Hapo kwenye lango kuu la kuingilia nyumbani kwako
almaarufu getini bila shaka ndio mbele ya nyumba yako. Ni eneo ambalo mgeni
wako anapata hisia za mwanzo kabisa juu ya nyumba yako, kwa hivyo pafanye
pavutie. Elimika kwa dondoo hizi za namna ya kuongeza mvuto kwenye eneo la
mbele la lango kuu kwa kuboresha kile kilichopo na kuondoa muonekano wa nyumba
iliyochoka:
· Weka paa juu ya geti. Paa juu ya geti lina faida kama pambo
na matumizi vilevile.
Faida kuu ya paa ni ulinzi wa geti lenyewe kutokana na
maji ya mvua na jua kali. Jua kali linaharibu rangi kwa kuzipausha au
kuzimomonyoa na wakati huo huo maji ya mvua yakisababisha geti kupata kutu
ndani ya miaka michache hasa maeneo ya chini. Kwa kuweka paa inasaidia eneo la
chini liwe kavu na mvua isiloanishe geti moja kwa moja. Faida nyingine ya paa
getini ni kumpa kivuli mgeni wa miguu baada ya kugonga kengele nawe ukitafuta
funguo kwenda kumfungulia. Pamoja na kivuli vile vile paa getini linamkinga
mgeni wakati wa mvua. Kwa upande wa mapambo ni kwamba zipo paa za mitindo mingi
na pia rangi ya paa la getini inaoana na ya paa la nyumba na
hivyo kuvutia.
· Njia
nyingine ya kuleta mvuto getini ni kuweka taa, au hata kama taa zipo ni kwamba
wenye nyumba wengi wanakuwa na mtindo mmoja wa taa kwa miaka mingi wakati
mitindo mipya inakuwa ipo sokoni. Mbali na ulinzi na usalama taa za getini
zinaleta mvuto pale mwanga unapomulika kwenye miti, maua, nyumba na hata njia
iliko.
· Ongeza
mvuto wa mbele ya lango kuu kwa kuweka urembo wa mawe yawe ni ya asili ama ya
kutengenezwa viwandani. Mawe haya ndio sanaa pekee unayoweza kuweka kwenye
ukuta wa getini mbele ya nyumba na kuwa na amani kuwa mwizi hawezi kuyaiba kwakuwa yanajengewa mlemle ukutani
tofauti na sanaa nyingine ambayo ungeweza kuitundika na ikaibiwa. Chagua mawe
au urembo ambao unaendana na sehemu nyingine ya nyumba.
· Mara
kwa mara tunza geti kwa kulipaka rangi ili lisionekana kukukuu, kwakuwa eneo
lililopo bila shaka linapatwa na shurba
nyingi ambazo ni pamoja na upepo mkali. Usiruhusu muonekano wa geti uwe na
rangi yenye mikwaruzo. Kama kanuni nyingine zozote za rangi, paka rangi inayotakiwa
kwa eneo hilo iwe ni geti la mbao au chuma au mchanganyiko wa mbao na chuma.
Rangi ya geti inavyokuwa mpya na ya kupendeza moja kwa moja nyumba nzima
inavutia. Na rangi ipakwe baada ya matengenezo yoyote yanayohitajika kukamilika
kwanza.
· Endapo
eneo linaruhusu pandikiza ukanda wa maua getini kwako, huku ukitengeneza ukuta mfupi
wa kuvutia kuzunguka kitanda cha maua hayo. Ukuta huo unaweza kuwa wa mawe ya
asili ama wa saruji tupu na kupakwa rangi. Kwenye maua yako changanya makubwa
kwa madogo. Vilevile kama kuna uwezekano wa kutundika vyungu vya maua basi
fanya hivyo
· Weka
kengele yenye hadi ya nyumba yako.
· Tengeneza
sakafu ngumu getini kwenye njia ya kuingilia nyumbani. Hii sio tu itasaidia
eneo lisiwe chepechepe na tope wakati wa mvua bali pia italeta mvuto kwani mawe
ya kutengeneza sakafu ngumu ni mengi ya maumbo na rangi mbalimbali.
Kwa
maoni au maswali tembelea www.vivimachange.blogspot.com
No comments:
Post a Comment