ambavyo unaweza kufikiri kwani kuna maduka mengi yanayouza pazia ambazo zimeshonwa tayari. Na kwa swala la fimbo zake kwa ajili tayari kuna vishikizo vilivyotobolewa,  ni kiasi tu cha kuondoa fimbo ya mtindo mmoja na kupachika nyingine ya mtindo tofauti bila ya kutoboa ukuta tena.

Hizo ni njia za gharama nafuu na haraka zaidi za kupamba nyumba yako. Jaribu mojawapo na utarudi kunishukuru. 


Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ni mjasiriamali  upande wa usafi wa nguo, mazulia na magari; pia ana mapenzi makubwa ya muonekano wa nyumba. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com

No comments:

Post a Comment