Umechoka na nguo zako
kusinyaa, kupauka au kuchuja? Kuna suluhisho moja kuu: Acha kuziweka kwenye
maji huku umefumba macho! Yafuatayo ni mambo 12 ya kufanya kusaidia nguo zako
kudumu ziwe ni mpya au za zamani. Mambo haya unapaswa kuyafanya kwenye nguo
unazotaka kufua kabla ya kuanza rasmi zoezi hilo, na haijalishi kama utazifua
kwa mkono au kwa mashine.
· Kwanza kabisa soma maelekezo ya karatasi iliyopo
kwenye nguo kuhakikisha kuwa haisemi kuwa nguo husika inatakiwa isafishwa kwa
mafuta maalum tu (dry clean only). Wataalam wanasema kama nguo haijasema kuwa
ni dry clean tu, basi unaweza kuifua
kwa mafanikio kabisa nyumbani.
· Chambua nguo unazotakuta kufua. Maana yake ni Rangi
za kuchuja nyingi zinaonekana kwa macho. Kama una wasiwasi jaribu eneo dogo la
ndani kwa kulipaka maji, halafu chukua kipande cha pamba upafikiche. Kama rangi
nyeupe ya pamba itabadilika hata kwa mbali sana, basi fahamu moja kwa moja kuwa
nguo hiyo inachuja.
Tenga rangi zinazofanana pamoja, nguo kwa mfano
jeans za bluu zina tabia ya kutoa maji yenye ubluu kwa mbali, kama
utazichanganya na nguo za rangi nyingine bila shaka baada ya muda rangi halisi
ya zile nyingine itapotea. Zaidi ya kutenganisha nguo za mwanga na zile za
rangi za giza, unatakiwa pia kutenganisha nguo kwa kiwango cha uchafu, kwa mfano,
huenda nguo zote ni nyeupe lakini moja ina udongo zaidi ya nyingine hapo
itakubidi kutenganisha hizo mbili.
· Rekebisha matatuko. Ni muhimu kushona nguo pale palipotatuka
kama vile mapindo ya magauni na suruali na pia kurudishia vifungo vilivyotoka
kabla ya kuzifua.
· Hakikisha una sabuni sahihi. Endapo unafua na
mikono kwa mfano, sabuni za unga na maji zinafaa zaidi kwa kuloweka nguo kuliko
zile za mche. Vilevile sabuni zinazosema nguvu mara dufu unakuta kuwa kiasi
kinachotumika ni kidogo kuliko zile zisizoandikwa hivyo. Ilihali zile
zilizoandikwa kawaida zinafaa zaidi vitambaa laini na nyororo ambavyo
havihitaji nguvu kubwa. Vivyohivyo kwa dawa za kugharisha na kuondoa madoa.
· Tafuta na shughulikia madoa nguo chafu ingali bado
kavu, kabla hujaitumbukiza yote kwenye maji. Hii ina maana kwamba nguo ikiwa
kavu ni rahisi doa kuonekana kwani kuna madoa yakishaingia kwenye maji
yanapotelea sio rahisi kuyaona hadi pale nguo inapokuwa kavu tena. Hata hivyo
ni vyema kukumbuka kuwa kanuni kuu ya madoa inasema yashughulikie punde baada
ya kutokea. Endapo nguo unayotoa doa ni ya rangi tumia blichi ya kutoa madoa ya
nguo za rangi na endapo ni nyeupe basi tumia blichi ya rangi nyeupe. Fuata
maelekezo ya kwenye chupa.
· Angalia kama nguo ina pini zozote ama karatasi za
bei toka dukani na uzitoe.
· Kagua mifukoni hakikisha hakuna chochote na kisha
ifungue nje ndani na pia kama ni soksi zigeuze nje ndani.
· Ondoa mikanda na Kwa zile nguo ambazo zina kamba,
legeza kamba zake ili kuwezesha kutakata kila mahali kwenye yake marinda na pia
kuondoa mikunjokunjo.
· Tenga nguo dhaifu pembeni. Nguo hizi ni kama zile
za ndani, soksi aina ya stocking na zile nguo zenye wavuwavu eneo kubwa.
· Geuza nje ndani nguo zote unazoona kitambaa chake
au maandishi yanaweza kuharibiwa na mfikicho, kusababisha nyuzi kutokatoka na
pia kusababisha mpauko.
· Fungua vifungo vyote na pia nyoosha kola
· Loweka zinazotakiwa kufanyiwa hivyo kwanza. Maji
na sabuni yanatosha kuondoa uchafu mwingi hasa ule ambao haujakomaa. Hata madoa
ambayo ni ya muda kiasi yanapungua pale nguo zinapolowekwa. Loweka nguo ambazo
ni chafu sana kwenye ndoo kubwa, karai au sinki la kufulia kwa angalau saa
nzima kabla hujaanza kuzifua.
Makala hii
imeandaliwa na Vivi.
Je, unauza
bidhaa au huduma inayohusu usafi wa nguo ambayo unataka Watanzania waijue?
Nijulishe simu/whatsapp 0755200023
www.vivimachange.blogpot.com
No comments:
Post a Comment