Vyombo vya kupikia visivyong’ang’aniana na chakula ni
pamoja na masufuria na vikaangio. Vyombo hivi vina tabaka nyembamba ndani mwake
linalofanya chombo husika kising’ang’aniane na chakula. Kwa kawaida kusafisha
vyombo visivyong’ang’ania na chakula ni rahisi zaidi. Kiasi kidogo tu cha sabuni,
sponji na maji ndivyo unahitaji. Na baada
ya hapo ni kuvifuta vizuri kabisa hasa kama maji unayotumia yana chembechembe za
chumvi.
Zifuatazo ni dondoo za utunzaji wa vyombo vya aina hii.
Endapo wakati wa kuosha kutakuwa na kaugumu ka chakula
kutoka basi loweka chombo chako kwa muda na pia unaweza kutumia maji ya
uvuguvugu.
Mara nyingi kile kinachoonekana kama ni madoa kwenye
vyombo hivi huwa ni utando wa mafuta
uliojijenga. Tumia sabuni ya kutosha sponji na maji ya moto utamaliza kila
kitu. Hii itasaidia kuondoa uchafu wote hadi ule ulio kwenye miisho na mikunjo
ya vyombo hivi na hata harufu mbaya.
Usikate chakula ulichopika kikiwa bado kwenye vyombo hivi kwa kutumia kisu au kitu
cha chuma . Na vilevile wakati wa kupika
usitumie kijiko chochote kinachoweza kukwaruza. Yote haya ni kwa ajili ya
kuendelea kutunza lile tabaka jembamba la ndani ya chombo husika.
La mwisho ni kuzingatia namna unavyohifadhi vyombo hivi.
Watengenezaji wengi wanashauri kuhifadhi vyombo vya kupikia
visivyong’ang’aniana na chakula kwa kuvitundika ili kuvizuia visikwazurane. Ila
kama huna vitundikio basi inashauriwa kuhifadhi kabatini kwa kufunika bila
kutumbukiza kimoja ndani ya kingine lengo likiwa ni lilelile la kuzuia kitabaka
cha kuzuia vyakula kungangania kisikwaruzwe au kisiharibiwe na vyombo vingine
vya chuma.
Vyombo vya kupikia visivyong’ang’aniana na chakula vinatakiwa kubadilishwa pale tabaka
la ndani litakapoharibika. Wakati huu ni pale unapogundua chakula kuanza kung’ang’ania
kwenye maeneo fulani ya chombo na ukiangalia kwa makini utaona alama hizo.
Chombo kitaendelea kumomonyoka kwahivyo kukibadilisha ndio uamuzi muhimu. Iwe
umewekeza kwenye vyomba vya kupikia visivyong’ang’ania chakula vya bei kubwa au
ndogo unaweza kuongeza uhai wa chombo chako kwa utunzaji wakati wa kuosha
kupikia na kuhifadhi.
Kwa maswali au maoni tembelea
www.vivimachange.blogpot.com
No comments:
Post a Comment