Friday, September 26, 2014

---nitavukaje--Kutoka ualimu wa kuajiriwa hadi kujiajiri kwa kufungua media company

Leo katika mfululizo wa stori zangu za kukuwezesha kuvuka kutoka daraja ulilopo kwenda la juu nimeongea na entrepreneur  Fred Kirya ambaye alikuwa mwalimu hapo kabla lakini sasa ana media company. Nikamuuliza amevukaje? Akaniambia alivyokuwa mwalimu alijishughulisha pia na kuandaa program za vijana walioathirika na mambo mbalimbali, watukutu na hata wanajeshi waliotoka vitani halafu vichwa vikavyatuka kiana. Kutoka huko baadhi wa vijana walioweza kuachana na hali hizo wakawa wanaenda kuongea kwenye vituo mbalimbali vya redio. Hapo ndipo Fred alipojenga interest na media na akafungua media company yake ambayo anarekodi nyimbo za kwaya, singles za wasanii, program za watoto na vipindi vya vijana kwenye vituo vya redio. Fred anasema kwa kufanya kazi kwenye kampuni yake mwenyewe ana furaha ya kufanya anachokipenda, kuwa makini zaidi kwa mfano matumizi na utunzaji wa vifaa vya kazi na kubwa zaidi financially amekuwa na wise spending...... Kaa standby kusoma stori nyingine itakayofuata...

usisahau kuwekea mbolea bustani yako kwenye vuli hii

Mvua za vuli zimepamba moto kabla ya kuingia kwenye masika. Ukiweka mbolea kipindi hiki ikakutana na masika yanayokuja itasaidia mno kuboresha bustani yako.


Thursday, September 25, 2014

my article for newspaper: jiko safi ukiendelea kupika


Baadhi ya siku unaweza kushangaa kama kupika kunalipa kwa nguvu yote inayotumika. Kweli, unaweza kuweka mlo kabambe mezani, lakini jiko lako likaishia kuwa chafu mno kwa, mrundikano wa vyombo vichafu. Unaweza ukawaza kuwa inaenda kuchukua muda mwingi kusafisha kuliko kula!

Kanuni kuu ya jiko kuwa safi wakati ukiendelea kupika, ni kuanza na jiko safi. Kwa njia hii uchafu unaokuogopesha ni ule unaotengeneza wakati wa kupika tu. Kwa mazoea wengi wanajitahidi kuacha jiko safi kabla ya kwenda kitandani kila ifikapo usiku. Vyombo visafi vinawekwa kabatini, vile vichafu vinaoshwa, viporo vinawekwa kwenye vikontena na kuwekwa ndani ya jokofu, ndoo ya uchafu inamwagwa na kwa namna hiyo hakuna uchafu unaobaki jikoni.
.
Siri ya kufanya jiko liwe safi wakati unapoendelea kupika ni kuosha kadri vinavyochafuka. Nadhani hakuna njia nzuri zaidi ya kusisitiza hili. Kama wali unaendelea kuiva kwa dakika 20, una muda wa kusafisha. Kama kuna muda wa kusubiria chakula kiive, basi kuna muda wa kusafisha. Inashangaza jinsi tunavyodharau hizi dakika 10 (au zaidi!) ambazo zingeweza kurahisisha kazi yetu ya kusafisha hapo baadaye. Safisha kwanza, na utakuwa na muda wa kupumzika na kufurahia chakula chako baadaye.

Pimia vyakula ndani ya sinki, na rudisha kila kitu mahali pake baada ya kukitumia ili kaunta isishamiri vitu. Jitihidi kuwa unafanya maandalizi yanayotakiwa kabla ya kuwasha jiko. Kama unatumia kikombe au kijiko cha kupimia, hakikisha unakisuuza papo kwa hapo mara baada ya kukitumia. Futa vyakula kwenye kaunta kila vinapowagika, hii itasaidia kuzifanya kaunta zako zisiwe vululu vululu na kukusababishia kazi kubwa ya kusafisha baadaye. Hii pia inasaidia kuwa na eneo la kutosha kufanyia kazi. Nyanya ndio kiungo kinachochafua zaidi kaunta. Haiepukiki kupata matone ya nyanya ukutani na hata juu ya stovu. Kufuta punde kwa kitambaa cha unyevu kunasafisha mara moja, kwa ajili tone halijakomaa. Kwa chakula ama kiungo chochote kile kilichomwagika jikoni mwako safisha kabla hayijakaukia kwenye eneo husika. Itasaidia kuokoa muda na machukizo baadaye.

Hifadhi vifaa na vyakula unavotumia mara kwa mara maeneo ya karibu na safisha makabati yako ya jikoni na jokofu kwa msimu. Kwa namna hii hutakuwa na haja ya kuondoa vitu vyote kabatini kwa ajili ya kutafuta kitu kimoja unachohitaji.

Wakati unapopika tumia vyombo vichache. Kwa mfano, wakati unapotaka  kumenya viazi badala ya kumenyea maganda kwenye chombo, tumia mfuko au gazeti mbapo utabeba na kutupa moja kwa moja kwenye ndoo ya taka na hivyo kupungukiwa na chombo cha kuosha.

Kwa siku zile ambazo una muda mchache sana, pika vyakula rahisi ambavyo havihitaji kutumia sufuria na vikaangio vingi. Fanya mapishi ambayo chakula zaidi ya kimoja kinapikiwa kwenye sufuria moja, mifano ni mchemsho na mbogamboga.

Endapo utakuwa na mapishi kwa ajili ya wageni kadhaa nyumbani, basi gawa kazi yako. Fikiria ni nini unaweza kuandaa usiku mmoja kabla ya ugeni wako. Hii itasaidia kufanya maandalizi na kujikuta baada ya tukio ukiwa na vyombo vichache vya kusafisha. Kama utapika maharage kwa mfano, unaweza kuyasafisha na kuloweka usiku. Halafu unayaacha yamekaa kwenye jokofu, hadi kesho yake wakati wa kuyapika.

Kupunguza mrundikano kwenye kaunta inafanya wepesi wa kusafisha jiko lako. Unavyokuwa na vitu vingi kwenye kaunta ndivyo inavyokupasa kuvisogeza vyote kabla ya kusafisha na hii inakupa kazi kubwa. Baadhi ya watu kanuni ni kuwa, hakuna kifaa chochote kukaa juu ya kaunta vinginevyo kiwe ni kile tu kinachotumika kila siku kwa mfano kipashio cha chakula. Vingine vyote kama visagio na kadhalika vinahifadhiwa kabatini hadi wakati wa matumizi ndipo vinapotolewa. Usipende vijiko na visu vyako vikae juu vikibeba mafuta mafuta na vumbi. Viweke kwenye droo lililo karibu na stovu, ili unapovihitaji iwe rahisi kufungua na kuchuka. Havina haja ya kuwa juu ya kaunta na kula eneo lako la kazi.

Hizi ni baadhi ya njia za kukuwezesha kuweka jiko safi wakati ukiendelea kupika. Je, wewe msomaji wangu ni kwa namna gani unaweka jiko lako safi wakati ukiendelea kupika? Nitafurahi kusikia toka kwako!


Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi na pia ni mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com

--vuka--kutoka architect muajiriwa hadi kujiajiri

Vijana wetu wengi mara wanapomaliza chuo wanaanza kusaka ajira. Wengi wanashindwa kuamini kuwa wanaweza kujiajiri kwa kufanya kile ambacho tayari wameshakuwa na ujuzi nacho. Leo nimechat na Caleb ambaye ni architect, nikamuuliza ni kwa vip ameweza kujiajiri. Alichoniambia ni kuwa mara baada ya kumaliza chuo aliajiriwa kwa miaka miwili. Wakati huo alikuwa anafanya vikao na wateja wake binafsi nyakati za jioni baada ya kazi za mwajiri wake. Mambo yalivyochanganya akajiajiri. Nikamuuliza maana ya mambo kuchanganya ni nini? Akasema alipata mradi wa mwaka mmoja kwenye kazi yake hiyo ambapo alijiaminisha kuwa akijiairi wakati wa mradi huo itakuwa ni wakati muafaka kwani hata kwa miaka miwili mbele asingepata mradi, mwingine mkubwa bado angeweza ku survive kwa zile kazi ndogondogo. Anasema ana uhuru zaidi wa binafsi na kipesa alivyo sasa kuliko alivyokuwa ameajiriwa. Umepata cha kujifunza hapo? Nawe waweza vuka ulipo kwenda upande wa pili ulio bora zaidi.

Tuesday, September 23, 2014

-vuka---kutoka daraja la uzururaji hadi fundi mechanic

nimekutana na hii nikaipenda na nikaamini ni daraja ambalo vijana wengi wangeweza kuvukia. unaweza ukadhani walivyolifumua fumua gari wapo Japan kumbe ni hapa hapa TZ...
hii ni chasis mpya baada ya gari kufumuliwa na ile ya zamani kuondolewa. Inaoshwa ipakwe rangi ndio kijumba cha gari kipachikwe.
chasis la zamani lililoondolewa kwa ajili gari lilikuwa limepata ajali na hivyo chasis kupinda.

kijumba kikisubiri chasis ikamilike ili kipachikwe.

----vuka----

friends,
as nina spirit ya biashara nimependa kuweka "nitavukaje" ambacho ni kijisegement kitakachokupa hadithi fupi sana ya mafanikio itakayokutia moyo na hata kuweza kukupa wazo la biashara. karibu...

Monday, September 22, 2014

vitu hivi vitaiongezea bedroom yako mashiko...

1. ki carpet...chochote kile ili mradi miguu isipate ubaridi na ugumu

2. mito ya kumwaga...

3. sehemu ya kukaa ambayo sio kitandani

4. vitu/picha unazopenda zinazokupa kumbukumbu nzuri

5. ugiza giza...bedroom ikiwa nyeupe saana mashiko yanapungua, weka pazia ambazo zinaua mwanga kiaina

Thursday, September 18, 2014

my article for newspaper: vifaa vya msingi jiko dogo la kisasa


Huenda pengine ndio unaanza maisha ya kujitegemea au ya ndoa, unahitaji kuwa na vifaa vya msingi jikoni vya kuanzia kwa miezi michache ya mwanzo—hata miaka michache. Au labda ni mzazi unayetaka kumsaidia huyo kijana wako, binti au rafiki namna ya kuanza maisha. Pia kama ni bibi harusi mtarajiwa makala hii inakuhusu. Nimefanya kazi kubwa ya kutafiti katika maduka ya vifaa vya jikoni na kukuandalia orodha ya vifaa vya msingi kabisa vinavyotakiwa kuwepo jikoni kwa ajili ya kukuwezesha kuandaa chakula katika maisha yako hayo mapya.

Nia hapa ni kuonyesha orodha ya vifaa vya kawaida kabisa vya msingi vya jiko dogo la kisasa.
Ni rahisi kuangukia kwenye ushawishi wa muonekano lakini kitu kimoja cha kujua kwa kweli ni kuwa hauna haja ya kuvunja benki ili kuwa na vifaa vya jikoni vya kiwango.  Orodha hii ya vifaa vya msingi jikoni inaweza kubadilika kutokana na hitaji la mhusika. Pia vyombo vya mezani kama vile sahani vijiko na glasi vinategemea zaidi ladha ya mtu binafsi na kwa sababu hiyo sijaviorodhesha hapa. Kwa hivyo vifaa vya msingi vya jiko dogo la kisasa ni kama vifuatavyo:

Visu

Kisu kikali cha mpishi ni moja kati ya vifaa muhimu zaidi jikoni, na kama utanunua kilicho sahihi kitatumika kwa miaka mingi. Nunua visu vya jikoni ambavyo havishiki kutu.

Ubao wa kukatia

Ubao sahihi wa kukatia utafanya visu vyako vidumu, na rahisi kusafishika. Kuna aina nyingi za mbao hizi kama vile plastiki, miti na hata glasi.

Kifungulia chupa na makopo (opener)

Nunua ambayo unaweza kufungulia chupa na makopo ya aina tofauti tofauti. Nzuri ni ile iliyo rahisi kwa matumizi.

Kisaga vyakula (Blender)

Kama kawaida nunua ambayo ni rahisi kutumia na yenye kazi nyingi tofauti ambapo utaweza kusaga vyakula vyako na kutengeneza juisi.

Vikaangio na masufuria

Iwe uko singo au ni wanandoa wapya kwa kuanzia unahitaji vikaangio japo viwili na sufuria nne hadi sita. Sokoni vikaangio na sufuria zipo zilizotengenezwa kwa material nyingi mno. Nunua ambazo hazing’ang’aniani na chakula (nonstick).
Stovu
Watengenezaji wengi wameunganisha stovu na tanuri ukinunua mbayo unaweza kutumia nishati zaidi ya moja itakuwa ni busara zaidi.

Jokofu
Kwa maeneo mengi ya nchi yetu walau inahitajika kuwa na jokofu kwa ajili ya kuhifadhia chakula kisiharibike. Kwa kuanzia si mbaya ukawa nalo dogo kwenye jiko lako hili la kuanzia maisha.

Kipasha chakula (Microwave)
Hiki kinafanya kazi kubwa ya kupashia na hata kupikia baadhi vya vyakula. Habari njema ni kuwa zipo za bei rahisi kabisa. Ni rahisi kutumia na wengi wanapendelea kuziweka juu ya kaunta ya jiko. Huna haja tena ya kupashia chakula kwenye sufuria.

Kikausha mikate (Toaster)

Hiki nacho kwa wengi wanaopendelea kula mikate iliyokaushwa huwa wanakiweka juu ya kauta.
Mabakuli/Vikontena
Wanasema mapishi ni sanaa, sio? Kuwa na mabakuli na vikontena ndani ya jiko lako la kuanzia maisha vitakusaidia katika maandalizi ya mapishi na hata vikontena vitakusaidia kupashia na pia kuhifadhia vyakula kwenye jokofu.

Kindoo cha uchafu
Unapoandaa chakula na kuosha vyombo lazima utahitaji hiki kindoo kwa ajili ya kuwekea uchafu. Ni muhimu kiwe kile cha mfuniko wa kujifunga chenyewe.
Jiko lenye vifaa vya msingi vinavyopaswa kuwepo jikoni ni rafiki kwa mpishi. Unapokuwa na vifaa sahihi na unajua jinsi ya kuvitumia, unaweza kuelekeza akili yako kwenye chakula unachoandaa. Kama nilivyosema awali vifaa hivi vinaweza kuongezeka kutegemea na mhusika na mazingira unaweza kuwa na vifaa hivi vya msingi jikoni kwa kuanzia na baadaye ukaongeza kidogo kidogo kwa kadri ya mahitaji yako. Mpishi mzuri anatumia vifaa tofauti tofauti na mwishoni anapata vile hasa anavyohitaji.


Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi na pia ni mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com

Tuesday, September 16, 2014

pambo hili lina faida lukuki...

Pambo hili na jamii yake linafaa kuwekwa ukutani na mlangoni kwa ajili kwa umbo lake huwa linakuwa flati upande mmoja na kitumbo upande wa pili. Ndani kuna nafasi kiasi kwamba likiwa kama pambo; wakati huohuo unaweza kuhifadhi vitu vidogo dogo kwama vile dawa zilizo kwenye pakiti, uzi na kadhalika. Laa kama unataka kusisitiza pambo lako basi weka maua ya artificial badala ya vikorokoro kama huyu hapa kwenye picha alivyoweka. Lilivyotengenezwa material yake sio nzito. Unaweza kulitumia miaka nenda rudi. Linapatikana kwenye maduka yanayouzwa mapambo ya ndani. Perfecto!



Thursday, September 11, 2014

my article for newspaper: Jinsi ya kupata kizulia sahihi cha jikoni


Wengi tutakubaliana kuwa zulia la ukuta kwa ukuta sio sahihi kuwekwa jikoni, ila kizulia cha kutupia kina faida kadha wa kadha jikoni. Kizulia hiki kinasaidia kuepusha miguu na sakafu ya baridi na kinaongeza rangi, hata kiwe kidogo namna gani. Yote kwa yote sababu kuu yaweza kuwa ni kwa ajili ya burudani ya miguu na kuiepusha na baridi. Kama unaweza kusikia baridi ya kukera kwenye nyumba yako mwenyewe basi ni ukakasi. Kuweka kizulia jikoni kunakamilisha sakafu na mvuto wa jiko. Vinginevyo uwe unapenda sana rangi kiasi kwamba umepaka kabati zako za jikoni rangi ya kung’aa kama vile pinki, kijani ama nyekundu.

Kizulia cha kutupia kinaweza kuleta rangi bila kukufanya utumie hela nyingi, kama hii ndio sababu ya kuamua kuweka kizulia jikoni hapa basi ni dondoo chache za kukusaidia kupata kilicho sahihi.
Kuchagua kizulia sahihi kwa ajili ya jiko, ni vyema kufahamu nia yako kuu ya kuamua kukinunua. Inaweza kuwa ni kwa ajili ya kuepusha miguu na ubaridi wa sakafu au kuongeza staili, rangi na mvuto kwenye sakafu ya jiko. Pia fikiria ukubwa na umbo la kizulia ambacho kitafaa zaidi kwa nafasi iliyopo. Usisahau kuzingatia vifaa vilivyotumika kutengenezea kizulia utakacho na kufahamu ni utunzaji kiasi gani utakaohitajika. Chagua kizulia ambacho hakitelezi (hakikimbii sakafu) kwa ajili ya sababu za kiusalama.

Hasa kama sakafu ya jiko lako ni laini, yakung’aa na inayoteleza, ni muhimu sana kuchagua kizulia chenye mnato/mpira kwa chini kinaposhikana na sakafu. Mpira huo utasaidia kizulia kikae mahali pamoja kisihame hame kinapokanyagwa, ambapo kinaweza kusababisha mtu kuanguka.

Chagua mahali sahihi pa kuweka kizulia chako cha jikoni. Ni wapi unapotumia muda mwingi unapokuwa  jikoni? Pengine ni mbele ya sinki, kwa hiyo ni kuwa utachagua kuweka kizulia eneo hili. Au labda una eneo kubwa la kutembea kwenye sakafu ya jikoni. Basi angalia mahali hapo kati unapoweza kutupia kizulia chako ili kilete burudani ya miguu maeneo kadhaa. Vile vizulia vyembamba virefu vinafaa zaidi wa jiko lenye sakafu ndogo.

Kama lengo lako kuu la kuhitaji kizulia jikoni ni kuondoa ubaridi na kuleta nesa nesa ya miguu, basi unene wa kizulia unahusu. Utahitaji mbonyeo kati ya sakafu ngumu na miguu yako kwa burudani. Ulaini wa kizulia pia unaepusha miguu yako na baridi la sakafu ya marumaru au mbao au hata saruji. Hakuna anayetaka kuwa kwenye maumivu wakati akiosha vyombo!

Chagua manyonya sahihi, iwe ni sufi au pamba. Kizulia ambacho kinasafishika kirahisi kwa sabuni na maji. Urahisi wa kusafisha ni lazima ukumbukwe kwenye kuchagua kizulia cha jikoni, hasa kwa vile vinavyowekwa chini ya sinki au mbele ya stovu au jokofu. Vizulia vya sufi vinaweza kuwa chaguo sahihi kimuonekano ila kwa kawaida vinashika madoa kirahisi na vinahitaji usafishaji wa kitaalam kwahivyo ni vyema kuweka vizulia vya aina hii kwenye vyumba vingine nyumbani ila sio jikoni au chumba cha kulia chakula, anasema muuzaji Aisha Mbegu. Vizulia vya kufumwa kwa mimea ya asili kama vile katani au majani ya baharini vinaweza kuwa chaguo sahihi kwa ajili ya kuweka chini ya meza ya kulia chakula, kwa ajili kwa kawaida ni rahsisi kuvifuta na kusafisha hata kwa kufagia.

Haijalishi utaamua kuchagua kizulia cha jkoni kilichotengenezwa kwa vifaa vya aina gani, kuchukua kipimo cha eneo unalotaka kuweka kizulia ndani ya jiko lako itakusaidia kupata kilicho sahihi. Wakati wa kuamua aina za vizulia, jitahidi kutafakari rangi, na ni kwa namna gani ukubwa  na muundo utakavyogusa muonekano mzima wa jiko lako.

Wacha kizulia chako kitengeneze stori. Chagua ambacho kitaongeza uzuri kwenye jiko lako. Sakafu za jiko huwa zinapooza, kizulia kinaweza kuongeza uchangamfu na ladha binafsi kwa kuunganisha rangi za jiko pamoja. Kama nilivyosema kabla, chagua kizulia kitakachoongeza rangi, ambapo ni rahisi kubadilisha kizulia ili kuondoa muonekano wa jiko utakapochoka zile rangi zake za kudumu ulizozizoea.

Hongera kwa kufanya eneo kla sakafu ya jiko lako kuwa na mvuto, nesanesa na budurani! Utakapoweka kizulia cha jikoni hutatamani kukiacha.


Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi na pia ni mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com

Wednesday, September 10, 2014

kwanini ni muhimu kufua carpet kwa sabauni na maji ya pressure

ninapata amazing deal ya kufua mazulia ya manyoya kwa ajili wateja wengi wanayaleta kutokana na kuwa yananuka vibaya. Carpet linapokuwa na harufu mbaya kwa kuwa labda limemwagikiwa vimiminika pengine ni wakati wa sherehe au maisha ya kawaida ya kila siku na pilika za watoto, kusafisha kwa vacuum cleaner au form cleaner haitawezekana kuondoa harufu mbaya ya zulia la manyoya likiloa linavyonuka.

Kinachotakiwa kufanyika ni kuniletea carpet lako kwa kuwa tuna pressure washer ya kuweza kulipiga maji, kuweka detergent na kulisugua hadi mabaki yote ya vyakula (eg ubwabwa wa sikukuu) na vimiminika vyote vitoke. Baada ya hapo tunaanika kwenye jua kali kwa siku mbili na zulia lako linakuwa tayari kama jipya. Kuamua kufua zulia kwa maji inaweza kuchangiwa pia na uchafu mwingine wowote kama vile vumbi na tope.

Karibu sana ian car wash tung'arishe tena carpets zako. Tuwasiliane 0755200023
carpets zilizofuliwa, kukauka na kukunjwa

mteja yuko tayari kupelekewa carpets zake kwenye gari

hizi nazo ni za mteja mwingine zinamsubiri

 hizi hazijakaula hivyo tumetandaza ndani tuanike tena kesho


Monday, September 8, 2014

---vitu vizuri---getting better with age

2014, uso unaonekana tight

2014, hapa ni kama vile my face is dropping! heeee he, in my mid 30's

2002, 12 years before nilikuwa hivi; ni nini siri ya kutoruhusu makunyanzi kuja fastaaa. enjoy your monday gators....

Thursday, September 4, 2014

my article for newspaper: kuepusha wadudu ndani ya nyumba

Wakati baadhi ya watu wanaogopa wadudu, wengine wanaweza kuwa wanavutiwa nao. Lakini kitu kimoja ambacho wengi tutakubaliana ni kuwa wadudu makazi yao sio ndani ya nyumba. Si tu kuwa wanaleta mazingira hatarishi kiafaya, bali pia, ni rahisi tu ya kuwa wanaudhi, kuanzia mbu wanaokupigia mziki masikioni mwako, kukuuma na kukusababishia maradhi hadi kwa nyigu anayeweza kukusababishia kidonda.

Hata yule mende wa kawaida anaweza akasababisha mzio hasa kwa watoto, anasema dokta Emil.
Kuepusha wadudu ndani ya nyumba inaweza kuwa ni vita vilivyoshindikana. Bahati nzuri ni kuwa, kwa kufahamu ni nini kinachovutia wadudu ndani ya nyumba yako, unaweza kuanza kufanya mabadiliko ambayo yatawakimbiza kimya kimya.

Kama ilivyo kwa binadamu, wadudu nao wanahitaji chakula, maji na makazi ili kuishi. Kwa kukata usambazaji wa chakula chao na kuvuruga maeneo yao ya kujifisha, unaweza kupunguza tatizo la kuwa na wadudu ndani ya nyumba yako. Kata chanzo chao cha chakula kwa kuhakikisha kuwa vyakula vyote vinawekwa kwenye kontena zilizofungwa vizuri. Mabaki ya vyakula ndani ya nyumba yatupwe eneo moja tu ambalo ni ndoo ya uchafu  yenye mfuniko wa kujifunga wenyewe iliyopo jikoni. Ndoo hii imwagwe na kusafishwa kila siku baada ya kuosha vyombo vya chakula cha usiku. Futa michuzi na mabaki yoyote yanayoweza kuwepo maeneo ya wazi ndani ya nyumba. Osha vyombo punde mara baada ya kutumika. Pipa linalomwagwa uchafu nje nalo liwe na mfuniko.

Usisahau vyakula vya wanyama waliopo nyumbani kwako. Kwa mfano unafuga mbwa na una vyakula vyake vya unga umehifadhi stoo, unga huu unaweza kuvuta mende na sisimizi. Unaweza kuweka dawa za kuzuia wadudu kwenye stoo yako ya chakula cha wanyama unaofuga.
Vifaa vyote vya kuhifadhia mabaki ya vyakula ndani na nje ya nyumba viwe vinasafishwa kwa dawa za kuua wadudu mara kwa mara.

Kama vile mlango uliolokiwa unavyoweza kuwaweka wavamizi nje, mlango uliozibwa sahihi unaweza kuwazuia wadudu wasiingie ndani. Kuepusha wadudu wanaotambaa kuingia ndani kwa kupitia sehemu ya wazi mlangoni, weka kizuizi cha mpira au brashi chini ya mlango. Vizuizi hivi vinapatikana kwenye maduka ya vifaa vya ujenzi, anasema mseremala Simon.

Kumbuka kuwa mbinu zote hizi za kuziba chini ya mlango hazitafanikiwa kama mlango wenyewe utaachwa wazi. Kama una watoto ambao wanasahau kufunga mlango, fikiria kusimika vifunga mlango.
Wenye nyumba wengi wanategemea hewa safi ya nje iingie ndani kupitia milangoni na madirishani. Hii inaweza kuwa majaribu hasa wakati wa kiangazi. Bahati mbaya ni kuwa kiangazi ni wakati mbaya kwa vile mbu na wadudu wengine wengi wanavamia ndani ya nyumba. Kufurahia raha ya hewa safi bila kupata bughudha ya wadudu weka wavu wa kuzuia wadudu kama mbu kwenye madirisha na milango.

Eneo la nje ya nyumba linaweza kuwa linasababisha wingi wa wadudu ndani ya nyumba yako. Endapo mioto ya asili ni mingi na iko karibu sana na ukuta wa nyumba basi tegemea kuwa na mazalia makubwa ya wadudu na hivyo uwezekano wa wengi kujaribu kukimbilia ndani. Hii pia itakufanya hata wewe mwenye nyumba kushindwa kufurahia kukaa kuburudika nje ya nyumba yako, kwa hivyo njia nzuri ya kuepusha wadudu ndani ya nyumba ni kuhakikisha wanaondoka pia kwenye maeneo ya nje ya nyumba.

Majani yaliyorundikwa, matofali yaliyopangwa kwenye yadi yako na hayatumiki tena na mashimo ya maji taka yanafanya makazi ya wadudu mbalimbali. Maeneo haya ni sehemu za kujificha kwa wadudu kama mende nyoka na wengine wengi na hata panya. Mashimo ya maji taka yawe na mifuniko iliyoziba vizuri na mrundikano mwingine wowote uondolewe na utashangazwa ni kwa jinsi gani wadudu watakimbia na mazingira yako yatakavyovutia.

Baadhi ya wenye nyumba wanapendelea kutumia dawa za kupulizia kwa ajili ya kuua wadudu kama mbu na mende. Haijalishi ni njia ipi unatumia ili kuepusha wadudu kufanya makao ndani ya nyumba yako; njia kuu ya kuwafanya wakimbie ni kukata “mirija” wa kile kinachowavutia. Hii inamaanisha ni pamoja na kuondoa mrundikano, vyakula na vyanzo vya maji. Bila kuwa na rasilimali hizi, wadudu watakimbia kwako kuelekea nyumba ya pili na kukuacha ukiwa na amani.

Makala hii imeandaliwa na Vivi Machange ambaye ana mapenzi makubwa juu ya muonekano wa makazi na pia ni mjasiriamali wa usafi wa magari, mazulia na nguo. Kwa maoni au maswali tuma kwenda 0755 200023 au christines.daughter@yahoo.com