Monday, April 4, 2016

Kanuni kuu mbili za kuwezesha chumba kidogo kionekane kikubwa

Linapokuja swala la kufanya chumba kidogo ndani ya nyumba kionekane kikubwa au hata ndani ya nyumba ndogo kuonekane ni kukubwa na kumfanya aliyemo kupata hisia ya nafasi zaidi, kuna kanuni kuu mbili muhimu unazotakiwa kuwa nazo kichwani. Kanuni hizo ni kwanza kuruhusu
mwanga kwa kadri iwezekavyo na pili ni kutumia vihifadhio vya aina mbalimbali. 

Makala hii itakujuza namna unavyoweza kutumi kanuni hizi mbili kutengeneza chumba chenye nafasi na mpangilio.

Kanuni ya kwanza na muhimu ni mwanga. Mwanga unavyokuwa mwingi chumbani, ndivyo unavyopata hisia za kuwa na nafasi kubwa  na wepesi uwapo chumbani. Vilevile chumba kinapokuwa cha mwanga hafifu, ndivyo kinavyozidi kuonekana kidogo na unahisi kuelemewa fulani uwapo ndani.

Sasa basi, kwakuwa unataka chumba chako kiwe na mwanga kadri iwezekanavyo, ni vyema kutumia rangi nyepesi ukutani na mandhari nzima ya chumba kwa ujumla. Rangi sahihi kwa dari na kuta ni nyeupe na krimu. Ni vyema kufahamu kuwa pamoja na maeneo haya kuwa meupe bado unatakiwa kuwa na fenicha za rangi nyepesi kwenye chumba kizima ili kupata mwanga unaoutaka na utakaowezesha kufanya chumba kionekane kikubwa.

Madirisha makubwa ni njia nzuri ya kuruhusu mwanga wa jua kuingia ndani kwa wingi. Ni njia rafiki kwa mazingira na pia gharama nafuu kwani huhitaji kuwasha nishati kwa ajili ya mwanga mchana.

Endapo huna madirisha ya kutosha au yaliyopo ni madogo sana, ndipo inakulazimu kuutafuta mwanga kwa njia nyingine kama vile kutumia balbu na vioo. Vioo vikubwa vilivyowekwa kutazamana na dirisha vinasaidia kuakisi mwanga kutoka nje na kuurudisha ndani. Vilevile milango yenye panel za vioo inafanya vyema zaidi kuingiza mwanga ukilinganisha na ile iliyozibwa kotekote. Pia maeneo yanayong’aa iwe ni makabati au sakafu yanasaidia kuongeza mwanga ndani na hivyo kufanya chumba kionekane kikubwa.

Kanuni ya pili ya kufanya chumba kidogo kionekane kikubwa ni kuwa na vihifadhio vingi aina mbalimbali kadri iwezekanavyo. Kwa mfano, mashelfu ya ukutani ni njia nzuri sana ya kuweka mpangilio katika chumba chochote Yanaweza kuwa ni mashelfu ya wazi kama ya vitabu au ni yaliyo ndani ya makabati. Uzuri wa shelfu za ukutani ni kwamba unaweza kuziweka kwenye ukuta wa juu ambao usingetumika kwa kazi nyingine.

Mashelfu unaweza kuyatumia kuhifadhi chochote kutokana na chumba yalipo. Yatumie kuhifadhi vibakuli, sahani, viatu, nguo za kukunja, vitabu, michezo na midoli ya watoto na vitu vingine vingi.


Vivi  anakuwezesha kupendezesha nyumba yako. Endapo unahitaji ushauri wowote uwe ni kununua fenicha au kuchagua rangi au chochote kuhusu kupendezesha nyumba yako tafadhali tuwasiliane....Simu 0755 200023

No comments:

Post a Comment