Tuesday, April 19, 2016

Maeneo 7 unayotakiwa kuondoa mrundikano angalau mara moja kwa juma


 Kuna maeneo nyumbani ambayo ni kama sumaku inayovuta vitu vinaavyoingia nyumbani. Maeneo haya yanakuwa na mrundikano hata ujitahidi kiasi gani kuyafanya yawe nadhifu. Ila kwakuwa huwezi kuweka kila inchi ya nyumba yako nadhifu kila sekunde, unaweza kuweka maeneo haya huru na
mrundikano kwa kuyatupia jicho angalau mara moja kila juma.

1.      Kwenye jokofu
Kusafisha jokofu na kulipanga upya kuondoa vyakula vilivyopitwa na muda au kama ni mbogamboga zilizoharibika na kunyauka inaweza kuwa ni kazi kubwa. Si mbaya kama ukiwa unatupia jicho kwenye jokofu lako walau mara moja kwa juma ili kuweka mambo sawa.

2.      Kabati la nguo
Mara moja kwa juma hakikisha unaingia kwenye kabati lako la nguo, kunja, tundika na ondoa nguo ambazo zinazagaazagaa. Pia weka pembeni chochote ambacho unadhani hukihitaji tena. Hivi unaweza kuvikusanya kwa muda hadi vikiwa vingi ugawe. Hii inakusaidia kwa ajili kwa juma nzima unajua ni nguo au viatu vipi vinavyokufaa au visivyokufaa tena.
Kwa wengi wakati wa kutizama kwenye kabati la nguo wanautumia pia kutembea chumbani kwa ujumla na kukiweka sawa. Huenda kuna glasi uliyotumia hapo chumbani juma hilo  ukasahau kuirudisha mahali pake, ndio muda sahihi wa kufanya hivyo.

3.      Meza ya vipodozi
Kama unatumia kipodozi cha aina moja kila siku, kuna uwezekano kuwa kuna vingine vingi ambavyo huvitumii juma hilo. Hakikisha meza yako inabeba vipodozi unavyotumia tu na kuondoa vile vyote vilivyoisha na pia usivyotumia. Vitu vingine vya kuangalia kwenye meza hii ni pamoja na vibanio vya nywele, hereni, bangili na mikufu na hata wakati mwingine dawa zilizopitwa na muda wake au ulishapona kitambo.
Vilevile wakati wa kupaka vipodozi vipo ambavyo vinamwagika juu ya meza. Wakati huu nao ni mufaka kwa kusafisha eneo hilo ili kuifanya meza isionekane shaghala baghala.

4.      Stoo
Wengi tunafanya makosa ya kufikiria kuwa stoo inatakiwa kurundikana. Stoo  yoyote iwe ni ya vyakula au vifaa vya usafi na utunzaji wa nyumba inapaswa kuwa katika mpangilio. Kufanikisha hili hakikisha kila juma unapitia kwenye stoo zako na kuondoa mrundikano wowote uliojitengeneza kwa kipindi hicho. Na faida utakayopata ni kwamba utapunguza kazi kubwa ya baadaye na pia utaepuka uharibifu unaoweza kujitokeza. Kwa mfano kama stoo ni ya vyakula kama viazi na vitunguu tunajua vyema kwamba vikiwepo vilivyoharibika bila kuondolewa vinaharibu na vya jirani yake, na vilevile vinazalisha mende na wadudu ambao wanaendelea kuharibu.

5.      Meza ya kahawa
Meza ya kahawa imekuwa ikionewa kwa kurundikwa vitu kama majarida na magazeti ambayo yamekuwa yakiwekwa ya leo na kesho yake na kesho kutwa yake. Hali hii inasababisha mrundikano na kumpa mwenye nyumba au mgeni usumbufu pale anapotaka kuweka kinywaji chake mezani. Ifanye meza ya kahawa kuepukana na mrundikano kwa kuitembelea angalao mara moja kila wiki.

6.      Droo za jikoni
Ni ukweli kwamba mara nyingi droo zza jikoni zinachanganyikana vyombo. Eneo lililotakiwa kuwa na vijiko si ajabu ukakuta kuna kisu kimejichanganya humo. Vilevile droo la vikontena laweza kuwa limechanganywa sufuria  kwa mfano. Pitia droo za jikoni mara moja kila juma kuhakikisha kuwa kila chombo kiko mahali pake.

7.      Fikra
Unaweza ukashangaa eneo hili ila ni muhimu kuondoa mrundikano kwenye akili yako pia kadri unavyofanya kwenye nyumba yako. Ndani ya juma tafakari ni mawazo yapi yanafanya fikra zako zirundikane na yaondoe kwa kuongeza mengine mapya japo kwa kusoma kitabu! Fikra za mwenyenyumba zisiporundikana zinamwezesha kuweka nyumba katika mpangilio.


Vivi anakuwezesha kupendezesha nyumba yako. Simu 0755 200023

No comments:

Post a Comment