‘AY’ au Mzee wa
Commercial ni mmoja kati ya wasanii ambao kwa muda mrefu sasa wako katika
muziki wa kizazi kipya na amefanikiwa kujitunzia jina na ubora wa kazi zake
unazidi kukua siku hadi siku.
Moja ya sababu zilizomfanya kufikia hapo alipo ni
kutokana na kutambua kipaji alichonacho lakini pia amekuwa akionyesha juhudi
binafsi.
Akizungumza na Starehe AY anasema ndoto yake nikuwa
mfanya biashara mkubwa ndani na nje ya nchi na juhudi za kufanikisha hilo
ameonyesha kupitia baadhi ya biashara alizo zianzisha nchini ikiwemo kumiliki
vipindi viwili vinavyotambulika kama ‘Siasa za siasa’ na Mkasi vinavyorushwa
katika kituo cha runinga cha Eatv.
Kipindi hicho kinachorushwa kila siku ya Jumatatu na
luninga ya EATV ni maalum kwa mahojiano ya watu maarufu wa kada mbalimbali
wakiwemo wafanyabishara, wanasiasa na wasanii.
Tofauti na vipindi vingine vya mahojiano, hiki hufanyika
eneo la saloni ambapo muhojiwa hupata fursa ya kuchagua huduma yoyote
inayotolewa na saluni hiyo huku akiendela na mahojiano ambayo hufanywa na
mtangazaji maarufu wa kike Salama Jabiri.
Hata hivyo, katika kipindi hicho Salama anashirikiana na
vijana wawili ambao hufanya kazi katika saloni hiyo ambao pia wakati wa
mahojiano hufanya kazi ya kutoa huduma kwa mteja wao.
“Kufanya biashara na kuwa mfanyabiashara mkubwa ni ndoto
yangu na muziki na umiliki wa vipindi haunipi changamoto sana kutokana na kuwa
nafanya kazi na wasomi, wanaojielewa na kazi zao haziingiliani na kazi yangu ya
muziki,” anasema.
Kwa mujibu wa AY, muziki kwake una faida na hafikirii
kutoka katika tasnia ya muziki kutokana na kuwa ameufanya kwa muda mrefu na
azidi kufanikiwa japo miaka mitano nyuma ulikuwa haulipi ukiliganishwa na sasa.
Anataka mwanamke gani?
AY anasema kuwa hajaoa, hana mchumba wala mtoto wa
kusingiziwa ingawa anatamani kuwa na mwanamke mwenye hekima,akili zakuleta
maendeleo katika familia na nchi kwa ujumla na si urembo pekee.
“Wanawake wazuri wapo wengi, nimekutana na wengi bali
kuchagua mke sahihi ni kitu kinachohitaji busara na endapo nikisema niangalie
uzuri wa mwanamke nitapoteza malengo yangu,naitaji mwanamke ambaye yuko ‘Smart’
kichwani” ,alisema.
Akizungumzia jina la Mzee wa Commercial’ AY anasema jina
hilo alipewa na mtayarishaji wa muziki nchini, Pfunk Majani kutokana na kumuona
akiweza kuitendea haki kila aina ya midundo aliyokuwa akipewa wakati wa
utayarishaji muziki.
“Wasanii Watanzania ni waoga kuuliza yale wasioyajua au
wanayoyajua ila hawana uhakika nayo, wengine hudhani kuwa wanajua mengi kuliko
walio watangulia, tusiwe waoga kuuliza na kufatilia yanayohusu tasnia ya muziki
ili tuweze kufikia malengo kwasababu muziki ni biashara,”anasema.
Akizungumzia kuhusu siasa, AY anasema kuwa hajawahi
kuwaza kuingia katika siasa na wala hapendi japo hana budi kuwaunga mkono
wasanii waliojitokeza kuwania nafasi mbalimbali.
“Tanzania ni nchi ya kidemokrasia, kila mtu anahaki
yakuonyesha mapenzi yake juu ya chama flani, wasanii wanao wasapoti wanasiasa
wako sahihi ila nawasihi kuwa makini na kuepukana na rushwa za muda mfupi
wakumbuke kwamba kuna maisha. baada ya uchaguzi,”anasema Ambwene.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment