Tuesday, March 22, 2016

Vigezo vya pazia za chumba cha kulala



Katika chumba chochote ndani ya nyumba, pazia linachukua sehemu kubwa ya muonekano kwa kivyo linaweza kuwa kivutio au likaharibu. Habari njema ni kwamba kuna aina nyingi za mitindo ya mapazia kuendana na kila nyumba na kila gharama. Yapo mapazia ya kifahari sana na yapo ya gharama nafuu kabisa.

Ili kupata matokeo unayoyataka, kuna baadhi ya
mambo ya kuzingatia unapotaka kununua pazia za chumba cha kulala tofauti na zile za sebuleni au chumba cha chakula.

Ingawa wengi wanachukulia kuwa kipaumbele cha kuchagua mapazia ni kuangalia michoro na rangi kwanza, kiuhalisia hivi ni vitu vya mwisho kabisa kuvitazama wakati unapotaka kununua pazia kwa ajili ya chumba unacholala. Hii ni kwa sababu, pazia utakazoweka lazima zina mguso fulani kwenye maisha yako ya hapo chumbani.

Kimsingi jambo la kwanza kabisa la kuangalia kwa pazia za chumbani ni uzito na unene wa kutosha kuweza kuzuia mwanga unaoingia  chumbani ukiwa umelala. Mwanga huu unaweza kuwa wa jua la asubuhi ama wa taa za nje zilizowashwa usiku au hata wa radi. Swala la mwanga linaweza lisiwe kikwazo kwa wanaoishi vijijini maeneo ambayo nyumba imezungukwa na mimea/miti mingi, ila ni muhimu sana kwa wanaoishi nyumba zenye uwazi mkubwa nje unaoruhusu mwanga mwingi kuingia ndani ya nyumba. Pazia kama za pamba na sufi ni nzito ambazo zinaweza kukidhi vigezo hivi.

Kujaribu pazia ili kuona linapitisha kiasi gani cha mwanga, ni rahisi kama kuchukua tochi ndogo ya mfukoni na kumulika kitambaa cha pazia unalotaka kununua. Kwa jinsi hiyo unatapa uelewa wa kiasi cha mwanga ambacho pazia hiyo inaruhusu.

Ni muhimu kufahamu pia kuwa pazia zenye rangi za giza au kwa maneno mengine rangi nzito kama zile za zambarau, bluu na rangi ya udongo zinazuia mwanga zaidi kuliko zile za rangi nyepesi. Kwa maana hiyo hizi za rangi nzito zinakufaa zaidi kwenye chumba cha kulala.

Kama ukiona pazia lenye michoro ambayo hakika umeipenda lakini linaruhusu mwanga mwingi, ambacho unaweza kufanya ni kulinunua lakini ukaenda kwa fundi cherehani akaliongezea kitambaa cha rangi nzito kwa ndani. Kitambaa hiki tunakiita lining. Kwa mfano ukiwa na pazia lenye michoro hiyo unayopenda na ukaweka lining nyeusi bila shaka utakuwa umenunua pazia unalolipenda na hapohapo likakidhi hitaji la kuzuia mwanga. Kwa mwingine lining inaweza kuwa gharama mara mbili kwa ajili ukubwa wake ni sawa na ule wa pazia. Endapo ni hivyo unachoweza kufanya ni kununua pazia yako uliyopenda japo haikidhi kiwango cha mwanga lakini ukatengeneza vitambaa vya kufunika madirishani ukiwa umelala. Vitambaa hivi vitakuwa tu sawa na ukubwa wa dirisha na sio ukubwa wa pazia tofauti na vile vya lining. Wakati ukiwa umeamka unaondoa vitambaa hivyo na kubakia na pazia lako unalolipenda.

Natumai umejifunza kitu kutokana na mambo ya kuzingatia kwa ajili ya pazia za chumba cha kulala. Tukutane makala ijayo.


Vivi anakkuwezesha kupendezesha nyumba yako. Simu 0755 200023

No comments:

Post a Comment