Tuesday, December 23, 2014

My Article for Newspaper: Malengo ya 2015 Nyumbani Kwako

Mazingira ya nyumbani kwako yasaidie kufanikisha maazimio yako ya mwaka mpya
Ni wakati mwingine tena wa mwaka ambao wengi wetu wanapenda kufanya mabadiliko kwenye maisha yao. Je umeshafikiria mabadiliko ya mwaka mpya kwa ajili ya kiota chako? Japo mabadiliko haya yanajulikana na wengi zaidi kama maazimio, kwa kutia msisitizo zaidi makala hii itayaita malengo. Malengo yanatamkwa kwa kusisitiza wakati uliopo ni nini tamanio lako (kwa mfano kuamua kubadili mpangilio wa fenicha za sebuleni kwako ili kuwezesha kunogesha zaidi mazungumzo) wakati maazimio yanatamka ni nini ungependa huko mbeleni ya kuwa unaenda kufanya nini wakati ujao.
Mara nyingi malengo (au maazimio) ya mwaka mpya yanatupiliwa mbali hata kama nguvu za kutosha ziliwekwa ili kuhakikisha yanafanikiwa. Moja ya sababu za malengo kutofanikiwa ni mazingira ya nyumbani kwako kutosaidia kuwezesha mafanikio ya malengo hayo. Kama unataka kufanya mabadiliko ndani ya maisha yako bila kuhusisha mazingira yako kufanikiwa ni mbinde. Kwa maana ya kwamba kama unaweka malengo yako ya mwaka 2015 kwa ajili ya makazi yako na ukayaacha mazingira yalivyo, ni ngumu sana kubadili chochote. Hata matangazo kwa mfano ya kujikinga na maambukizi ya VVU yanaonyesha uhusiano kati ya maambukizi na mazingira fulani ambayo yanachochea maambukizi hayo.
Kanuni ya malengo kuwa na uhusiano na mazingira inahusika karibia katika kila kitu. Kama unataka mwaka huu uwe tofauti basi unatakiwa kuweka mazingira ya kuwezesha malengo yako.
Je mazingira yako yanakusaidia kupata kile unachokihitaji? Kwenye mazingira ya nyumbani kwako vitu ambavyo havijakaa mahali pake au vimekaa mahali ambapo havifanyi kazi yake au havitumiki tena vinakukwamisha kutimiza malengo yako hapo nyumbani. Tembelea kwenye makabati ya nguo na vyombo angalia kwa umakini kuona ni vitu gani vya kuhifadhi, vya kugawa ama vya kutupa. Fanya hivyo kwa nia ya kupata nafasi ya kile tu kitakachosaidia kufanikisha malengo yako.
Pengine lengo lako la mwaka mpya ni kutokula hovyo kwa nia ya kupungua uzito. Je mara zote unaingia nyumbani kwa kupitia mlango wa nyuma ambapo unaingilia moja kwa moja jikoni? Kumbuka kanuni kuwa unachokiona mwanzo kinagusa zaidi akili yako, kwa hiyo kama mara ungiapo ndani unakutana na jokufu, chakula na kadhalika utapata hamu ya kula hapo hapo.
Mahusiano mengi yanaweza kuboreshwa kwa mapambo ya nyumbani hasa katika swala la kuwasiliana. Je chumba cha kulala cha wakuu wa familia ni mahali patakatifu kwa wawili? Hakikisha vitu kama taa, vimeza, na viti kwenye chumba hicho viko viwili viwili.
Au lengo lako mwaka mpya ni kuwa na wageni wengi zaidi nyumbani? Hakikisha basi mlango wa mbele unaonekana na kuna njia ya wazi ya kuingilia. Taa zinazomulika njia ya kuelekea mlango huo ziwe zinafanya kazi. Pitia mlango wa mbele kama mgeni mtarajiwa uone kama kila kitu kiko sawa. Je njia hiyo inakaribisha? Na sebule yako je nayo inavutia kwa ajili ya wageni wako wengi ambao unapenda kuwaalika nyumbani mwaka mpya ?
Kwa wale ambao azimio lao kuu la mwaka 2015 ni kupamba nyumba zao hakikisha unachagua rangi kwa umakini, fikiria mpangilio wa fenicha je zinawatendea haki watumiaji wa chumba husika. Angalia vitu ambavyo inabidi uvifanyie kazi ili kuboresha muonekano wa makazi yako. Kama kwa mfano sakafu ya sebule yako ni ya marumaru na unachoka kusugua na kusafisha kila siku na unakiri kuwa ni ngumu kuifanya iwe safi; basi weka zulia kubwa ambapo utasafisha kwa mashine ya upepo mara mbili au tatu kwa wiki.
Ikiwa unaazimia kutojaza vyombo vichafu kwenye karo basi mwaka ujao lenga kuosha chombo mara baada ya kukitumia. Na hata hakikisha wanafamilia wengine pia wanafanya hivyo.
Huenda kijani kinakubariki lakini huna eneo kubwa ya kuweza kuwa na bustani za ardhini. Otesha basi bustani za kwenye vyungu walau ukifungua pazia la chumba cha kulala kunapopambazuka ukutane na kijani. Azimia kupamba ndani mwako kwa maua freshi japo mara moja kwa mwezi.
Kweli, baadhi ya mabadiliko ya nyumbani kwako unaweza kuhitaji kutafuta msaada, lakini kuna mabadiliko mengi sana ambayo hayahitaji gharama lakini yanahitaji muda na nguvu ( na pengine kaujuzi)  kwahiyo kwa 2015 kwa nini usiazimie kupamba mwenyewe? Unaonaje? Ni azimio moja zuri kwa ajili ya makazi yako ambalo unaweza kutekeleza. Fanya usafi mkubwa ndani ya nyumba yako mara moja kwa mwezi ( weka tarehe kwenye kalenda yako na isismamie). Mwanamke unatakiwa upende usafi na usiwe mvivu. Shirikisha na wanafamilia wengine pia.
Hii inaweza isikubalike kwa baadhi ya watu ila ni mawazo binafsi kuwa azimia kila anayeingia ndani avue viatu mlangoni. Viatu vya wanawake vilivyo na visigino vya ncha kali mara nyingine vinakwaruza sakafu za marumaru na mbao na kuacha alama na vile vya wanaume baadhi vina soli zinazoacha rangi sakafuni na hivyo kufanya sakafu ionekane zee kuliko kawaida.
Mwaka huu lenga kuweka nyumba yako nadhifu kila mara kama vile unategemea mgeni wa heshima!

Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi ni mjasiriamali upande wa usafi wa magari, nguo na mazulia; pia ana mapenzi makubwa ya muonekano wa makazi. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christinesdaughter@yahoo.com

Monday, December 22, 2014

Laundry Talk: Umuhimu wa Kutumia Bleach


As ninafanya biashara ya dry cleaning na laundry nimeona kuwa hakuna mbaya nikiwa na share na wewe tips za mambo hayo. So kuna mambo elfu moja na moja kidogo ya kuongelea kuhusu usafi wa nguo tatizo nadhani ni muda mchache uliopo!

Naanza na kwanini tutumie bleach? Nyeupe zizidi kuwa nyuepe zaidi, inaondoa udongo na inaua vijidudu.


Zaidi ya maelezo ya kwenye chupa bleach inatakiwa kuchanganywa na maji kabla ya kusweka nguo endapo unafua kwa mkono, baadhi ya watu kwa kutojua wanaweka nguo kwanza halafu wanamimina bleach juu ya nguo, hii ni makosa as inaweza kuunguza nguo endapo utaimimina moja kwa moja juu ya nguo.

Of course, kama unatumia mashine una ile sehemu ya ku dispense bleach, kwa hivyo unamimina tu pale kwa maana hiyo huna haja ya kuchanganya maji na bleach manually.

Kabla hujatumia bleach kwenye nguo hakiksha kwanza unasoma label ya nguo, kwa ajili kuna baadhi zinasema kabisa "No Bleach" - kwa maana hiyo usitumie bleach kwenye nguo yenye label inayosema hivi.

Na usisahau kuwa kuna bleach za kutumia kwenye nguo za rangi pia ...watu wengi hawajui hili, kwa mfano unaona zile chupa za jik za rangi ya bluu? hizi ni kwa ajili ya nguo za rangi.

TAHADHARI wakati wa kutumia bleach - kuna dondoo mbalimbali zinatolewa kwa ajili ya kufua nguo zitakate zaidi kama vile kutumia limao, vinegar na kadhalika. Kuchanganya vitu hivi na bleach kunaweza kuzalisha kemikali zitakazoharibu nguo zako, ambapo usingependa litokee hili.

Sunday, December 21, 2014

...mjini tumekuja kutafuta maisha...

wakati wa sikukuu tunachapa lapa kama hivi...usisahau chimbuko lako mdau...watu wangu wadogo washasepa zao xmas hiyoooooo yaja...




Thursday, December 11, 2014

my article for newspaper: kuhifadhi taulo na ugeni

Jinsi unavyoweza kuhifadhi taulo za bafuni kwa ajili ya wageni watakaokutembelea msimu huu wa sikukuu.

Moja ya faida za kipindi cha sikukuu  ni fursa ya kufungua nyumba yako kwa wageni ambao hamjakaa pamoja mwaka mzima.  Kama utakuwa na wageni nyumbani msimu huu wa sikukuu, makala hii inakuhusu. Mahoteli yanafanya wageni wao wajisikie spesho kwa ajili wanafahamu jinsi ya kuwafanya wajisikie  nyumbani kwa kuwapatia mahitaji muhimu. Wewe pia unaweza wafanya wageni wako wajisikie kama wameshukia kwenye hoteli ya kitalii wanapokuwa nyumbani kwako, kwa ajili tu ya buduriko wanalopata wanapokuwa kwenye chumba au vyumba vyao vya wageni hapo kwako.

Ni  bafu chache zenye sehemu ya kutosha kwa ajili ya kuhifadhi taulo za wenyeji na wageni kwa wakati mmoja, na huenda unafikiria ni jinsi gani utahifadhi taulo za wageni wako watakapokutembelea. Lakini usijali kwani hata kama bafu lako ni dogo namna gani njia mojawapo kati ya hizi itakufaa kutundika ama kuhifadhi taulo za wageni wako.

Kuweka fimbo za kutundika taulo kwenye ukuta wa bafu ama nyuma ya mlango (uwe wa mbao kwa uimara) ni njia rahisi zaidi ya kuhifadhi taulo za bafuni. Fimbo hizi hazichukui nafasi kubwa na wala hazina marembo kwahivyo ni suluhisho tosha kuhifadhi taulo kavu na hata zile zenye unyevu. Fimbo za taulo zinaruhusu taulo kukauka kwa usafi zikiwa zimetundikwa kwa kukunjwa nusu. Fimbo za bafuni za kuwekea taulo zinasaidia mambo makubwa mawili: kwanza, zinaweka taulo kavu na safi kwa jinsi ambayo ni rahisi kuchukua na kutumia; pili, zinatandazwa taulo zenye unyevu na kuzifanya kukauka kirahisi, hivyo kuzuia kuota kwa ukungu.

Licha ya kufungwa bafuni fimbo za taulo zinaweza kufungwa pia jikoni kwa ajili ya kuwekea taulo za mkononi.

Muonekano wa fimbo za taulo ni kawaida sana. Ni fimbo iliyosimikwa ukutani ama nyuma ya mlango kwa kutumia mashine ya kutobolea ukuta na taulo huwekwa hapo, hutolewa kutumika na hurudishwa tena hapo baada ya kutumika kwa ajili ya kukauka. Ni muhimu fimbo hizi zimewekwa imara kwakuwa kama tujuavyo taulo zikiwa mbichi zinakuwa nzito na pia mara nyingine fimbo hizi hutumika na watoto kwa utundu wao wa kupenda kubembea kila wapoona panafaa, na pia wazee kujishikilia wakiwa bafuni. Kwahivyo siwezi kuacha kusisitiza kuwa fimbo za taulo ni lazima zifungwe kwenye ukuta wa tofali ama mlango wa mbao kwa ajili ya uimara.

Fimbo za taulo sizo tu zinazoweza kuhifadhi taulo kwa usafi na kuruhusu zile zenye unyevu kukauka. Kulabu (hook) za taulo, susu (rack) za kusimama wima, bangili na ngazi za taulo nazo ni njia nyingine za kuhifadhi taulo za bafuni. Bangili iliyotobolewa ukutani ambapo taulo kadhaa zinatundikwa ni maarufu sana siku hizi na kwenye maduka ya fenicha wanaziita bangili za taulo.

Ngazi za taulo ni chuma kingine kinachoonekana kama ngazi ndogo ambacho hutumika kuwekea taulo,  ni njia mojawapo ya kuhifadhi taulo za bafuni. Je una nafasi kwenye ukuta wa chumba cha kulala cha wageni wako ambapo unaweza kuweka ngazi hii? Ni kiasi cha kuishikilia na braketi juu ili isianguke na unaweza kuhifadhi kwa kutandaza taulo za kuogea. Uzuri wa ngazi ya taulo ukilinganisha na fimbo ni kuwa wakati kwenye fimbo unaweza kuweka taulo zisizozidi 2 kwenye ngazi ya taulo unaweza kuweka hadi taulo 6.

Lakini kuna njia nyingine ambazo hazitakufanya uusumbue ukuta wako ambazo zinaonekana za kimapambo zaidi kwa mfano kuweka susu ya kusimama inayojitegemea kama ile ya kutundika makoti ofsini. Kama chumba cha kulala cha wageni wako kina nafasi kidogo ya ziada basi simamisha susu ya koti kwa ajili ya kutundikia taulo za bafuni. Susu inaweza kutundikwa taulo kadhaa kwa wakati mmoja. Fikiria kuiweka sehemu ambayo inaingiza hewa au vinginevyo wageni wako wawe wanazigeuza mara kadhaa kuwezesha kukauka. Kama susu hii inatundika taulo za wageni tofauti tofauti basi wawe na taulo za rangi tofauti kwa kila mmoja. Hakuna anayependa kushirikiana taulo.

Badala ya ile susu ya kusimama kuna hii nyingine inayofanana na ya kuhifadhia chupa za mvinyo. Kama unataka wageni wako wajisikie kama wako kwenye hoteli yenye hadhi ya nyota tano nenda kistaili zaidi kwa kuhifadhi taulo zao safi zilizobiringishwa vizuri kwenye susu ya taulo. Susu za taulo zina muonekano wa kuvutia kwahivyo kwa upande mwingine ni kama pambo. Taulo safi zinabakia zimebiringishwa vizuri ndani ya susu hadi wakati wa kutumiwa, na hii inachukua nafasi kidogo kuliko ile ya kusimama. Kuhifadhi taulo kwa kutumia susu ya taulo inakubidi uwe ni mtu wa kutumia taulo mara moja tu na kulifua.

Kama ulijisikia kwamba bafu lako ni dogo kiasi kwamba huna mahali pa kuhifadhi taulo za wageni wako msimu huu wa sikukuu hatimaye leo umefahamu njia kadhaa za kuweza kuhifadhi na kutunza taulo wakati huo huo ukiwa unazitumia. Wekeza katika njia mojawapo kati ya hizi ilikurahisisha maisha bafuni sikuzote na hata msimu wa wageni.


Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye anajishughulisha na usafi wa magari, mazulia na nguo aina zote; pia ana mapenzi makubwa ya muonekano wa makazi. Kwa maoni au maswali tuma kwenda christines.daughter@yahoo.com au 0755 200023

...nothing happier than to watch them growing...







Wednesday, December 10, 2014

ideas za makabati ya bafuni

Kila mmoja wetu ana ladha na mahitaji mbalimbali tofauti na mwingine. Wakati baadhi yetu tukiamini kuwa muonekano wa sebule ndio kipaumbele namba moja kwenye makazi yetu, wengine wanajali zaidi ni kwa namna gani mabafu yao yanaonekana, kwahivyo makabati ya bafuni kwa watu hawa ni kitu muhimu zaidi kwao  kwa uzuri na kwa matumizi ya bafu.
Wenye nyumba wengi wanaona uhaba wa eneo la kuhifadhi vitu bafuni kama vile shampoo na vipodozi. Sasa basi yawezekana ulikumbuka hivi wakati wa ujenzi na hivyo kuwa na mababati yaliyojengewa humo humo. Vinginevyo yapo hata ya kusimama peke yake, kama makabati ya bafuni ni jambo muhimu kwako bado hujachelewa, pata mionekano ya makabati haya ambapo staili mojawapo yaweza kukuvutia.




Friday, December 5, 2014

....my babies....

ulishahudhuria msiba ambapo marehemu ana miaka 80 lakini ukashangaa jinsi wanae wanavyomwaga chozi...kumbuka usemi wa kiswahili kuwa mtoto kwa mama hakui...lol




Thursday, December 4, 2014

my article for newspaper: ubora wa tile za bafuni

Umuhimu wa kujali ubora wakati wa kununua marumaru za bafuni


Bila shaka kila mmoja anataka apate bidhaa au huduma kwa thamani ya hela aliyotoa wakati wa ujenzi wa nyumba yake, lakini chaguo la marumaru za bafuni inahitaji kuwa makini zaidi ya hilo. Katika makala hii nitakuwa na Mhandisi David ambaye atatujuza umuhimu wa kuzingatia ubora zaidi ya gharama wakati wa kununua marumaru za bafuni.

Unaweza kuwa umepata marumaru za bei nafuu, lakini zisizokuwa na kiwango. Marumaru za aina hii zitakugharimu kwa kiasi kikubwa muda wote utakaokuwa unaishi kwenye nyumba yako hiyo.
Linapokuja swala la marumaru za bafuni, malighafi, rangi, uimara, mtelezo, na usimikaji ni mambo muhimu zaidi ya kuzingatia, anasema David. Hakikisha kuwa unapata ushauri kwa fundi mwenye uwezo kabla ya kufikia kufanya uamuzi.

Marumaru za bafuni zipo za kuanzia maumbo madogo zenye nyongeza ya border za aina na michoro mbalimbali. Wajenzi wanatafuta marumaru za maumbo tofauti tofauti  kutoka umbo la pembe nne lililozoeleka hadi malighafi nyingine kama mawe ya asili na vioo. Wanapenda pia mabafu yao yawe na muonekano wa  kazi za sanaa zaidi, anasema David. Ila marumaru za bafuni zinafanya kazi kubwa, zinatakiwa kufanya mvuke usisambae vyumba vingine na kulinda kuta zisiharibiwe na ukungu na hali ya umajimaji. Zinatakiwa zizibwe vyema na grout maeneo ya miungio na ziwe na usalama kutembea juu yake zinapowkuwa zimeloa, anasema mhandishi.

Pamoja na mawe ya asili, marumaru bado zitabaki kuwa chaguo maarufu zaidi kwa ajili ya kuta na sakafu za bafuni. Marumaru ngumu zina rangi sawa kwenye unene wake wote, ingawa zina gharama zaidi, na hapa ndipo mnunuzi anapopaswa kuwa makini. Ujue kutofautisha kama unanunua marumaru zilizopakwa rangi kwa juu tu, na hizi ni zile nyepesi na bei yake iko chini. Aina hii ni kuwa baada ya muda si mrefu rangi inatoka kutokana na kukanyagwa mara kwa mara, kwa kuwa rangi imepakwa kwenye eneo la juu la marumaru kwa unene kiasi tu na sio unene wote. Hizi zilizopakwa rangi inakuwa eneo la juu tu mfano barafu kwenye mlima au kwenye keki! Hizi za aina hii zinafaa zaidi kwa mapambo pengine kutengenezea ua la ukutani lakini sio kwa kuhimili shurba za sakafu ya bafuni. Marumaru  ambazo zina rangi hiyo hiyo hadi ndani kwenye kiini na unene wote wa marumaru ni imara zaidi kwa matumizi ya sakafu ya bafuni.

Kwa hivyo muhimu zaidi ni kutumia marumaru hizi ngumu zenye rangi sawa kila mahali kwa ajili ya sakafu na kuchagua za bei rahisi zinazoendana na zile ngumu kwa ajili ya ukuta, anasema David. Usimikaji wa marumaru ni kazi ya sanaa kwahivyo inahitaji fundi mwenye uwezo nayo.

Zaidi ya kuweka marumaru bafuni unaweza kuweka pia jiwe la asili kama vile marble lakini iliyo ngumu. Ubora wa jiwe na usimikaji wake ni muhimu sana. Uwekaji wa jiwe la asili ni wa kitaalam. Kunaweza kuwa na shida ya kufitisha slabu kubwa ya jiwe hilo kwenye maeneo ya kutolea maji machafu na kuingiza maji safi,  na muhimu zaidi ya yote sio kila jiwe la asili linafaa kwenye mazingira ya mvuke na majimaji ya bafuni, anasema mhandisi. Mawe mengine ya asili yananyonya maji na mwishowe kuwa na mipasuko.

Marumaru zitaongeza thamaini ya nyumba yako, kwahivyo kuwa tayari kutumia muda na pesa. Kwa bafu la kisasa na muonekno wa kifahari chagua marumaru zenye rangi za mwanga kama vile nyeupe ukutani huku ukiweka miisho na mpangilio fulani  wenye mvuto kwa baadhi ya maeneo ya ukuta.
Haijalishi ni mtindo gani wa marumaru utakaochagua kwa ajili ya bafu lako, zingatia ubora na usimikaji wa kitaalam kabla ya kufanya maamuzi yoyote. Dondoo muhimu kuliko zote, kabla hujaanza kutengeneza bafu lako angalia thamani ya nyumba yako. Ubora wa bafu uendane na thamani ya nyumba. Kwa kuzingatia hilo utafanya uamuzi sahihi kwa kushirikisha wataalam watakaokufanya usijutie maamuzi yako hapo baadaye.


Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi na pia ni mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com