Njia za gharama nafuu na haraka za kubadilisha muonekano wa ndani ya
nyumba yako.
Watu wengi wanafikiria kuwa kupamba ndani ya nyumba ni jambo
kubwa na ambalo linahitaji hela nyingi. Lakini hii sio kweli, mtu anaweza
kutafiti njia za kupamba nyumba kwenye mitandao au majarida ya mapambo ya
nyumbani na kuona ni njia zipi
zinazoweza kumfaa kwa gharama aliyo nayo. Makala hii ni mojawapo ya vyanzo vitakavyokupa
mawazo ya njia rahisi na za haraka zaidi za kupamba ndani ya nyumba yako kwa
namna maridadi kabisa.
Kabati la mapambo ni njia mojawapo ya gharama nafuu na ya haraka
ya kupamba ndani ya nyumba. Kabati hili unaweza kulitengenezersha kwa fundi kwa
mtindo unaotaka wewe mwenyewe iwe ni kwa sehemu kubwa kuwa ni kioo kitupu au
mchanganyiko wa mbao nusu na kioo nusu. Linaweza kuwekwa sehemu
ya kona ya chumba.
Linapokuja swala la mapambo ya kabati la mapambo, eneo la
ndani ndio la kujali zaidi. Pamoja na mtindo wa kabati husika vioo pamoja na
taa ya ndani ya kabati vinamaliza kila kitu! Mapambo ya aina mbalimbali huwekwa
ndani ya kabati hili na kuleta muonekano wa kuvutia. Na pia wengine hupendelea
kuweka glass za kifahari za mvinyo za aina ya crystal na hii inalipendezesha mno kabati kwa kweli. Tunu sio kitu ambacho umenunua karibuni kwa hela nyingi. Ni kitu ambacho
kina thamani kwako zaidi ya pesa inavyoweza kununua. Inaweza kuwa ni sanaa
uliyopewa toka kwa bibi na imepitia vizazi kadha wa kadha hadi kukufikia wewe
au inawezekana ni kitu kilichokuwa sehemu ya maisha yako ya utotoni au kitu
maalum ulichopewa na mtu maalum. Ukizungusha macho yako kukitazama kinakupa
burudiko la nafsi.
Ndani ya kabati la mapambo waweza weka pia mdoli
wako ambao unadhani ni wa kipekee na unafaa kuwepo hapo. Pia waweza weka vitu
mbalimbali kutoka sehemu tofauti za dunia. Zingatia kua huna haja ya
kusongamani kila sanaa uliyonayo kwenye kabati lako la mapambo. Hakikisha
unaacha nafasi kati ya kitu na kitu ili isilete muonekano wa mrundikano. Chochote
ambacho unadhani kitafanya kabati lako lipendeze waweza weka humo.
Njia nyingine ya kupamba ndani kwa gharama nafuu na kwa
haraka ni kwa kutumia maua ya kutenengeneza (maua mfu). Maua na mimea inafanya
muonekano wa mahali uwe wa kuvutia. Mtu anaweza kuweka mimea na maua kadhaa ya
kutengeneza katika sehemu tofauti tofauti za nyumba yake. Staili na rangi ya
maua na mimea hii iendane na rangi ya chumba cha nyumba. Maua hayo yanaweza
kuwekwa sakafuni au juu ya meza vilevile.
Mtu
anaweza kutumia vibebeo vya mishumaa kupambia nyumba yake na ikaonekana
maridadi. Unaweza kutafuta aina mbalimbali ya vibebeo hivi kwenye maduka ya
mapambo ya ndani na unaweza kuchagua vya mbao au vya kioo.
Mito
ni njia nyingine ya kupamba kwa gharama nafuu na kwa haraka. Unajisikia
burudani ukiwa na mito ya staili na maumbo mbalimbali. Unaweza kutupia mito
kadhaa ya mapambo kwenye seti zako za sofa
ambapo zitaleta matokeo makubwa na itakuwa vyema zaidi kama ukitumia mito ya rangi
nyekundu na ya chungwa.
Badilisha muonekano wa madirisha kwa kubadilisha pazia na
fimbo. Hii sio usumbufu kama ambavyo unaweza kufikiri kwani kuna maduka mengi
yanayouza pazia ambazo zimeshonwa tayari. Na kwa swala la fimbo zake kwa ajili
tayari kuna vishikizo vilivyotobolewa, ni kiasi tu cha kuondoa fimbo ya mtindo mmoja
na kupachika nyingine ya mtindo tofauti bila ya kutoboa ukuta tena.
Hizo ni njia za gharama nafuu na haraka zaidi za kupamba nyumba yako.
Jaribu mojawapo na utarudi kunishukuru.
Makala hii imeandaliwa
na Vivi Machange ambaye ni mjasiriamali
upande wa usafi wa nguo, mazulia na magari; pia ana mapenzi makubwa ya
muonekano wa nyumba. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au
christines.daughter@yahoo.com