Monday, April 25, 2016

Je, velveti ni kitambaa kizuri kwa sofa?

Ingawa kuchagua kitambaa cha sofa ni changamoto, kuchagua malighafi iliyotengenezea kitambaa sahihi kwa sofa inaweza kuwa changamoto zaidi. Ni vyema kufahamu kuwa malighafi kuu sokoni kwa ajili ya vitambaa vya sofa ni pamba, hariri na velveti. Vitambaa vyovyote
kama sio vya malighafi hizi tatu basi ni mchanganyiko wa malighafi hizi hizi.

Velveti ni moja kati ya malighafi inayoongoza kupendwa kwa ajili ya sofa. Kuna kitu cha kipekee kuhusu hiki kitambaa, ni kilaini na hakina hisia ya ubaridi kitu ambacho kinafanya sofa liwe na mvuto machoni na tamanio la kulikalia ili kupumzika.

Wana historia wanasema velveti ni ya zamani sana, ila kwa bahati nzuri haipitwi na wakati. Kwa wewe unayechagua kitambaa cha sofa bila shaka velveti inaweza kuwa ndiyo unahitaji. Kuna faida unazopaswa kufahamu za kwanini ya kuchagua velveti kama malighafi ya kitambaa kwa ajili ya sofa zako.

Faida ya kwanza ni kuwa velveti ina muonekano wa kifahari na pia ni laini sana. Tembeza mkono wako juu ya hiki kitambaa na utakubaliana na ninachosema.

Ingawaje velveti inaonekana kujaa, bado ni kitambaa chepesi sana jambo ambalo linakupa urahisi wa kuondoa uchafu pale unapotaka kusafisha sofa. Na pia ina manyoya yanayobadilika ung’avu kadri unavyoigusa hali inayofanya uchafu na madoa madogodogo yasionekane.

Velveti inashika na kujaa rangi vizuri sana. Siku zote sofa inapoonekana imejaa inapendeza kuliko sofa nyembamba. Endapo utachagua velveti ya rangi moja au yenye michoro utagundua kuwa rangi zake zinaonekana sana. Hii ni muhimu sana kwa kupendezesha ndani kwani unataka rangi ya sofa zako itoe ushirikiano na mapambo mengine yaliyopo sebuleni.

Sasa kwa kujua faida hizo, unatakiwa pia ujue changamoto kabla hujaamua kuchagua kitambaa cha malighafi hii na kukitumia kwenye sofa zako unazotaka kutengeneza au hata kununua ambazo tayari zimetengenezwa kwa velveti. Ni bahati mbaya kuwa kitambaa cha malighafi hii kina gharama kubwa kuliko malighafi nyingine. Pia kutokana na hali yake ya manyoya endapo sofa hazitawekwa kwenye hali ya usafi, kuna uwezekano wa kubeba vumbi na kusababishia watu hasa watoto mafua.

Kama ilivyo kwa pamba na hariri ni vyema kufahamu kuwa sio kila velveti ni velveti kwa asilimia mia moja. Huwa zipo zinazochanganywa na malighafi nyingine. Hakikisha unanunua iliyo sahihi kwako.

Changamoto ya mwisho ya velveti ni kwamba, endapo utachagua ile ya bei rahisi sana kuna uwezekano wa kuwa inatoa nyuzi ndogondogo mfano wa manyoya na kuwa kero kwa aliyekalia sofa kwa kuharibu muonekano wa nguo yake.


Vivi anakuwezesha kupendezesha nyumba yako. Simu 0755 200023

No comments:

Post a Comment