Tuesday, September 22, 2015

Jinsi ya kuepuka mende ndani

Hakuna anayeweza kusimama na kusema anajisikia raha kuwa na mende ndani ya nyumba yake. Endapo mende wataingia ndani wanaweza kuharibu vyakula, vitabu, kusambaza magonjwa na hata kusababisha ukakasi machoni pale anapokuwa anakatiza.
Mara wanapofanya makao ndani ya nyumba, inaweza kuwa ngumu sana kuwaondoa. Zifuatazo ni dondoo za kuwaondoa mapema pale tu unapogundua wameingia kwenye nyumba yako.

Hakikisha hawapati maji na chakula. Kuacha maji na vyakula visivyofunikwa kutafanya mende walioingia ndani kwa bahati mbaya  kuneemeka na kuendelea kuzaliana ndani ya nyumba yako.

Ili mende waweze kukaa mahali lazima wawe na chanzo cha majimaji hata kama hamna chakula kwa wingi. 

Endapo chanzo chao cha maji kitakatwa basi wanahamia kwenye vyakula vya majimaji. Na ili wasiweze kupata hivi vyakula hakikisha unafuta meza vizuri baada ya mlo. Safisha mabaki ya vyakula sakafuni. Na ukuta usiachwe na majimaji, kumbuka wanapenda maji.

Hakikisha vyombo vya kuhifadhia vyakula vina mifuniko na vinafunikwa vinapokuwa na vyakula.
Mende wanapenda zaidi kutafuta vyakula usiku kwahivyo usiache mabaki ya chakula au matunda yaliyokatwatwa yabaki bila kuhifadhiwa, ukaenda kulala.

Mwaga taka mara kwa mara , usiziache zikae sana na ndoo ya taka iwe na mfuniko na pale umwagapo ioshwe na kusafishwa vizuri.
Tumia dawa za kuua mende za kuweka kwenye chakula. Dawa hizi unaweza kuzichanganya na chakula halafu ukaiweka zile sehemu ambazo watoto wadogo hawawezi kufikia na pia yale maeneo ya gizani katikati ya mbao na milango ya kabati ambapo mende hupenda kujificha. Na kwa kawaida itaua hata wadudu wengine wadogowadogo. Ukishafanikiwa kuua kizazi hicho cha mende usidhanie kuwa wameisha kwakuwa mayai yaliyobaki nayo yataanguliwa kwahivyo baada ya muda mfupi weka dawa tena kuua wale wadogowadogo walioanguliwa na ndiposa unazingatia usafi ili wasifanye makao. Wakati huohuo ukizingatia umuhimu wa kufunga mlango kwani mende huwa wanatokea nje ndipo wanaingia ndani.

Tumia dawa za kuua mende za kupuliza. Jipatie dawa za kuua mende ambazo zina maelezo kabisa kuwa ni kwa ajili ya kazi hiyo. Hii ni njia rahisi ya kuua wale mende wawili watatu wakubwa wanaoonekana wakizunguka kutafuta chakula, wamejificha au wakitokea nje kuingia ndani. Dawa hizi za kupuliza ni kwa ajili ya kuua mende mara moja hapohapo wakati unapomuona.

Endapo hutaweza kumaliza mende kwa njia hizo zote, basi unaweza kuhitaji kupata ,wataalam wa kuua wadudu. Wataalam hawa wana vifaa na madawa ambayo hupulizia maeneo ya nje na ndani ya nyumba yaani fumigation. Hii inahitajika pale mende ni wengi kiasi kwamba njia zingine haziwezi kuleta matokeo ya kudumu na kwa haraka.

No comments:

Post a Comment