Jinsi
unavyoweza kuhifadhi taulo za bafuni kwa ajili ya wageni watakaokutembelea
msimu huu wa sikukuu.
Moja ya faida za kipindi cha sikukuu ni fursa ya kufungua nyumba yako kwa wageni
ambao hamjakaa pamoja mwaka mzima. Kama utakuwa
na wageni nyumbani msimu huu wa sikukuu, makala hii inakuhusu. Mahoteli yanafanya
wageni wao wajisikie spesho kwa ajili wanafahamu jinsi ya kuwafanya
wajisikie nyumbani kwa kuwapatia
mahitaji muhimu. Wewe pia unaweza wafanya wageni wako wajisikie kama wameshukia
kwenye hoteli ya kitalii wanapokuwa nyumbani kwako, kwa ajili tu ya buduriko
wanalopata wanapokuwa kwenye chumba au vyumba vyao vya wageni hapo kwako.
Ni bafu
chache zenye sehemu ya kutosha kwa ajili ya kuhifadhi taulo za wenyeji na
wageni kwa wakati mmoja, na huenda unafikiria ni jinsi gani utahifadhi taulo za
wageni wako watakapokutembelea. Lakini usijali kwani hata kama bafu lako ni
dogo namna gani njia mojawapo kati ya hizi itakufaa kutundika ama kuhifadhi
taulo za wageni wako.
Kuweka fimbo za kutundika taulo kwenye ukuta wa bafu
ama nyuma ya mlango (uwe wa mbao kwa uimara) ni njia rahisi zaidi ya kuhifadhi taulo
za bafuni. Fimbo hizi hazichukui nafasi kubwa na wala hazina marembo kwahivyo ni
suluhisho tosha kuhifadhi taulo kavu na hata zile zenye unyevu. Fimbo za taulo zinaruhusu
taulo kukauka kwa usafi zikiwa zimetundikwa kwa kukunjwa nusu. Fimbo za bafuni za
kuwekea taulo zinasaidia mambo makubwa mawili: kwanza, zinaweka taulo kavu na safi
kwa jinsi ambayo ni rahisi kuchukua na kutumia; pili, zinatandazwa taulo zenye unyevu
na kuzifanya kukauka kirahisi, hivyo kuzuia kuota kwa ukungu.
Licha ya kufungwa bafuni fimbo za taulo zinaweza kufungwa
pia jikoni kwa ajili ya kuwekea taulo za mkononi.
Muonekano wa fimbo za taulo ni kawaida sana. Ni
fimbo iliyosimikwa ukutani ama nyuma ya mlango kwa kutumia mashine ya kutobolea
ukuta na taulo huwekwa hapo, hutolewa kutumika na hurudishwa tena hapo baada ya
kutumika kwa ajili ya kukauka. Ni muhimu fimbo hizi zimewekwa imara kwakuwa kama
tujuavyo taulo zikiwa mbichi zinakuwa nzito na pia mara nyingine fimbo hizi hutumika
na watoto kwa utundu wao wa kupenda kubembea kila wapoona panafaa, na pia wazee
kujishikilia wakiwa bafuni. Kwahivyo siwezi kuacha kusisitiza kuwa fimbo za taulo
ni lazima zifungwe kwenye ukuta wa tofali ama mlango wa mbao kwa ajili ya uimara.
Fimbo za taulo sizo tu zinazoweza kuhifadhi taulo kwa
usafi na kuruhusu zile zenye unyevu kukauka. Kulabu (hook) za taulo, susu
(rack) za kusimama wima, bangili na ngazi za taulo nazo ni njia nyingine za kuhifadhi
taulo za bafuni. Bangili iliyotobolewa ukutani ambapo taulo kadhaa zinatundikwa
ni maarufu sana siku hizi na kwenye maduka ya fenicha wanaziita bangili za taulo.
Ngazi za taulo ni chuma kingine kinachoonekana kama ngazi
ndogo ambacho hutumika kuwekea taulo, ni
njia mojawapo ya kuhifadhi taulo za bafuni. Je una nafasi kwenye ukuta wa chumba
cha kulala cha wageni wako ambapo unaweza kuweka ngazi hii? Ni kiasi cha
kuishikilia na braketi juu ili isianguke na unaweza kuhifadhi kwa kutandaza taulo
za kuogea. Uzuri wa ngazi ya taulo ukilinganisha na fimbo ni kuwa wakati kwenye
fimbo unaweza kuweka taulo zisizozidi 2 kwenye ngazi ya taulo unaweza kuweka hadi
taulo 6.
Lakini kuna njia nyingine ambazo hazitakufanya uusumbue
ukuta wako ambazo zinaonekana za kimapambo zaidi kwa mfano kuweka susu ya kusimama
inayojitegemea kama ile ya kutundika makoti ofsini. Kama chumba cha kulala cha
wageni wako kina nafasi kidogo ya ziada basi simamisha susu ya koti kwa ajili ya
kutundikia taulo za bafuni. Susu inaweza kutundikwa taulo kadhaa kwa wakati mmoja.
Fikiria kuiweka sehemu ambayo inaingiza hewa au vinginevyo wageni wako wawe wanazigeuza
mara kadhaa kuwezesha kukauka. Kama susu hii inatundika taulo za wageni tofauti
tofauti basi wawe na taulo za rangi tofauti kwa kila mmoja. Hakuna anayependa kushirikiana
taulo.
Badala ya ile susu ya kusimama kuna hii nyingine inayofanana
na ya kuhifadhia chupa za mvinyo. Kama unataka wageni wako wajisikie kama wako
kwenye hoteli yenye hadhi ya nyota tano nenda kistaili zaidi kwa kuhifadhi taulo
zao safi zilizobiringishwa vizuri kwenye susu ya taulo. Susu za taulo zina muonekano
wa kuvutia kwahivyo kwa upande mwingine ni kama pambo. Taulo safi zinabakia zimebiringishwa
vizuri ndani ya susu hadi wakati wa kutumiwa, na hii inachukua nafasi kidogo kuliko
ile ya kusimama. Kuhifadhi taulo kwa kutumia susu ya taulo inakubidi uwe ni mtu
wa kutumia taulo mara moja tu na kulifua.
Kama ulijisikia kwamba bafu lako ni dogo kiasi kwamba
huna mahali pa kuhifadhi taulo za wageni wako msimu huu wa sikukuu hatimaye leo
umefahamu njia kadhaa za kuweza kuhifadhi na kutunza taulo wakati huo huo ukiwa
unazitumia. Wekeza katika njia mojawapo kati ya hizi ilikurahisisha maisha bafuni
sikuzote na hata msimu wa wageni.
No comments:
Post a Comment