MGOMBEA Urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Edward Lowassa, ambaye anaungwa mkono na vyama vya upinzani
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), jana alitangaza kuitua mbeleko
aliyokuwa akimbebea Mgombea Ubunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la
Monduli, Namelok Sokoine.
Vyama vinavyounda Ukawa ni pamoja na Chadema yenyewe,
Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na National League for Democracy (NLD).
Lowassa alitangaza uamuzi wake huo katika mkutano wa
kampeni uliofanyika Uwanja wa Barafu, uliopo Mto wa Mbu, Wilaya ya Monduli,
baada ya baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano huo kumhoji namna
anavyowaacha na Namelok ambaye ni mtoto wa Waziri Mkuu wa zamani, Hayati Edward
Moringe Sokoine.
Akijibu swali hilo, Lowassa alisema atakutana na Namelok
kumshawishi ili abadili msimamo wake wa kuendelea kuwa CCM na badala yake
ajiunge naye kwenye vuguvugu na mabadiliko katika Ukawa.
“Nimeongoza jimbo hili kwa miaka 20, nastahili kumfahamu
atakayekuja badala yangu, sasa kuna maneno maneno, wamepotea mabasi, wamepotea
malori, niachieni kidogo nifanyie kazi.
“Kesho nitakwenda Pemba nitarudi jioni, nitakutana na
madiwani na Namelok ili mambo yetu tuliyoongea tuulizane yamekuwaje. Nasema
hivyo kwa sababu nisingetaka kuvunja umoja wetu. Katika uchaguzi uliopita
tulikuwa na kauli, ‘tulihuzunika pamoja, tulifurahi pamoja na tutasonga mbele
pamoja,’ ningependa tubaki na kauli hiyo, kwa hali hiyo, hili mniachie kesho
tutakubaliana, akikataa kuingia basi la wengi, basi itakuwa bahati mbaya,”
alisema Lowassa.
Lowassa alitumia pia mkutano huo kumnadi Mgombea Ubunge
wa Chadema wa Jimbo la Monduli, Julius Kalanga, akimtaja kuwa ni jembe huku
akikwepa kumtaja kwa namna ya kumshambulia kisiasa au kuwashawishi wapigakura
kutomchagua Namelok.
Baadaye jioni Lowassa alifanya mkutano wa kampeni zake
huko Babati, mkoani Manyara na kueleza kuwa Serikali yake itakuwa rafiki kwa
mama ntilie, bodaboda na watu wote ambao wanahangaika kutafuta maendeleo.
“Katika serikali yangu mtu atakayesumbua hawa watu, mtu
anaingiza daladala yake barabarani anakamatwa huyo atakayemkamata nitamfunga,
najua watasema mimi ni dikteta, lakini ni dikteta wa maendeleo,” alisema
Lowassa.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye,
ambaye amekuwa bega kwa bega na Lowassa katika shughuli za kampeni, alisema
anawashangaa baadhi ya viongozi wa CCM wanaodai kuwa amekuwa akiilalamikia
serikali wakati aliwahi kuwa huko.
Alisema alipotoka madarakani mwaka 2005 bei ya sukari
ilikuwa Sh 500, lakini hivi sasa haikamatiki.
“Nilipoondoka niliacha unga wa sembe ukiwa Sh 200, lakini
leo haukamatiki, mchele Sh 600 lakini leo haukamatiki, kipande cha sabuni Sh 50
lakini leo hakikamatiki. Nimeondoka huko kwa kuwa serikali imeshindwa kujibu
hayo mambo,” alisema Sumaye.
Akimzungumzia Namelok, Sumaye alimtaja mwanasiasa huyo
kijana kuwa ni mdogo, ndugu yake na kwamba hana ugomvi naye, lakini kwa sababu
anagombea ubunge kupitia gari ambalo halina matairi afahamu kuwa yupo kwenye
genge ambalo halifai.
“Tutaongea naye aachane na hiyo kambi ya kijani aje, msije
mkampigia kura kwa sababu hatashinda, aje aungane na Lowassa. Lowassa atashinda
kwa zaidi ya asilimia 80, Magufuli mwenyewe amekata tamaa na CCM ndiyo maana
anasema ni kitanda chenye kunguni, CCM ni chama kilichojaa rushwa, ufedhuli,
Namelok kwa kuwa bado ni binti msikivu tutaongea naye,” alisema Sumaye.
Mkutano wa kwanza wa Lowassa
akiwa mpinzani
Lowassa, ambaye amekuwa Mbunge wa Monduli kwa miaka 20,
jana alifanya mkutano wa kwanza katika Jimbo la Monduli akiwa chama cha
upinzani.
Licha ya mkutano wake wa jana kupangwa kufanyika saa 5:00
asubuhi, tangu saa 1:30 asubuhi wananchi walianza kujitokeza uwanjani, huku
Lowassa mwenyewe akifika eneo la mkutano saa 7:58 mchana.
Akizungumza juu ya uongozi wake jimboni hapo na hatima
yake, alisema: “Nimesema napita Mto wa Mbu niwapungie mkono kwa sababu nitakuja
kuaga rasmi, watu uliokaa nao miaka 20 huwaagi hivi hivi. Nilishawahi
kusema watu tulihozunika pamoja tutafurahi pamoja.
“Nataka kila mwana Monduli anitafutie kura popote
Tanzania, ni muhimu kupata kura nyingi mno. Hawa jamaa ni mahodari wa kuiba
kura kwa hiyo lazima tupate kura nyingi,” alisema Lowassa.
Alisema kwa sasa hatakuwa tena mbunge wa jimbo hilo,
ila atakuwa mbunge wa zamani wa Monduli, hivyo anataka kuendelea kushirikiana
nao katika kutatua matatizo ya jimbo hilo.
“Nataka Monduli iendelee kubaki na amani ile ile,
tusaidiane, tuzikane, hata asiyekuwa kwenye chama chetu tumuelimishe siyo
kutengana, tuache ugomvi kati ya wakulima na wafugaji,” alisema.
MTANZANIA
No comments:
Post a Comment