Wednesday, April 20, 2016

Jinsi ya kuchagua rangi ya kuta na vitu vya nyumba

 
Muonekano wa nyumba kwa sehemu kubwa unachukuliwa na rangi na ndipo naweza kujiamini kwa kusema nyumba ni rangi. Karim Msheki  ambaye ni mtaalam wa kuchanganya rangi anatueleza maana na namna ya kuchagua rangi tunapotaka kupendezesha nyumba zetu.

Anasema,
kuna mafungu makuu mawili ya rangi ambayo ni rangi za msingi na zile za sekondari. Kila fungu lina rangi 3 ambapo za msingi ni njano, nyekundu na bluu. Na za sekondari ni kijani, chungwa na zambarau. Hizi za sekondari ni mchanganyiko wa hizi 3 za msingi.

Rangi ni somo la kina kimtizamo wa sayansi, hisia, muonekano na dini, ila huhitaji kuwa daktari wa filosofia ya rangi bali kuelewa yale mambo machache ya muhimu kwako.

Kwanza kabisa, rangi zina chanzo chake ambacho ni mwanga wa jua. Kwahivyo rangi ni jinsi unavyoimulika! Ndio maana pasipo mwanga huoni rangi yoyote.

Rangi inaweza kuelezewa katika nyanja 3 ambazo ni jina la rangi, kivuli cha rangi na akisi ya rangi.
Njano inaonekeana kama jua, na inaelezea ubora ambao jua linautoa. Njano chumbani inaleta maana hiyohiyo kama ya jua.

Nyekundu inazungumzia moto na damu. Inaambatana na uchangamfu, nia na kukomalia jambo. Ni vyema kujua kuwa kwa tabia hizi chumba kilichopakwa rangi nyekundu kinaleta kisia ya kuwa ni kidogo kimuonekano.

Bluu ni kinyume cha nyekundu. Inaelezea hisia za utulivu na umbali. Umbali unasababisha chumba kionekane kikubwa.

Kijani ni muunganiko wa njano na bluu na hivyo ina tabia ya rangi zote mbili. Hakuna sehemu inayoweza kuwa tulivu na ya kustarehe kama  kukaa kwenye viti vilivyowekwa juu ya ukoka wa kijani kibichi chini ya kivuli cha kijani cha miti katikati ya siku ya joto kali.

Kivuli ni Nyanja nyingine ya kuelezea rangi. Ni ile hali ya wepesi au uzito wa rangi kutoka kwenye jamii ya rangi hiyo. Kwa mfano kijivu nyepesi inakaribia nyeupe wakati ile nzito ikikaribia kabisa nyeusi, pinki ni kivuli cha jamii ya nyekundu na vivyo hivyo kwa damu ya mzee.

Cha maana zaidi ni kufahamu hili swala la kuchagua rangi kwa ajili ya kuta na pia vitu vilivyomo ndani ya nyumba. Kanuni hizi mbili zitakujibia jambo hili:

1.      Kwa lengo ya kupendezesha ni kwamba background zinatakiwa kuwa na rangi nyepesi kuliko vitu. Huenda unajiuliza maana yake ni nini, ni kwamba kuta, dari na sakafu zinatakiwa ziwe na rangi nyepesi wakati fenicha na sanaa za ukutani zikiwa na rangi nzito.

2.      Kitu (hapa si yale maeneo makubwa ya background)  kinapokuwa kikubwa ndivyo kinavyotakiwa kiwe kwenye kivuli cha upande ule wa rangi ambao ni nyepesi na kinyume chake ni kwamba kinapokuwa kidogo uzito wa rangi unatakiwa uongezeke. Hii ni katika kusadia hivyo vitu vidogo navyo vichomoze vionekane. Kutokana na kanuni hii ni kwamba vile vitu vikubwa kama zulia kwa mfano vinapaswa kuwa vya rangi nyepesi kuliko vile vidogodogo kama mito ya kwenye makochi na vivuli vya taa za mezani.

Kwa elimu hii ndogo ya rangi ni imani kuwa utachagua rangi ya kuta na vitu kwa uelewa.


Simu 0755 200023

No comments:

Post a Comment