Mazingira
ya nyumbani kwako yasaidie kufanikisha maazimio yako ya mwaka mpya
Ni wakati
mwingine tena wa mwaka ambao wengi wetu wanapenda kufanya mabadiliko kwenye
maisha yao . Je
umeshafikiria mabadiliko ya mwaka mpya kwa ajili ya kiota chako? Japo mabadiliko
haya yanajulikana na wengi zaidi kama
maazimio, kwa kutia msisitizo zaidi makala hii itayaita malengo. Malengo
yanatamkwa kwa kusisitiza wakati uliopo ni nini tamanio lako (kwa mfano kuamua
kubadili mpangilio wa fenicha za sebuleni kwako ili kuwezesha kunogesha zaidi
mazungumzo) wakati maazimio yanatamka ni nini ungependa huko mbeleni ya kuwa
unaenda kufanya nini wakati ujao.
Mara
nyingi malengo (au maazimio) ya mwaka mpya yanatupiliwa mbali hata kama nguvu za kutosha ziliwekwa ili kuhakikisha
yanafanikiwa. Moja ya sababu za malengo kutofanikiwa ni mazingira ya nyumbani
kwako kutosaidia kuwezesha mafanikio ya malengo hayo. Kama
unataka kufanya mabadiliko ndani ya maisha yako bila kuhusisha mazingira yako
kufanikiwa ni mbinde. Kwa maana ya kwamba kama unaweka malengo yako ya mwaka
2015 kwa ajili ya makazi yako na ukayaacha mazingira yalivyo, ni ngumu sana
kubadili chochote. Hata matangazo kwa mfano ya kujikinga na maambukizi ya VVU
yanaonyesha uhusiano kati ya maambukizi na mazingira fulani ambayo yanachochea
maambukizi hayo.
Kanuni ya
malengo kuwa na uhusiano na mazingira inahusika karibia katika kila kitu. Kama unataka mwaka huu uwe tofauti basi unatakiwa kuweka
mazingira ya kuwezesha malengo yako.
Je
mazingira yako yanakusaidia kupata kile unachokihitaji? Kwenye mazingira ya
nyumbani kwako vitu ambavyo havijakaa mahali pake au vimekaa mahali ambapo
havifanyi kazi yake au havitumiki tena vinakukwamisha kutimiza malengo yako
hapo nyumbani. Tembelea kwenye makabati ya nguo na vyombo angalia kwa umakini
kuona ni vitu gani vya kuhifadhi, vya kugawa ama vya kutupa. Fanya hivyo kwa
nia ya kupata nafasi ya kile tu kitakachosaidia kufanikisha malengo yako.
Pengine
lengo lako la mwaka mpya ni kutokula hovyo kwa nia ya kupungua uzito. Je mara
zote unaingia nyumbani kwa kupitia mlango wa nyuma ambapo unaingilia moja kwa
moja jikoni? Kumbuka kanuni kuwa unachokiona mwanzo kinagusa zaidi akili yako,
kwa hiyo kama mara ungiapo ndani unakutana na jokufu, chakula na kadhalika
utapata hamu ya kula hapo hapo.
Mahusiano
mengi yanaweza kuboreshwa kwa mapambo ya nyumbani hasa katika swala la
kuwasiliana. Je chumba cha kulala cha wakuu wa familia ni mahali patakatifu kwa
wawili? Hakikisha vitu kama taa, vimeza, na
viti kwenye chumba hicho viko viwili viwili.
Au lengo
lako mwaka mpya ni kuwa na wageni wengi zaidi nyumbani? Hakikisha basi mlango
wa mbele unaonekana na kuna njia ya wazi ya kuingilia. Taa zinazomulika njia ya
kuelekea mlango huo ziwe zinafanya kazi. Pitia mlango wa mbele kama mgeni
mtarajiwa uone kama kila kitu kiko sawa. Je
njia hiyo inakaribisha? Na sebule yako je nayo inavutia kwa ajili ya wageni
wako wengi ambao unapenda kuwaalika nyumbani mwaka mpya ?
Kwa wale ambao
azimio lao kuu la mwaka 2015 ni kupamba nyumba zao hakikisha unachagua rangi
kwa umakini, fikiria mpangilio wa fenicha je zinawatendea haki watumiaji wa
chumba husika. Angalia vitu ambavyo inabidi uvifanyie kazi ili kuboresha
muonekano wa makazi yako. Kama kwa mfano sakafu ya sebule yako ni ya marumaru
na unachoka kusugua na kusafisha kila siku na unakiri kuwa ni ngumu kuifanya
iwe safi; basi weka zulia kubwa ambapo utasafisha kwa mashine ya upepo mara
mbili au tatu kwa wiki.
Ikiwa
unaazimia kutojaza vyombo vichafu kwenye karo basi mwaka ujao lenga kuosha
chombo mara baada ya kukitumia. Na hata hakikisha wanafamilia wengine pia
wanafanya hivyo.
Huenda
kijani kinakubariki lakini huna eneo kubwa ya kuweza kuwa na bustani za
ardhini. Otesha basi bustani za kwenye vyungu walau ukifungua pazia la chumba
cha kulala kunapopambazuka ukutane na kijani. Azimia kupamba ndani mwako kwa maua freshi japo mara moja
kwa mwezi.
Kweli,
baadhi ya mabadiliko ya nyumbani kwako unaweza kuhitaji kutafuta msaada, lakini
kuna mabadiliko mengi sana ambayo hayahitaji gharama lakini yanahitaji muda na
nguvu ( na pengine kaujuzi) kwahiyo kwa
2015 kwa nini usiazimie kupamba mwenyewe? Unaonaje? Ni azimio moja zuri kwa
ajili ya makazi yako ambalo unaweza kutekeleza. Fanya usafi mkubwa ndani ya
nyumba yako mara moja kwa mwezi ( weka tarehe kwenye kalenda yako na
isismamie). Mwanamke unatakiwa upende usafi na usiwe mvivu. Shirikisha na
wanafamilia wengine pia.
Hii
inaweza isikubalike kwa baadhi ya watu ila ni mawazo binafsi kuwa azimia kila
anayeingia ndani avue viatu mlangoni. Viatu vya wanawake vilivyo na visigino
vya ncha kali mara nyingine vinakwaruza sakafu za marumaru na mbao na
kuacha alama na vile vya wanaume baadhi vina soli zinazoacha rangi sakafuni na
hivyo kufanya sakafu ionekane zee kuliko kawaida.
Mwaka huu
lenga kuweka nyumba yako nadhifu kila mara kama
vile unategemea mgeni wa heshima!
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi
ni mjasiriamali upande wa usafi wa magari, nguo na mazulia; pia ana mapenzi
makubwa ya muonekano wa makazi. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au
christinesdaughter@yahoo.com
No comments:
Post a Comment