Friday, January 31, 2014
Tuesday, January 28, 2014
Friday, January 24, 2014
my article for newspaper: rangi za mazulia
Kupamba nyumba yako
ni zaidi ya kuchagua rangi za kuta na aina ya fenicha — unatakiwa pia
uchague rangi sahihi ya zulia.
Kuchagua rangi sahihi
za mazulia kwa ajili ya nyumba yako sio uamuzi mdogo, mazulia ambayo utakaa
nayo kwa miaka. Kwa ajili kuweka mazulia ni moja ya mapambo ya ndani
yanayogharimu zaidi kimuda na kipesa. Kwa mfano si busara kutandika zulia la
ukuta kwa ukuta ambalo unategemea kuondoa chini ya miaka mitatu. Kwanza si kazi
ya kitoto kuanza kutoa vitu ndani kwa ajili ya kutanzika zulia la aina hii, na
pili huwa zulia hili ni kubwa kwa hivyo pia ni gharama. Nimefanya mahojiana na
Bi Aisha Idd ambaye anauza mazulia ya nyumbani kutaka kujua mambo ya kuzingatia
kwa upande wa rangi wakati wa kununua mazulia ya nyumbani.
Bi Aisha anasema
michoro na rangi za mazulia zinabadilika kila wakati kwa hivyo kwa ajili
mazulia ni gharama, unatakiwa kuchagua yale ya rangi ambazo zitaoana na
muonekano wa sasa ama mipango ya baadaye kama ipo juu ya nyumba yako. “Kwa
kawaida rangi za mapambo ya sakafu huwa zinakuwa nyuma mwaka 1-2 kulinganisha
na zile rangi za mitindo ya nguo, anasema Bi Aisha” Hii ina maana kwamba rangi
maarufu zaidi kwenye maduka ya nguo za wanawake, zitaanza kuonekana kwenye sakafu
za nyumba miaka kadhaa mbele. Upo hapo!
Kwa mazulia ya
nyumbani ambazo zinaonekana zimepitwa na wakati kwa sasa ni rangi za dhahabu,
kijani, silva, damu ya mzee na rangi ya udongo. Rangi zisizokolea au kwa maneno
mengine rangi za mwanga kama vile bluu, khaki, kijivu na rangi ya maziwa
zinaonekana kuwa maarufu zaidi kwa sasa. Hata hivyo hakuna rangi ambayo
inashika kasi kwa sasa kama kijivu na khaki na wala haijalishi mabadiliko ya
mara kwa mara ya rangi hizi. Aisha anasema labda ni kutokana na kuwa kuna jinsi
nyingi ya kuoanisha rangi hizi mbili na vizulia vya kutupia.
Sasa basi wakati wa
kuchagua mazulia kwa ajili ya sakafu za nyumba yako zingatia mambo kadha wa
kadha. Bahati nzuri ni kuwa vizulia vile vya kutupia baadhi ya maeneo vinakuja
kwa bei, michoro na rangi lukuki ambapo ushindwe wewe tu. Kwa kweli sio ngumu
kupata ukubwa na rangi unazotaka kwa uwezo ulio nao. Siku zote kumbuka kuwa
uchaguzi wako wa mazulia ya nyubani kwa kila chumba ni msingi wa ladha yako.
Baadhi
ya dondoo zifuatatzo zitakusaidia kuchagua rangi sahihi ya mazulia ya kwenye vyumba
vya nyumba yako. Kwa kuwa zulia huwa ni la kudumu na kuweka la rangi fulani ni uamuzi wa gharama kufanya, hapa ni dondoo
chache za kukusaidia katika uamuzi huo mgumu.
Kwanza kabisa fahamu kuwa zulia ni moyo wa
nyumba yako. Linatoa utambulisho wako hasa lile la sebuleni. Kwa vile mnachukua
muda mwingi sebuleni kama familia, fikiria rangi ambayo inaenda kukubaliana na
mfumo wa maisha yenu. Je sebule yako ni rasmi au ni ya kujimwaya mwaya?
Kuamua ni mazulia ya rangi ipi ununue, fahamu ni kwa kiasi gani yatakanyagwa.
Zulia linavyozidi kukanyagwa ndivyo kuna uwezekano wa kuchafuka kwa maana ya
kumwagikiwa vimiminika vilivyobebwa na wapitaji, madoa na majasho ya miguu. Mazulia
ya rangi za mwanga kwa mfano khaki na kijivu huonyesha uchafu kirahisi lakini
yanaweza kusafishika kwa dawa za kuondoa madoa kwenye mazulia ila kama mazulia
yenyewe sio imara basi yataanza kuonyesha alama za uchakavu kwenye maeneo hayo
ukiliinganisha na mazulia ya rangi za giza. Kama una wanyama wa ndani au sakafu
ya nje ya nyumba isiyo ngumu ni rahisi mazulia yako kuchafuka kuliko yule
anayeishi kwenye nyumba yenye mazingira ya nje yaliyowekwa sakafu ngumu.
Familia nyingi haziweki zulia jikoni.
Fikiria matumizi ya eneo ambapo zulia litawekwa kabla ya kuamua rangi. Je
unataka zulia lilete mwanga ama lipunguze mwanga chumba ambacho kina mwanga
mkali zaidi? Nyekundu ni sahihi kwa vyumbani, sebuleni na kwenye ujia kwani haionyeshi
madoa kwa hasira kama rangi za mwanga. Ila kwa vyumba ambavyo vina kiasi
kikubwa cha mwanga wa jua fikiria juu ya zulia kuchuja, tatizo ambalo
linaonyesha sana kwenye zulia za rangi za giza.
Kuchagua rangi kunahusika sana na vitu
mbalimbali anbavyo vinahusika kwenye zulia hilo. Chagua rangi za giza kama kuna
watoto wadogo ili kuficha yale madoa yasiyoepukika. Kama una wanyama wa ndani
fikiria vitu kama tope wanaloweza kuingiza. Hata kama huhusiki na hivyo vyote
basi fikiria hata sherehe na wale wageni ambao kwa vyovyote vile hawatainama
kuvua viatu vyao!
Chagua rangi ya zulia itakayoendana na haiba na mazingira ya nyumbani
kwako. Kwa mfano, kuna familia ambazo kuna sebule rasmi kwa ajili ya wageni tu na
kuna nyingine ya familia. Hii rasmi
huenda kwa kawaida huwa na muonekano wa rangi za kifahari na rangi za mazulia yake
huwa ni moja kwa mfano zulia la sakafu yote ya sebule rasmi yaweza kuwa ya rangi
ya maziwa. Sasa kabla ya kuamua rangi ya zulia jiulize je unapenda kutembea
kwenye chumba ambacho zulia lake lote ni la rangi moja tena ya mwanga?
Rangi za zulia utakazochagua zinahusiana vip na rangi za kuta na mapambo
mengine hapo chumbani? Kila chumba kinahitaji sehemu moja ambayo ni kitovu.
Zulia lako linaweza kuwa ndio kitovu, hautaki zulia lishindane na mapambo yako
mengine kwa ajili chumba kinaweza kuonekana vurugu vurugu.
Shirikisha
wanafamilia na chukua kura! Kwa ajili wote mnaenda kutumia mazulia haya,
inaweza kuwa vyema kujua ni rangi zipi familia yako inaona zitafaa zaidi chumba
fulani. Lete sampo nyumbani mshauriane pamoja. Huenda ukagundua rangi ambayo haukuwa
umeiwaza mwanzo.
Thursday, January 23, 2014
buriani Mhe. Bwa'mdogo; tuta miss biashara uliyokuwa unatupa
jana nilishtushwa kujua kuwa Marehemu Mheshimiwa Saidi Bwanamdogo kumbe ni aliyekuwa mteja wangu wa kufua nguo. toka nianze kufanya DC & Laundry sijawahi kupata biashara kubwa kwa wakati mmoja kama nilivyokuwa napata kwa Mheshimiwa Bwa'mdogo, kiasi kikubwa kabisa cha nguo alichowahi kuniletea ni kanzu 500. kwa mara ya kwanza alipokuja ofsini kwangu kama mteja nilimuuliza jina la kwenye risiti niandike nani? akaniambia Bwa'mdogo, nikadhania kama ananitania kwa ajili hata muonekano wake alioneekana mdogo mdogo nikadhani ndio maana kajiita hivyo; ila baada ya kifo chake jana nilipoona picha du! ndio nikajua kuwa lilikuwa jina lake rasmi. sikuwahi hata kufahamu kuwa alikuwa mbunge tena wa Chalinze. buriani Bwa'mdogo..you will be missed!
Ian DC & Laundry
Tuesday, January 21, 2014
Monday, January 20, 2014
uzazi kweli kazi...
mwanakabumbu wangu akiandaliwa kwa ajili ya mechi ya alhamisi. kaniambia mechi yao inaitwa under 6 eti!
Saturday, January 18, 2014
Friday, January 17, 2014
Thursday, January 16, 2014
My article for newspaper: chumba cha kufulia
Eneo la kufulia liwe
na muonekano na vifaa hivi.
Ni mara ngapi kwa juma ambazo unafua nguo? Familia ya watu wanne
kwa mfano, inaweza kuwa inafua kati ya mara 3-4 kwa juma. Kwa maana hiyo ni
vyema kuwa na chumba ama eneo maalum la kufulia nguo ambalo lina vitu muhimu
vinavyotakikana kuwepo ili kufanikisha kwa haraka na kwa urahisi mchakato mzima
wa kuondoa nguo kutoka kwenye uchafu hadi kuiweka katika hali ya kufaa kuvaliwa
tena.
Asilimia kubwa ya kaya katika nchi zinazoendelea hakuna
mahali au chumba maalum cha kufulia na badala yake hasa maeneo ya mijini mahali
pa kufulia ni juu ya shimo la maji taka! Hii sio sawa kwa mfuaji kwani muda
wote anaokuwa anafua pale anavuta hewa chafu inayotoka shimoni humo hivyo
kuhatarisha afya. Kwa wenzetu walioendelea na baadhi ya familia katika nchi
zinazoendelea, kwenye makazi yao wana chumba au eneo maalum la kufulia
linalokidhi viwango vya vifaa na mahitaji. Si sawa kuwa na eneo tu la nje
karibia na chanzo cha maji kwa ajili ya kufulia kwani kuna vitu muhimu ambavyo
vinafanikisha zoezi la kufua na kwa kweli huwezi kuvihifadhi nje tu kwenye eneo
hilo.
Eneo ama chumba cha kufulia kitafaa zaidi kikiwa kiko maeneo
ya uani. Ili kuwa na eneo sahihi la kufulia ambalo utaokoa muda na nguvu zako
na kukufanya uvutiwe na kazi hiyo fikiria shughuli zitakazofanyika hapo:
kuchambua nguo, kufua, kukausha, kunyoosha, kutundika na kukunja. Weka
mpangilio wa kuwezesha vifaa vyako viendane na mtiririko huo. Wala hutakiwi kuwa
na eneo kuubwa kwa kazi hii, dogo liwavyo, eneo hili litawezesha nguo zitoke
kwenye sinki iwapo unafua kwa mikono au kwenye mashine kwenda kukaushwa/kuanikwa,
na kupelekwa meza ama kaunta ya kunyooshea na kukunjwa ama kutundikwa kuendana
na hitaji la kila nguo.
Nchi yetu imejaaliwa kuwa kwenye ukanda wa jua la kutosha
ambapo hatuna haja ya kuwa na mashine za kukaushia nguo. Rasilimali ya jua tuliyonayo
inatutosha hatuhitaji kukausha kwa mashine za umeme. Kinachotakiwa tu ni kuwa
na kamba za kukaushia karibia na mahali pako hapo pa kufulia.
Ni lazima kuwa na mahali pa kutundikia nguo zinazonyooshwa
ambazo hazitakunjwa. Fimbo za kutundia mahali pa kufulia zinahusu. Fimbo hizi ziwe
mbali kidogo na ukuta ili nguo zilizokwisha nyooshwa zisiuguse. Fimbo hizi ni
za kutundika nguo kwa muda tu wakati wa kunyoosha kabla hasijasambazwa katika
makabati ya nguo husika. Zile nguo zinazokunjwa baada ya kunyooshwa nazo
zinahitajika mahali pa kuhifadhia kwa muda katika chumba cha kufulia kabla
hazijasambazwa kwenye droo zinazohusika. Kwa maana hiyo pamoja na fimbo ya
kutundikia, pia unahitaji kuwa na shelfu. Huu mpangilio ni kwa ajili ya
kurahisisha mchakato wa kuondoa nguo kwenye kutoweza kuvalika kutokana na
uchafu hadi kuiwezesha kuvalika tena; kwa hiyo ni kwa kaya yoyote na wala
usidhanie ni maisha ya watu wa daraja fulani tu.
Gawa sakafu ya eneo
lako la kufulia katika maeneo mawili. Lile la maji maji kwa mfano kwenye sinki
na lile kavu kwa mfano pale pa kunyooshea. Utajikuta hili eneo kavu halipati
maji kabisa na waweza kupamba hata kwa kizulia. Kama una mashine ya kufulia
weka upande sawa na wa sinki ili hata imuwie rahisi fundi bomba endapo kutakuwa
na tatizo lolote kwani bomba zote zitakuwa eneo moja na kufanya zile shughuli
za maji maji kuwa pamoja. Tenga la nguo chafu liwe jirani kwa ajili ya urahisi
wa kubeba na kuweka kwenye mashine au kwenye sinki.
Eneo la kamba za kukaushia lisiwe mbali na panaponyooshewa
ili iwe rahisi kuanua nguo na kupeleka moja kwa moja kwenye kaunta ya
kunyooshea. Ili kutumia eneo dogo mara nyingi baadhi ya wenye nyumba wanapenda
kujenga kaunta ya kunyooshea juu ya mashine ya kufulia. Inakuwa ni busara
kutumia eneo hili la juu ya mashine badala ya kuliacha bure na badala yake kwenda
kuweka kimeza cha kunyooshea kwingine. Na kwa bahati nzuri mashine za kufulia
kwa ajili ya majumbani zina urefu chini kidogo ya meza ya kunyooshea kwa hivyo
hakuna ubaya kujengea hii kaunta ya kunyooshea juu yake. Pia kaunta iliyojengwa
kwa zege kwa ajili ya kunyooshea ni imara na inadumu maisha kulinganisha na
meza.
Kuweka vifaa katika mpangilio kunarahisisha mambo. Kusanya
sabuni na dawa zako zote za kufuli katika shelfu mojawapo ili kila kitu kiwe
kwenye ncha ya vidole vyako pale unapokihitaji. Hakikisha baadhi ya madawa na
blichi zinakuwa eneo la juu ambalo watoto wadogo hawawezi kufikia, kama vipi
weka loki kabisa.
Mahali pako pa kufulia pawe na mwanga wa kutosha. Mwanga
mwingi wa asili ni mzuri zaidi hasa wakati wa kufua kwa mkono na kunyoosha. Mwanga
pia unakuonyesha ndani ya mashine kukuridhisha kuwa hakuna nguo iliyosahaulika.
Sakafu inayofaa
bafuni na jikoni inafaa pia eneo la kufulia. Sakafu ya marumaru ni rahisi kusafisha,
haipitishi maji na ikitokea kumwagika haiharibiwi na blichi.
Kufua haitakiwi kuwa kazi ya kuchukiza. Weka mpangilio huu
mahali pako pa kufulia na kamwe
hutachukia mchakato mzima wa kufua na kunyoosha nguo.
Makala hii imeandaliwa
na Vivi O. Machange. Vivi ni mjasiriamali upande wa usafi wa magari, nguo na
mazulia; pia ana mapenzi makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni
au maswali tuma kwenda 0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk
Tuesday, January 14, 2014
Venus ni mtu kama wewe
wadau hii ni nyumba ya mwanatenis Venus Williams iliyoko sokoni huko
Marekani. hapa nakuonyesha picha chache za vitu basic vinavyotakiwa walau
viwe kwenye makazi ya binadamu. Of course V ni celebrity mkubwa ila na
wewe unaweza kuwa na nyumba similar na hii ingawa ya kwako inaweza kuwa ndogo
ya kawaida. kaza buti tutafika tu!
eneo la mlango wa mbele. nimeyapenda mawe ya kukanyagia
sebuleni hamna mbwembwe na ung'aro ung'aro wa kichina mwingi, sofa zake bomba, kimeza chake cha kahawa murua, TV yake ya ukutani superb na kizulia chenye mashiko
eating area. umeona hiyo taa?
jikoni kuna my favorite kizulia cha jikoni. eeh, unajua unasimama sana kuosha vyombo na shughuli nyingine za kwenye sinki kwa hivyo muhimu miguu kuburudika juu ya zulia.
bedroom na ki bedside carpet chake
sink la bafuni na ki medicine cabinet chake
taulo zimehifadhiwa hygienically
Thursday, January 2, 2014
My article for newspaper: malengo ya mwaka mpya
Ni wakati
mwingine tena wa mwaka ambao wengi wetu wanapenda kufanya mabadiliko kwenye
maisha yao. Je
umeshafikiria mabadiliko ya mwaka mpya kwa ajili ya kiota chako? Japo mabadiliko
haya yanajulikana na wengi zaidi kama
maazimio, kwa kutia msisitizo zaidi makala hii itayaita malengo. Malengo
yanatamkwa kwa kusisitiza wakati uliopo ni nini tamanio lako (kwa mfano kuamua
kubadili mpangilio wa fenicha za sebuleni kwako ili kuwezesha kunogesha zaidi
mazungumzo) wakati maazimio yanatamka ni nini ungependa huko mbeleni ya kuwa
unaenda kufanya nini wakati ujao.
Mara
nyingi malengo (au maazimio) ya mwaka mpya yanatupiliwa mbali hata kama nguvu za kutosha ziliwekwa ili kuhakikisha
yanafanikiwa. Moja ya sababu za malengo kutofanikiwa ni mazingira ya nyumbani
kwako kutosaidia kuwezesha mafanikio ya malengo hayo. Kama
unataka kufanya mabadiliko ndani ya maisha yako bila kuhusisha mazingira yako
kufanikiwa ni mbinde. Kwa maana ya kwamba kama unaweka malengo yako ya mwaka
2014 kwa ajili ya makazi yako na ukayaacha mazingira yalivyo, ni ngumu sana kubadili chochote.
Hata matangazo kwa mfano ya kujikinga na maambukizi ya VVU yanaonyesha uhusiano
kati ya maambukizi na mazingira fulani ambayo yanachochea maambukizi hayo.
Kanuni ya
malengo kuwa na uhusiano na mazingira inahusika karibia katika kila kitu. Kama unataka mwaka huu uwe tofauti basi unatakiwa kuweka
mazingira ya kuwezesha malengo yako.
Je
mazingira yako yanakusaidia kupata kile unachokihitaji? Kwenye mazingira ya
nyumbani kwako vitu ambavyo havijakaa mahali pake au vimekaa mahali ambapo
havifanyi kazi yake au havitumiki tena vinakukwamisha kutimiza malengo yako
hapo nyumbani. Tembelea kwenye makabati ya nguo na vyombo angalia kwa umakini
kuona ni vitu gani vya kuhifadhi, vya kugawa ama vya kutupa. Fanya hivyo kwa
nia ya kupata nafasi ya kile tu kitakachosaidia kufanikisha malengo yako.
Pengine
lengo lako la mwaka mpya ni kutokula hovyo kwa nia ya kupungua uzito. Je mara
zote unaingia nyumbani kwa kupitia mlango wa nyuma ambapo unaingilia moja kwa
moja jikoni? Kumbuka kanuni kuwa unachokiona mwanzo kinagusa zaidi akili yako,
kwa hiyo kama mara ungiapo ndani unakutana na
jokufu, chakula na kadhalika utapata hamu ya kula hapo hapo. Tumia mlango wa mbele
ambapo utaona kitu tofauti mara uingiapo ndani - kitu ambacho hakitakufikirisha
kula.
Mahusiano
mengi yanaweza kuboreshwa kwa mapambo ya nyumbani hasa katika swala la
kuwasiliana. Je chumba cha kulala cha wakuu wa familia ni mahali patakatifu kwa
wawili? Hakikisha vitu kama taa, vimeza, na
viti kwenye chumba hicho viko viwili viwili.
Au lengo
lako mwaka huu ni kuwa na wageni wengi zaidi nyumbani? Hakikisha basi mlango wa
mbele unaonekana na kuna njia ya wazi ya kuingilia. Taa zinazomulika njia ya
kuelekea mlango huo ziwe zinafanya kazi. Pitia mlango wa mbele kama mgeni
mtarajiwa uone kama kila kitu kiko sawa. Je
njia hiyo inakaribisha? Na sebule yako je nayo inavutia kwa ajili ya wageni
wako wengi ambao unapenda kuwaalika nyumbani mwaka huu?
Kwa wale ambao
azimio lao kuu la mwaka 2014 ni kupamba nyumba zao hakikisha unachagua rangi
kwa umakini, fikiria mpangilio wa fenicha je zinawatendea haki watumiaji wa
chumba husika. Angalia vitu ambavyo inabidi uvifanyie kazi ili kuboresha
muonekano wa makazi yako. Kama kwa mfano sakafu ya sebule yako ni ya marumaru
na unachoka kusugua na kusafisha kila siku na unakiri kuwa ni ngumu kuifanya
iwe safi; basi weka zulia kubwa ambapo utasafisha kwa mashine ya upepo mara
mbili au tatu kwa wiki.
Ikiwa
unaazimia kutojaza vyombo vichafu kwenye karo basi mwaka ujao lenga kuosha
chombo mara baada ya kukitumia. Na hata hakikisha wanafamilia wengine pia
wanafanya hivyo.
Huenda
kijani kinakubariki lakini huna eneo kubwa ya kuweza kuwa na bustani za
ardhini. Otesha basi bustani za kwenye vyungu walau ukifungua pazia la chumba
cha kulala kunapopambazuka ukutane na kijani. Azimia kupamba ndani mwako kwa maua freshi japo mara moja
kwa mwezi.
Kweli,
baadhi ya mabadiliko ya nyumbani kwako unaweza kuhitaji kutafuta msaada, lakini
kuna mabadiliko mengi sana
ambayo hayahitaji gharama lakini yanahitaji muda na nguvu ( na pengine
kautaalamu) kwahiyo kwa 2014 kwa nini
usiazimie kupamba mwenyewe? Unaonaje? Ni azimio moja zuri kwa ajili ya makazi
yako ambalo unaweza kutekeleza. Fanya usafi mkubwa ndani ya nyumba yako mara
moja kwa mwezi ( weka tarehe kwenye kalenda yako na isismamie). Mwanamke
unatakiwa upende usafi na usiwe mvivu. Shirikisha na wanafamilia wengine pia.
Hii
inaweza isikubalike kwa baadhi ya watu ila ni mawazo binafsi kuwa azimia kila
anayeingia ndani avue viatu mlangoni. Viatu vya wanawake vilivyo na visigino
vya ncha kali mara nyingine vinakwaruza sakafu za marumaru na mbao na kuacha
alama na vile vya wanaume baadhi vina soli zinazoacha rangi sakafuni na hivyo
kufanya sakafu ionekane zee kuliko kawaida.
Mwaka huu
lenga kuweka nyumba yako nadhifu kila mara kama
vile unategemea mgeni wa heshima!
Makala hii imeandaliwa na Vivi O. Machange. Vivi
ni mjasiriamali upande wa usafi wa magari, nguo na mazulia; pia ana mapenzi
makubwa ya mitindo na mapambo ya nyumbani. Kwa maoni au maswali tuma kwenda
0755 200023 au viviobed@yahoo.co.uk
Subscribe to:
Posts (Atom)