Sakafu nyeusi naona kama inaonyesha ufahari na ukisasa...wee unaonaje? Sema nami..
NYONGEZA YA MAKALA:
Ulishawahi Kufikiria kuwa na sakafu nyeusi?
Iwe ni sakafu nyeusi ya zulia, marumaru au mbao bila
shaka kuna hisia unayopata ukiingia ndani ya nyumba ambayo ina sakafu nyeusi.
Sakafu nyeusi wengi wanaishangaa kwa umaridadi wake, wakati wengine wanaweza kuionea
aibu, kwa kufikiria kuwa inafanya chumba kiwe cha giza ama kama pango.
Hakuna
rangi ya sakafu ambayo ni sahihi, yoyote utakayoamua ni kiasi cha kuwa na
sababu zinazokufanya uichague.
Sakafu nyeusi inaweza kufanya nyumba yako ing’ae kuendana
na rangi utakazochagua kwenye maeneo mengine kwa vile ya fenicha, kuta, pazia
na dari. Kama ulikuwa unashangaa ni kwa namna gani unayoweza kuwa na sakafu
nyeusi basi hizi hapa ni diondoo za kukuwezesha kufanya uamuzi:
Kabla hujaamua kuwa na sakafu nyeusi, kwanza unatakiwa
ujiulize maswali haya.
Ni nini unachopendelea?
Ni ipi staili ya nyumba yako pamoja na mapambo yake?
Ni kiasi gani cha pilika kipo ndani ya nyumba?
Ni kwa mara ngapi unasafisha nyumba yako?
Ukubwa wa vyumba ukoje? Unapata mwanga kiasi gani? Kuta zina
au zitakuwa na rangi gani na je utabadilisha rangi hiyo baadaye?
Ni zipi rangi za makabati na fenicha nyingine utakazoweka
ndani ya nyumba yako?
Sakafu nyeusi ina tabia ya kufanya chumba kionekane
kidogo. Hata hivyo inatakiwa kuwa na rangi za mwanga maeneo mengine ya chumba
ili kuleta muonekano wa ukweli wa ukubwa wa chumba.
Sakafu nyeusi inafanikiwa zaidi kwenye nyumba kubwa na
yenye vyumba vikubwa na maeneo mengi ya wazi ndani na hata kama ni ujia
kwamfano, uwe mpana. Kama utaamua kuwa na sakafu nyeusi hakikisha ndani una
mwanga wa kutosha na sio ule wa jua tu bali hata wa taa za madukani.
Sakafu nyeusi zinaficha “udhaifu” vizuri zaidi. Kwa mfano
ikizeeka uwezekano wa kuona vitundu au madoa ni mdogo. Na hata ile kusinyaa na
kutanuka kwa ardhi ambapo inaweza kuleta ufa kwenye marumaru endapo umeweka nyeusi
ni ngumu kuona ufa ule, ingawaje hata hivyo unaweza kufanya marekebisho kwa
kuondoa marumaru iliyopata ufa na kuweka nyingine nzima.
Mbinu nyingine ya kufanikiwa na sakafu nyeusi ni kutupia
kizulia cha rangi nyingine juu yake endapo utataka kupunguza ule weusi. Hii
italeta mpishano wa rangi ambapo itatengeneza mvuto.
Pia unaweza kuwa na sakafu nyeusi chumba kimoja na ya
rangi ya mwanga chumba kingine. Kwa mfano, wakati chumba cha chakula kikiwa na sakafu
ya mwanga kile cha jikoni kikapishana nacho kwa kuwa na sakafu nyeusi. Hii
inapendeza zaidi pale vyumba vinapokuwa vimefuatana.
Salafu nyeusi ina tabia ya kuonyesha ufahari na umaridadi
hasa pale rangi za ndani za maeneo mengine ya chumba chenye sakafu hiyo zinavyokuwa
zimepangiliwa vyema na kuleta mwanga wa kutosha, bila shaka hutajutia kuwa
nayo.
Sakafu yoyote iwe nyeusi au ya mwanga zote zinafaa, ni
wewe tu kuchagua ni ipi sahihi kwa nyumba yako.
Makala hii imeandaliwa na Vivi.
Je, unauza bidhaa au huduma
inayohusu nyumba na bustani ambayo unataka Watanzania waijue? Nijulishe
simu/whatsapp 0755200023 au nifuate instagram: vivimachangeblog
No comments:
Post a Comment