Msomaji
wangu kichwa cha makala hii ni kama vile
kinakurudisha darasani! Je, unaikumbuka milango mitano ya fahamu? Mara nyingi
tunasahau, wakati wa kupamba nyumba zetu tunazingatia mlango mmoja tu wa fahamu
ambao ni macho. Ni vyema kuhusisha
pia milango minne iliyobaki, ambayo ni ngozi
inayokupa hisia au mguso, pua inayokupa harufu, masikio yanayokupa sauti na ulimi
unaokuwezesha kutambua ladha.
Mfano mzuri wa eneo
ambalo ninaweza kusema kuwa kuonekana kwake kunahusisha milango yote mitano ya
fahamu ni ufukweni. Muonekano wa uzuri wa
bahari, sauti ya mawimbi yake, harufu, ladha ya maji ya chumvi, hisia za
mchanga kwenye nyayo za miguu na upepo
unaokupiga usoni.
Ingawaje ufukwe unaonekana
mzuri lakini kuleta manadhari yake ndani ya nyumba haifurahishi kwa ajili
hupati kuhusisha ile milango mitano ya fahamu kama ufukwe halisi, utanisamehe
kama mapambo yako ya ndani yana mandhari ya ufukweni.
Kwahivyo kwa wengi
wetu wakati wa kupamba mlango pekee wa fahamu tunaouhusisha ni jicho, kwa maana
ya kujali tu muonekano utakaopatikana.Kuhusisha milango minne ya fahamu
iliyobaki ni njia ambayo itafanya sehemu unayopamba ipendeze na itumike zaidi
kwa lengo lililokusudiwa.
Tukianza na mlango wa
fahamu wa jicho; mpangilio, rangi na mwanga ni vitu vikuu vitatu ambavyo
vinahusika hapa. Rangi inaweza kukuchangamsha au kukutuliza. Mwanga unaweza
kuelekeza jicho lako mahali fulani na mpangilio uwe ni wa fenicha na mapambo
madogodogo unaleta hisia za uwiano na utulivu.
Kwa upande wa pua
ambayo inawezesha kunusa kwenye kupamba unaweza kuhusisha mapambo ambayo
yatakupa harufu, iwe ni maua, mishumaa, viungo, mafuta, mimea inayotoa harufu
au pafyum . Harufu ndani ya nyumba inasaidia kuleta hisia za mahaba. Vilevile usisahau faida za kufungua dirisha,
hewa safi toka nje inasaidia kuboresha ile ya ndani.
Njia kuu ya kuhusisha
mlango wa fahamu wa ngozi ni kwa vitambaa na malighafi unazotumia kupambia. Iwe
iwavyo chumba kilichopambwa pindi kinapotumika kinagusishwa na ngozi, yupo
atakaye kalia kiti na yupo atakayependa kulala sakafuni na vilevile kugusana na
vitu. Chagua vitambaa na blanketi ambazo unajisikia vizuri zinapokusa ngozi
yako. Chagua sakafu ambayo utapenda kutembea ukiwa miguu mitupu. Kwa mfano kuna
malighafi za sofa ambazo ukiiangalia hujisikii hata ukalie sofa lenyewe na zipo
zingine unatamani kukaa kabla hata ya kukaribishwa ukae. Tuseme unaishi maeneo
ya baridi au ndani kwako ni baridi labda kwa ajili unatumia kiyoyozi; halafu
malighafi iliyotengenezea sofa nayo ni aina ya plastiki, bila shaka huwezi
kuvutiwa kukalia sofa lenyewe. Unaweza kubadilisha malighafi kuendana na msimu,
kwa mfano msimu wa baridi kali malighafi za pamba zinaleta hizia nzuri zaidi
kuliko za plastiki. Kwahivyo hisia zinazopatikana wakati wa mguso wa ngozi na
mapambo yako zitaonyesha ni kwa jinsi gani umeshirikisha vyema mlango huo wa
fahamu.
Kwa upande wa
kushirikisha mlango wa fahamu wa sikio ambao unakupa sauti, fahamu kuwa sauti
ndani ya nyumba ni jambo muhimu mno katika kuonyesha tabia ya nyumba husika.
Sikiliza sauti zinazosikika ukiwa ndani mwako ili uweze kutengeneza mazingira
ya utulivu. Je sauti ya hiyo mota ya jokofu au kicheko cha jirani au mlango
wenye bawaba zinazopiga kelele zinakupa mazingira unayofurahia? Endapo
unafurahia mziki mkubwa basi sambaza spika ndogo ndogo chumbani ili sauti isambae vizuri kwani ikitoka kwenye
chanzo kimoja inasababisha kelele. Fikiria namna ya kuondoa sauti zinazokukera.
Mlango wa mwisho wa
kuuongelea katika upambaji wako ni ulimi, ambao unakupa ladha. Katika upambaji
ladha inakuwa tofauti na ile ya chakula. Ladha hapa inamaanisha ni kwa namna
gani upambaji wako unakurahisia maisha yako ya kila siku. Tunaangalia ni kwa
namna gani chumba kilichopambwa kitatumika kuburudisha katika maisha ya kila
siku. Je kuna kimeza pembeni cha kuwekea kikombe cha kahawa pale utakapokuwa
umekaa kwenye sofa huku unataka kunywa kahawa yako? Inakuwaje kama ukimwagia
kitu kwenye sofa? Ni ile ladha tunayotaka chumba kiwe nayo kuwezesha yoyote anayeishia
hapo arahisishe maisha yake.
Kwahivyo kama ambavyo tumeona ni kwamba ukipamba kwa kuzingatia
milango yote mitano ya fahamu eneo linapendeza na kutumika ipasavyo tofauti na
pale unapotumia mlango mmoja tu. Unadhani ni mlango upi wa fahamu ambao umeutumia
zaidi kwenye mapambo ya nyumba yako. Nijulishe kwenye maoni!
Makala
hii imeandaliwa na Vivi, kwa maoni au maswali tembelea
www.vivimachange.blogspot.com
No comments:
Post a Comment