Meza ya chakula sio tu sehemu ya kukutana familia
na marafiki wakati wa chakula, bali pia ni fenicha kubwa yenye kuhusika na
muonekano wa ndani. Kama umeshanunua moja au labda unayo tayari bila shaka utakuwa
nayo maisha yako yote. Kwahivyo fanya kila uwezalo ili kuiwezesha ivutie na
idumu miaka mingi.
Pamoja
na kuwepo kwa meza za
chakula za aina mbalimbali, makala hii itakurahisishia
kujua faida ya ile ya mbao lakini yenye kioo juu yake. Kioo hicho aidha unaweza
kuwa umekinunua moja kwa moja na meza yake ama umekitengenezesha kuendana na
muuondo wa meza yako.
Kwanza
kabisa lazima tukubaliane kuwa meza
sahihi unayoweza kuweka kioo juu yake ni ile iliyotengenezwa kwa mbao ngumu
kama vile mninga mkongo na mahogany. Meza ya mbao ngumu hata inapowekewa kioo
cha uzito mnene (ambacho ndicho kinatakiwa) huna wasiwasi kuwa itaporomoka.
Meza nyingine za mbao laini au mabaki ya mbao zinaweza kukuridhisha tu kiuchumi
na muonekano lakini si kitu cha kudumu.
Kwa kawaida kioo ni njia mojawapo ya
kutengeneza hisia za ukubwa wa eneo. Kwahivyo endapo chumba cha chakula ni
kidogo, kuweka kioo juu yake inakupa faida ya kuakisi mwanga na chumba
kuonekana ni kikubwa. Na hata kama umebahatika kuwa na chumba kikubwa, muonekano
wa kioo juu ya meza unaleta umaridadi, mng’ao na fahari ndani ya chumba.
Pia
kioo juu ya meza ni moja ya mapambo ya ndani na kinaifanya meza kuwa kwenye
fasheni isiyopitwa na wakati kwa kuonekana mpya kila siku.
Kioo
juu ya meza kinasaidia kulinda mbao iliyopo chini yake. Hivi vioo huwa ni
vigumu, ambapo inamaanisha hakiwezi kukwaruzika na si cha kuparaganyka kama
kikigogwa. Pia vioo mahususi kwa ajili ya meza vina kiwango vyake vya usalama
kwa hivyo kama kioo hakijaja na meza tafadhali usitengenezeshe kienyeji
shirikisha mtaalam.
Faida
nyingine ya kuwa na meza ya chakula ya mbao yenye kioo juu ni kuwa huna haja ya
kitambaa cha meza. Na pia utunzaji wa meza hii ni rahisi sana. Unaweza kuifuta
bila kuogopa vyakula na majimaji yatabaki yamesimama mezani.
Vivi ni mshauri
wa mapambo ya nyumba. Kwa maoni au maswali tembelea
www.vivimachange.blogspot.com
No comments:
Post a Comment