Jinsi ya kupamba chumba cha kulala
Kwa nyumba nyingi chumba
cha kulala ni chumba binafsi zaidi. Ni chumba pia ambacho
kina vitu vingi zaidi binafsi. Kinaweza kuwa kama kiota cha mahaba au mahali
patakatifu pa kulala na kupumzika. Pia kinaweza kuwa chumba cha kuchangamka na
kutuliza kwa watoto, kwa jinsi wanavyokuwa wakigundua kuwa wanamiliki chumba
chao wenyewe.
Kupenda
kufurahisha marafiki, majirani na wageni; wenye nyumba wengi wanamalizia nguvu
zao kupamba vile vyumba vya kuonekana na hadhara ndani ya nyumba. Umefika
wakati wa kuwa mchoyo na kuelekeza nguvu zako kwenye chumba cha kulala. Juu ya
yote ni kuwa kabla ya kuoga kujiaandaa kutoka ni lazima kwanza utokee
kitandani.
Kwanza
kabisa anza na kitanda kwa ajii kitovu cha chumba chochote cha kulala ni kitanda.
Ni wazi kuwa kitu cha kwanza cha kuzingatia kwenye kitanda itakuwa ni godoro,
lakini usisahau ubao wa kichwani. Ni ngumu kudharau umuhimu wa sababu za
kisaikolojia katika kupata usingizi mwororo. Hisia na hata muonekano wa kitanda
chako wakati unapoingia humo inaweza kuelezea ni namna gani unavyojisikia wakati
unapotoka humo.
Kwa upande wa sakafu chaguo zuri zaidi kwa ajili ya chumba cha kulala ni
zulia na mara zote imekuwa hivyo. Hamna kitu kizuri kama kuamka na kuweka miguu
yako kwenye sakafu ambayo inaelekea kuwa na hisia kama za kitandani kwa kupata
joto lile lile mithili ya la kitandani. Wengine hupenda kuweka sakafu za
marumaru na mbao lakini eneo la pembeni mwa kitanda wengi wanapenda kuweka
zulia.
Wazo la mwanga katika chumba cha kulala kwa baadhi linadharauliwa. Taa zisizokuwa
na maridadi na balbu za juu ya kichwa tu zimeanza kupoteza mvuto kwenye chumba
cha kulala cha kisasa. Taa za vivuli za kuweka juu ya vimeza vya kando mwa
kitanda na za ukutani za maridadi ndio zinaendana na wakati kwa chumba cha
kulala, kwa ajili ya mwanga wa chumba hiki kwa matumizi ya wakati wowote iwe ni
mchana, jioni au usiku.
Taa ndogo zinaweza kuwekwa kwa ajili ya kutumia muda maalum ambapo hutaki
kuwasha taa zote kwa mfano wakati wa kusoma au kushikisha kifungo.
Kwa vyumba vidogo vya kulala mara nyingi vinafaidika na uwepo na makabati
ya nguo, madroo na shelfu kwa kusaidia kuhifadhi na kuweka mpangilio. Baadhi ya
vitu vidogo dogo na nguo vinapoukuwa vimewekwa kwenye sehemu hizi za kuhifadhia, chumba kinaonekana nadhifu.
Mara
nyingi rangi za mwanga zinashauriwa
zaidi kwenye chumba cha kulala kwa ajili zinaleta hisia ya mapumziko. Rangi za
vitambaa vya malazi viendane na rangi nyingine hapo chumbani na hata zile za
samani. Shuka za rangi na maua ya kuvutia zinunuliwe ili kuongeza uzuri wa
chumba.
Komfota
lenye rangi nzito litaendana na samani au ubao wa kichwani wa mbao. Hii pia ni
kweli kwa mapazia.
Wakati
huo huo kumbuka kuweka samani zenye ukubwa na wingi wa kuendana na ukubwa wa
chumba. Kabla hujanunua samani hizo ni vyema kwanza kufahamu mpangilio wa
sakafu na ukubwa uliopo.
Kutengeneza bajeti ni muhimu kwa mradi wowote wa maboresho ya nyumbani. Kujipa wastani wa gharama inayohitajika itakusaidia kuamua ni nini kinachoweza kufanyika na kipi si kipaumbele. Baadhi ya shughuli kwenye mradi huu unaweza kufanya mwenyewe, kwa baadhi itakubidi utafute mtaalam. Kama kipaumbele chako ni ukuta kwa mfano, basi unaweza kutafuta mtalam wa rangi akapaka, ilihali ukitandika zulia mwenyewe. Vyovyote utakavyoamua, ni wakati wa kufanya chumba chako kuwa chako tena.
Kupamba chumba cha
kulala ni shughuli mojawapo ya maboresho ya nyumbani ambayo inaweza kuhuisha
tena afya yako na mahali unapoishi.
Makala hii
imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa
makazi na pia ni mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au
maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com