Mke wa Edward Lowassa ambaye ni mgombea urais wa Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Regina Lowassa, amesema ana uhakika
mumewe atashinda katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 25, mwaka huu kutokana na muitikio
mkubwa anaoupata katika mikutano yake na pia kiu ya wazi ya wananchi katika
kufanya mabadiliko.
Kadhalika, ametaja vipaumbele vinne
alivyojiwekea katika
kumshauri mumewe ili mwishowe aliongoze taifa kwa mafanikio makubwa katika
kipindi chake cha kuwa madarakani.
Mbali na Chadema, Lowassa anawakilisha pia muungano wa
vyama vinne vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya NLD,
NCCR-Mageuzi na Chama cha Wananchi (CUF).
Mama Lowassa alielezea mambo hayo jijni Dar es Salaam
jana katika mkutano wake na wanawake walio katika Baraza la Wanawake wa
Chadema( Bawacha), Wilaya ya Kinondoni.
Akizungumza katika mkutano huo kuitikia shangwe
zilizokuwa zikimtaja Lowassa kama rais ajaye, Mama Lowassa alisema amejawa na
imani kuwa mumewe atashinda kwa sababu ameshuhudia mwenyewe muitikio wa
wananchi katika mikoa mbalimbali waliyopita katika harakati za kampeni
zinazoendelea nchini kote.
“Awali, nilikuwa ninafahamu kwamba Watanzania wengi wana
matatizo. Lakini baada ya kutembea zaidi katika kila pembe ya nchi, sasa nikiri
kugundua kwamba nilichokuwa nakifahamu juu ya matatizo ya Watanzania kilikuwa
kidogo sana kulinganisha na ukweli uliopo... sasa nimejionea, ni matatizo
makubwa na ndiyo maana wana kila sababu ya kuamua kufanya mabadiliko,” alisema
Mama Lowassa.
ATAKAVYOKUWA 'FIRST-LADY'
Akieleza zaidi, Mama Lowassa ambaye atakuwa 'first lady'
kama mumewe atashinda na kuwa rais baada ya Oktoba 25, mwaka huu, alisema
atajielekeza katika kushauri na kupigania vipaumbele vinne kwa ajili ya
wanawake nchini. Alivitaja vipaumbele vyake hivyo pindi atakapokuwa mke wa rais
kuwa ni katiba, elimu, afya na uchumi.
Akifafanua, Mama Lowassa alisema ataendeleza mapambano
kuhakikisha kuwa ukombozi wa mwanamke unapatikana kwa dhati kupitia Katiba ya
nchi, ambayo serikali itakayoundwa na Ukawa imeeleza wazi kuwa itaisimamia ili
iandikwe upya kwa maslahi ya Watanzania.
Alisema yeye kama Mke wa Rais mtarajiwa, atahakikisha
elimu kwa wanawake inapewa kipaumbele na kuingizwa kwenye katiba kwani huo
ndiyo ufunguo wa ukombozi wa kweli.
Akielezea kuhusu afya, alisema ni dhamira yake pia kuona
eneo hilo linaboreshwa kwani waathirika wakubwa wa huduma duni ya hospitali ni
pamoja na wanawake. Alizungumzia pia umuhimu wa kuwainua wanawake kiuchumi ili
hatimaye waondokane na umaskini.
Alisema hapendi kuona wanawake wanakuwa tegemezi na
kwamba atahakikisha mara zote anamshauri Rais ili kuhakikisha wanawake nao
wanajitegemea kiuchumi kwa kuhakikisha wanapata fursa za kujipatia mikopo,
elimu bora na afya bora tofauti na ilivyo sasa.
Aliwataka wanawake wajitokeze kwa wingi Oktoba 25 na
kumpigia Lowassa kura nyingi za ndiyo ili aingie madarakani na kuleta
mabadiliko kwa manufaa ya taifa.
Alisema mabadiliko na kuijenga Tanzania mpya
yanawezekana, wala si kwa kutumia gharama kubwa na nguvu kubwa isipokuwa kwa
kuweka mikakati mizuri, thabiti na kuitekeleza kwa vitendo.
“Ninaomba wanawake mniamini katika hili...kwa sasa siwezi
kusema mengi, ila ninanawahakikishia kuwa baada ya Lowassa kuchaguliwa,
nitarudi kwenu na tutapanga kwa pamoja mikakati zaidi ya kuishauri serikali ya
Ukawa katika kutimiza dhamira ya kuwakomboa wanawake na Watanzania wote,”
alisema.
Naibu Katibu Mkuu wa Bawacha, Kunti Yusuph, alisema
katika vipindi vyote vya uchaguzi, wanawake wamekuwa wakirubuniwa na chama
tawala kwa vizawadi vidogo kama khanga na kisha kutelekezwa baada ya uchaguzi,
lakini sasa hawapaswi kukubali hali hiyo bali washiriki kwa dhati ya kuleta
mabadiliko ya kweli kupitia Ukawa.
NIPASHE
No comments:
Post a Comment